Na Mwandishi Wetu.

Serikali imetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe wa muziki wa bendi, Steven Hiza, kilichotokea jijini Tanga, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akimuelezea marehemu huyo kuwa msanii mahiri aliyeacha alama kubwa katika tasnia ya muziki na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Samia alimtuma salamu hizo kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, akisisitiza kuwa mchango wa marehemu katika kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii kupitia sanaa hautasahaulika. Alibainisha kuwa Hiza alitumia muziki kama chombo cha kuimarisha maadili, umoja na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa marehemu aliwahi kulitumikia kundi la muziki la Atomic Jazz Band, ambapo alijipatia umaarufu mkubwa kupitia nyimbo zake zilizojaa ujumbe wa uzalendo na mshikamano wa kitaifa, ikiwemo wimbo uliogusa hisia za wengi kuhusu mapenzi ya nchi. Serikali imetambua mchango huo kama sehemu ya historia ya maendeleo ya muziki wa Tanzania.

Rais Samia pia aliwataka wanamuziki na wadau wa sanaa nchini kuuenzi mchango wa marehemu kwa kuendeleza misingi ya ubunifu, uzalendo na uwajibikaji katika kazi zao za kisanaa, akisisitiza kuwa sanaa ni nyenzo muhimu ya kujenga jamii yenye maadili na mshikamano.

Aidha, Rais ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wanamuziki na Watanzania wote, akiwaombea uvumilivu na moyo wa subira katika kipindi hiki cha maombolezo, huku akimuombea marehemu apumzike kwa amani.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: