Na Farida Mangube, Morogoro
Morogoro: Lori la mizigo lenye namba za usajili T729 BBT pamoja na tela namba T677 BTY limeteketea kwa moto katika eneo la Lugono, karibu na Nyama Choma, kando ya Barabara Kuu ya Iringa–Morogoro.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 19, 2026 katika mazingira ambayo bado hayajafahamika, huku sehemu ya mbele ya lori hilo ikiharibiwa vibaya na moto.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika kwa wakati katika eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto huo kabla haujasambaa zaidi, licha ya uharibifu mkubwa uliokuwa tayari umetokea.
Mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio, akiwemo mwandishi wa MMG, walishuhudia lori hilo likiwa limeteketea huku juhudi za uokoaji zikiendelea.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtu mmoja anasadikika kupoteza maisha kufuatia ajali hiyo. Inadaiwa kuwa mwili wa mtu huyo uliungua vibaya kiasi cha kufanya utambuzi kuwa mgumu, huku mabaki yanayoaminika kuwa ya binadamu yakionekana eneo la tukio, ingawa uthibitisho rasmi bado unasubiriwa kutoka kwa mamlaka husika.

Wakati huo huo, jitihada zinaendelea za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ili kutoa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha tukio hilo, kuthibitisha idadi kamili ya waathirika pamoja na kueleza hatua zinazochukuliwa.
Jeshi la Polisi linatarajiwa kutoa taarifa zaidi mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa awali.
Wananchi wametakiwa kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, huku wakishauriwa kuchukua tahadhari wanapotumia barabara hiyo hasa nyakati za usiku.





Toa Maoni Yako:
0 comments: