Afisa Uchunguzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, THBUB ofisi ya Zanzibar, Bw. Abdullatif Ali Sheha (kushoto aliyesimama) akiwasilisha mada ya “Haki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora” kwa wananchi wa kijiji cha Dunga Kiembaeni, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Afisa Sheria, Wilfred Msagati akiwasilisha mada ya “majukumu ya THBUB” katika mkutano wa pamoja baina ya Tume hiyo na wananchi wa Shehia ya Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Naibu Sheha wa Shehia ya Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Kesi Makame Mussa akiwakaribisha wanashehia wa kijiji hicho (hawapo pichani) katika mkutano wa pamoja baina yao na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).
Na Mwashamba Juma, Zanzibar.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ofisi ya Zanzibar imeendesha mkutano wa elimu kwa wananchi wa Shehia ya Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ukiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili waweze kuzitambua na kuzilinda.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Sheria wa THBUB, Wilfred Msagati, aliwahimiza wananchi kutambua haki zao na kuzitetea pale zinapovunjwa, huku akiwaelekeza kufika Tume kuwasilisha malalamiko yao ili yapatiwe ufumbuzi kwa mujibu wa sheria. Alieleza kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kulinda haki za binadamu zikiwemo haki za watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Msagati aliongeza kuwa pamoja na kupokea na kuchunguza malalamiko, Tume ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu, kuelimisha jamii kuhusu wajibu wao na kusambaza elimu ya utawala bora nchini. Pia alibainisha kuwa Tume hutembelea maeneo mbalimbali ya vizuizini kama magereza, vituo vya kulelea watoto yatima na makazi ya wazee ili kutoa elimu na kufuatilia hali ya haki za binadamu.
Kwa upande wake, Afisa Uchunguzi wa THBUB Zanzibar, Abdullatif Ali Sheha, alisema mkutano huo ulilenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua ukiukwaji wa haki na misingi ya utawala bora pamoja na kuwafundisha namna ya kuwasilisha malalamiko yao rasmi kwa Tume ili yashughulikiwe kwa ufanisi.
Wananchi wa Dunga Kiembeni waliishukuru THBUB kwa kuwafikia vijijini na kusikiliza changamoto zao. Katika mkutano huo, jumla ya malalamiko manne yalipokelewa, matatu yakihusu uvunjifu wa haki za binadamu na moja likihusu ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, huku wananchi wengine wakiahidi kufika ofisini kuwasilisha malalamiko zaidi.




Toa Maoni Yako:
0 comments: