TRENDING NOW

/>
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wenyekiti wa kamati ya kitaifa ya uratibu wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 akizungumza katika kikao cha kamati hiyo, ofisini kwa Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Oktoba 21, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Atangaza timu za mikoa za kusimamia fedha hiyo

*Asisitiza hakuna kulipana posho, ahimiza tathmini zifanyike kila mara

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Wakuu wa Mikoa yote nchini wanapaswa kusimamia kwa karibu fedha maalum ya sh. trilioni 1.3 zilitolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuimarisha huduma za jamii.

“Kule mikoani kutakuwa na kamati maalum na Mkuu wa Mkoa ndiye atakuwa Mwenyekiti wake na Katibu Tawala atakuwa Katibu wao. Pia kutakuwa na mchumi, Mhandisi wa Mkoa, Afisa Manunuzi, Afisa Elimu, Mganga Mkuu wa mkoa, Mwanasheria, Mratibu wa Sekta na tumemuongeza Mhandisi wa TARURA kwani atahitajika japo hayumo kwenye sekretarieti ya mkoa,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Alhamisi, Oktoba 21, 2021) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma wakati alipokutana Mawaziri na Makatibu Wakuu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia miradi ya fedha za kuimarisha huduma za jamii.

Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, amesema Kamati za Ulinzi za Mikoa (KUU) zitakuwa na jukumu la kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo na kama kutakuwa suala rushwa wataingia na kuchukua hatua. “Katika kipindi cha miezi tisa, tunatakiwa tuwe tumekamilisha hii miradi,” amesisitiza.

Amesema timu hiyo ndiyo itawajibika kwenda maeneo ya vijijini kuona kama kazi inafanyika kwa viwango vinavyotakiwa kwani kuna baadhi ya miradi utekelezaji wake unapaswa uwe umekamilika ndani ya miezi mitatu.

“Mkoa utaamua ni mfumo gani utumike kusimamia utekelezaji miradi kwenye wilaya zake. Waheshimiwa Mawaziri lazima mwende kukagua miradi hii kulingana sekta zenu na mkifika mkoani ni lazima muambatane na Afisa mhusika kutoka mkoani,” amesema.

Amesema Makatibu Wakuu pia wanapaswa kwenda kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo lakini kwa kupeana zamu na Mawaziri wao. “Hii ndiyo Kamati inayosimamia hizi fedha, kwa hiyo tunatakiwa tusimamie miradi yote ya kisekta ili ikamilike ndani ya miezi tisa kama ilivyopangwa. Mheshimiwa Rais ameshasema, sisi kazi yetu ni kuhakikisha kwamba inakamilika. Tusipokwenda hakuna ambaye atawajibika.”

Waziri Mkuu amesema watendaji wa vijiji na kata nao wana wajibu wa kusimamia miradi hiyo huko huko waliko na kusisitiza kuwa wahandisi wahakikishe viwango vya majengo vinaendana na fedha zilizotolewa. Amesema mafundi wanaoajiriwa wapewe mikataba ili wasikimbie kazi.

Kuhusu manunuzi ya vifaa vitakavyotumika kwenye miradi hiyo, Waziri Mkuu amewataka wahakikishe wanatumia ledger. “Manunuzi haya si ya kutoa fedha mfukoni yakaishia hapo. Ni lazima kuwe na ledger. Nimebaini kwenye miradi mingi, BOQ zinaandaliwa lakini kwenye manunuzi, bei inakuwa tofauti na miradi inakwama kukamilika.”

“Kwenye miradi hii, wakinunua vifaa kuwe na daftari la makabidhiano baina ya mnunuzi na Kamati ya Usimamizi. Vifaa vikishanunuliwa ni lazima vikabidhiwe kwa Kamati,” amesisitiza.

Kuhusu posho, Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa amesema: “Hakuna mtu anayepaswa kudai posho katika hii kazi. Tukifanya hivyo, hii miradi haitakamilika. Hata sisi hapa kwenye Kamati hii, Mheshimiwa Rais hajatoa posho, sana sana ametuongezea majukumu,” amesisitiza.

Mapema, akiwasilisha mchanganuo wa sh. trilioni 1.3 zilitolewa na IMF, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema fedha hizo zimetolewa kulingana na sekta. Sekta hizo ni maji, afya, elimu, utalii, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hifadhi ya jamii (social protection) ambako kuna TASAF, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Sekta ya maji imepangiwa sh. bilioni 139.4, afya (sh. bilioni 466.9), elimu (sh. bilioni 367.6), utalii (sh. bilioni 90.2), Zanzibar (sh. bilioni 231), TASAF (sh. bilioni 5.5), vijana, wanawake na wenye ulemavu (sh. bilioni 5) na uratibu sh. bilioni 5,” alisema.

Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ya Kitaifa ni Waziri wa Nchi, OWM – Sera Bunge na Wenye Ulemavu, Waziri wa Fedha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Maji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.
Na. Beatrice Sanga- Maelezo Oktoba 21, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono Sekta binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi katika kuhakikisha sekta binafsi inashiriki ipasavyo katika kukuza uchumi wa nchi na kujenga uchumi jumuishi ili kuchochea uchumi na kukuza ajira na kipato kwa wananchi.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wenye lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta binafsi ili kutoa hamasa kwa sekta hiyo kushiriki ipasavyo katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.

Katika hotuba yake Waziri Mwambe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Shilingi Trilioni 1.3 kwa ajiri ya kukabiliana na athari za Uviko -19 ambapo fedha hizo zimelenga kuleta ustawi katika sekta mbalimbali za huduma ikiwemo elimu, afya, maji na utalii.

“Naomba nitumie fursa hii, kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake kubwa aliyoionesha katika mapambano dhidi ya Uviko-19 kwa kuwezesha upatikanaji wa Shilingi Trilioni 1.3 ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ili kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19”, Amesema Mwambe
Mwambe ameeleza kuwa, utekelezaji huu, utahusisha manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali hivyo sekta binafsi itahitajika kushiriki ipasavyo ambapo bidhaa na huduma zinazohitajika ni pamoja na vifaa vya ujenzi, mashine na vifaa mbalimbali vya hospitali, elimu na maji, ujenzi na ukarabati wa majengo ya shule, vyoo na hospitali, ujenzi wa maeneo ya kufanyia bishara kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu pamoja na ujenzi na ukarabati wa mtandao wa barabara katika hifadhi za wanyama na ukarabati wa maeneo ya urithi na kutoa vivutio kwa wawekezaji katika tasnia ya utalii.

Ameongeza kuwa Utekeelezaji wa miradi hiyo utachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta binafsi nchini kwa kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa mpango hivyo ni wakati muafaka kwa sekta binafsi kujipanga kuhakikisha inatumia fursa hiyo kushiriki katika utekelezaji wa mpango na kuchangia katika kufanikisha jitihada za serikali za kukuza uchumi na kuzitaka sekta binafsi kudhalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora na viwango vinavyohitajika na soko.

“Nichukue fursa hii kuwaomba na kuwakumbusha sekta binafsi kuhakikisha inatekeleza wajibu wake kwa kufanya kazi zenye viwango kulinganana na mahitaji ya soko na uzalishaji wa bidhaa zenye kukidhi viwango vinavyohitajika na kutosheleza na kukidhi mahitaji ya utekelezaji wa mpango, hatua hii itawezesha bidhaa na huduma zinazotolewa na watanzania kuwa shindani katika bei na ubora wa bidhaa” Amesema mwambe

Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 ulizinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 10 Oktoba, 2021 Jijini Dodoma, Ambapo shilingi trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zimelenga kuleta ustawishaji katika sekta za huduma ikiwemo Elimu, Afya, Maji na Utalii.

Kati ya fedha hizo, TZS bilioni 139.4 zinaenda kutekeleza miradi katika sekta ya maji; TZS bilioni 466.9 zinaenda sekta ya elimu; TZS bilioni 64.9 zinaenda Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; TZS bilioni 302.7 zinaenda Ofisi ya Rais-TAMISEMI; TZS bilioni 5.0 zinaenda kwa ajili ya uwezeshaji wananwake, vijana na wenye ulemavu; TZS bilioni 5.5 zinaenda kwa kaya maskini; TZS bilioni 90.2 zinaenda sekta ya utalii; TZS bilioni 231.0 zinaenda Zanzibar; na TZS bilioni 5.0 zitatumika katika kuratibu zoezi hili.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) Gerlad Kusaya akiwa na ujumbe wake wakishiriki katika mkutano wa 64 wa majadiliano ya majadiliano ya Kamisheni ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani ulioanza Oktoba 18 - 21 Mwaka huu Jijini Vienna Nchini Austria.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) Gerlad Kusaya (Wa kwanza Kushoto), Mwenyekiti wa Mkutano wa UNCND Balozi Dominika Chrois (wa katikati) na Katibu Mtendaji wa UNCND Bibi Jo Bedeyne- Amann (wa kwanza Kulia) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano huo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. LIPANDE SAID @ SIMWICHE [62] na 2. JUMA PIUS [32] wote wakazi wa Kapyo wilayani Mbarali mkoani Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali vipande saba [07] vya Meno ya Tembo.

Watuhumiwa walikamatwa tarehe Oktoba 20, 2021 majira ya saa 10:00 asubuhi huko Kijiji cha Kapyo kilichopo Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kupata taarifa za siri na kisha kufanya msako na upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa LIPANDE SAID @ SIMWICHE na kufanikiwa kukuta nyara hizo zikiwa zimefichwa kwenye mfuko wa sandarusi.

Aidha katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa wakiwa na nyara nyingine za serikali ambazo ni kipande cha Ngozi ya Fisi Maji nacho kikiwa kimefichwa kwenye mfuko wa sandarusi.

Vipande hivyo saba vya Meno ya Tembo vina uzito wa kilogramu 33 na thamani ya Tshs. Milioni Sitini na tisa laki mbili kumi na nne elfu mia nne na kumi [Tshs.69,214,410/=] huku ikikadiriwa kuwa Tembo waliouawa ni wawili.

Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali kinyume cha sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kifungu namba 86 na kosa la uhujumu uchumi kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2019 kifungu namba 57
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akizungumza na wandishi wa habari leo kuelekea maadhimisho ya wiki ya UWT itakayofanyika Oktoba 23 Wilayani Rufiji Pwani.
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakary Kunenge kuelekea kilele cha wiki ya UWT kitaifa itakayofanyika Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakary Kunenge akizungumza na wandishi wa habari Ofisini kwake leo kuelekea wiki ya UWT kitaifa itakayofanyika Wilayani Rufiji.
Charles James, Michuzi TV

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) itakayofanyika katika eneo la Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani Oktoba 23 Mwaka huu.

Akizungumza na wandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka amesema maadhimisho hayo yamepangwa kufanyika Wilayani Rufiji kwa lengo la kuenzi mchango wa Mwenyekiti wa kwanza wa UWT na mpigania Uhuru wa Tanganyika, Bibi Titi Mohamed.

Kabaka amesema ahadi ya kufanyika kwa maadhimisho hayo wilayani Rufiji waliitoa katika kampeni za Urais mwaka 2020 ambapo akiwa na Rais Samia wakati huo akiwa mgombea mwenza waliahidi kumuenzi Bibi Titi ambaye licha ya kuzaliwa Mkoani Dar es Salaam Lakini ni mwenyeji wa Rufiji kwa kufanya maadhimisho hayo wilayani humo.

" Kilele Cha Wiki ya UWT kimelenga kumuenzi Mwanamke Shujaa na mpigania Uhuru wetu, Bibi Titi Mohamed ambaye Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alimuona anafaa kumsaidia Kwenye mapambano ya Uhuru na kumchukua kazi ambayo aliifanya kwa weledi na nguvu kubwa.

Lakini pia tumechagua mgeni rasmi awe Rais Samia kwa sababu hii ni mara ya kwanza kupata Rais na Mwenyekiti wa CCM Mwanamke tena akiwa shupavu na Shujaa kama Bibi Titi,"

Ametoa wito kwa Wanawake wote wa Mkoa wa Pwani mikoa jirani na Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo yenye kauli ya " Tushiriki kumkomboa Mwanamke kiuchumi, kifikra na kisiasa,".

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakary Kunenge amemshukuru Mwenyekiti wa UWT Taifa,Gaudentia Kabaka kwa kuridhia maadhimisho hayo kufanyika Mkoani Pwani na hasa katika Wilaya hiyo ya Rufiji kwa lengo la kumuenzi Bibi Titi Mohamed.

"Kama Mkoa tunashukuru kwa kupata fursa hii ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya ambayo yatachangia kukuza utalii wetu wa ndani na nje kwani itatoa fursa kwa wadau wa utalii kutembelea Wilaya y Rufiji katika kusoma historia ya Bibi Titi Mohamed na kutembelea mnara wake ambao tayari umeshajengwa.

Bibi Titi Mohamed alizaliwa Mkoani Dar es Salaam mwaka 1926 na alikua Mwenyekiti wa kwanza wa UWT na baadaye nafasi hiyo ilishikwa na Sophia Kawawa, Anna Abdallah, Sofia Simba na sasa Gaudentia Kabaka