Na Mwandishi Wetu
Mwanasiasa na msomi wa Tanzania, Profesa Mark James Mwandosya, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano, wakati wa ziara yake jijini Maputo nchini Msumbiji, akieleza kuwa mkutano huo ulikuwa wa heshima kubwa na wenye manufaa ya kihistoria na kielimu.
Prof. Mwandosya amesema alipata fursa ya kujadili kwa kina historia ya harakati za ukombozi wa kusini mwa Afrika pamoja na changamoto zilizojitokeza baada ya nchi nyingi kupata uhuru. Ameeleza kuwa maelezo na uzoefu wa Chissano, ambaye anaheshimika kimataifa kwa uongozi wake wenye busara na mchango wake katika kudumisha amani, yamempa mwanga mpana kuhusu historia ya ukombozi wa bara hilo.
Katika mazungumzo hayo, Prof. Mwandosya alimkabidhi Rais huyo mstaafu nakala ya kitabu chake kiitwacho 38 Reflections on Mwalimu Nyerere, kinachobeba tafakuri mbalimbali kuhusu maisha na mchango wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere. Amesema kitabu hicho ni sehemu ya juhudi za kuendeleza kumbukumbu za uongozi bora na falsafa za maendeleo zilizoasisiwa na Mwalimu.
Prof. Mwandosya amebainisha kuwa kukutana na viongozi wakongwe wa ukombozi ni njia muhimu ya kujifunza na kutafakari safari ya maendeleo ya Afrika, akisisitiza kuwa elimu na uzoefu vinaendelea kujengwa hata baada ya viongozi kung’atuka madarakani.
Amehitimisha kwa kumshukuru Rais Mstaafu Chissano kwa mapokezi na mazungumzo yenye manufaa, akieleza kuwa mafunzo aliyopata yataendelea kuwa mchango muhimu katika tafakuri za maendeleo, historia na uongozi barani Afrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments: