Na Mwandishi Wetu, MorogoroJeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza mazingira ya kifo cha kijana mmoja aliyefariki dunia ndani ya nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya Morogoro.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema marehemu ambaye ametambuliwa kwa jina la Gidioni Mbwambo (34), mkazi wa Manispaa ya Morogoro, alikutwa amefariki dunia ndani ya chumba alichokuwa amepanga katika nyumba ya kulala wageni ya Kisanga, iliyopo Mtaa wa Nguzo, Kata ya Mazimbu.Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, tukio hilo lilitokea Januari 27, 2026 majira ya asubuhi, huku marehemu akiwa amefika katika nyumba hiyo Januari 26, 2026 na kupanga chumba namba 106.Amesema tukio hilo liligundulika baada ya wahudumu wa nyumba hiyo kubaini dalili zisizo za kawaida nje ya chumba hicho, hali iliyosababisha kutoa taarifa kwa uongozi na baadaye kwa Jeshi la Polisi.“Baada ya hatua za kiusalama kuchukuliwa na uchunguzi wa awali kufanyika, ilibainika kuwa marehemu alikuwa tayari ameshafariki dunia. Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo kamili cha tukio hilo,” amesema Kamanda Mkama.Aidha, amesema taarifa za awali zinaonyesha marehemu alikuwa katika hali isiyo ya kawaida kabla ya tukio hilo, na uchunguzi unaendelea ili kupata ukweli zaidi.Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni kuendelea kuzingatia taratibu za usajili na utambuzi wa wageni wao, ili kurahisisha hatua za kiusalama na uchunguzi pindi matukio yanapotokea.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, ametuma ujumbe mzito wa rambirambi kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mwanzilishi wa chama hicho, Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei, akimtaja kama mjenzi wa taifa, kiongozi wa mfano na hazina ya historia ya Tanzania.
Katika ujumbe wake alioutoa akiwa Gereza Kuu la Ukonga, Lissu amesema kifo cha Mzee Mtei ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na wanachama wa CHADEMA, bali kwa taifa lote la Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa taifa, uchumi na demokrasia.
Lissu ameeleza kuwa marehemu Mtei alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa misingi ya uchumi wa Tanzania baada ya uhuru, akihudumu kama Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na baadaye Waziri wa Fedha, ambapo jina na saini yake zilionekana kwenye noti za kwanza kabisa za taifa.
Akizungumzia uadilifu wake, Lissu amesema Mzee Mtei alionesha ujasiri wa kipekee wa kisiasa pale alipothubutu kumshauri Mwalimu Julius Nyerere kubadili sera za kiuchumi za Azimio la Arusha baada ya kubaini kuwa zilikuwa zimeshindwa, na baadaye akaamua kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Fedha kwa misingi ya dhamira na uaminifu kwa nchi.
“Huu ndio uzalendo wa kweli. Mzee Mtei hakutafuta madaraka, bali alisimamia ukweli na maslahi ya taifa,” amesema Lissu katika ujumbe wake.
Kuhusu mchango wake ndani ya CHADEMA, Lissu amesema marehemu alikuwa mfano wa uongozi wa kujitolea, kwani hakuwahi kupokea mshahara, posho wala kunufaika binafsi kupitia nafasi yake ya uongozi ndani ya chama.
Ameongeza kuwa Mtei aliimarisha utamaduni wa uongozi wa kupisha damu changa, alipostaafu uenyekiti wa chama mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 66, jambo linaloendelea kuifanya CHADEMA kuwa chama chenye misingi ya kidemokrasia.
Lissu pia amemsifu marehemu kwa kuchapisha kitabu chake cha maisha “From Goatherd to Governor” mwaka 2009, akisema kitabu hicho kimekuwa hazina muhimu ya historia ya kisiasa na kiuchumi ya Tanzania.
Akihitimisha ujumbe wake, Lissu amesema badala ya kuomboleza kifo cha Mtei, Watanzania wanapaswa kusherehekea maisha yake yenye maana, busara na mchango mkubwa kwa taifa, huku akimuombea apumzike kwa amani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani, Mzee Edwin Isaac Mbiliewe Mtei, aliyefariki dunia usiku wa tarehe 19 Januari, 2026 jijini Arusha.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Samia alisema kifo cha Mzee Mtei ni pigo kubwa kwa taifa kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa uchumi na uongozi wa nchi. Rais alitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote walioguswa na msiba huo.
Rais Samia alimtaja Mzee Mtei kuwa miongoni mwa watumishi na viongozi waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha misingi ya uchumi wa taifa, hususan kupitia nafasi yake kama Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (1966–1974), ambapo alishiriki katika kuweka mifumo imara ya fedha na taasisi za kifedha nchini.
Aidha, Rais alieleza kuwa marehemu ataendelea kukumbukwa katika historia ya siasa za Tanzania kama mmoja wa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama vingi na kiongozi aliyetoa mchango mkubwa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akitambuliwa kwa misimamo yake na uadilifu katika uongozi.
Rais Samia pia aliwahimiza Watanzania kuendelea kujifunza kutoka katika maisha na falsafa ya Mzee Mtei, ikiwemo kupitia maandiko yake binafsi (autobiografia), ambayo yanaeleza safari yake ya maisha na mchango wake katika kujenga taifa.
Akihitimisha, Rais aliomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi na kuwapa familia, ndugu na taifa kwa ujumla faraja, nguvu na amani katika kipindi hiki cha majonzi.
Taarifa hiyo imesainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, na kutolewa rasmi Zanzibar tarehe 20 Januari, 2026.
Mwanahabari Joachim Ernest Mushi amefiwa na mama yake mzazi, Mecktilda Joseph Lugazu, aliyefariki dunia Januari 6, 2026, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya General Jijini Dodoma, tukio lililoacha simanzi kwa familia, ndugu, jamaa na wadau wa tasnia ya habari.Kwa mujibu wa taarifa za familia, taratibu za msiba zinaendelea kufanyika nyumbani kwa marehemu Kifuru–Kinyerezi jijini Dar es Salaam, ambako waombolezaji wanaendelea kujitokeza kutoa pole na faraja kwa familia iliyopatwa na msiba huo.
Imeelezwa kuwa mwili wa marehemu utasafirishwa kutoka Dodoma kuelekea Uru Mawela, mkoani Kilimanjaro, siku ya Januari 9, 2026, kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku inayofuata.
Mazishi ya marehemu Mecktilda Joseph Lugazu yanatarajiwa kufanyika Januari 10, 2026, nyumbani kwao Uru Mawela, huku familia ikitoa shukrani kwa wote wanaoendelea kutoa pole na kuomba dua ili Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
Dodoma, Tanzania – 12 Desemba 2025Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea jijini Dodoma.
Kupitia taarifa yake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo mzito na kutoa pole kwa Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki.
Rais Samia amemuelezea Marehemu Mhagama kama kiongozi shupavu na mtumishi wa umma aliyejitoa kwa moyo wake wote kwa kipindi cha zaidi ya miaka 38 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katika safari yake ya kisiasa, Mhagama aliwahi kuwa kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali za serikali, pamoja na kuwa mshauri wa wanasiasa na wananchi wengi.
“Kwa miaka 38, Mheshimiwa Mhagama amekuwa mwanachama mahiri wa CCM, kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali na mnasihi wa wengi katika siasa na maisha,” amesema Rais Samia katika salamu zake.
Rais Samia amewaombea wafiwa faraja katika kipindi hiki cha majonzi na kumkabidhi marehemu kwa Mungu, akisema: “Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.”
Mipango ya mazishi inaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Bunge na familia ya marehemu, na taarifa zaidi zinatarajiwa kutolewa.

Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ametoa wito kwa Wakenya kuendeleza misingi ya haki, uhuru na demokrasia aliyoisimamia marehemu Raila Odinga, akisisitiza kuwa mapambano hayo hayawezi kurudi nyuma.
Akizungumza katika shughuli ya kuuaga mwili wa Odinga kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Uhuru alisema, “Hatutakubali kama Wakenya haki za binadamu, demokrasia na mambo yote ambayo Raila alitetea yarudi nyuma. Tutasonga mbele tukiyalinda kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.”
Uhuru pia alikumbushia uhusiano wake wa karibu na Raila, akimtaja kama kiongozi shupavu aliyepigania haki za wananchi bila woga.
Mazishi ya Raila Odinga yanatarajiwa kufanyika Jumapili, Oktoba 19, 2025, nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, magharibi mwa Kenya.









































































