
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Katika hatua inayozidi kuipa nguvu ajenda ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya biashara nchini, Stanbic Bank Tanzania imeidhihirisha tena nafasi yake kama mdau muhimu wa masoko ya mitaji baada ya kushiriki kama Mratibu Mkuu wa Hatifungani ya Makazi iliyotolewa na First Housing Finance Tanzania (FHF), mpango unaofungua ukurasa mpya wa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya makazi.
Hatifungani hiyo yenye thamani ya awali ya shilingi bilioni 5, ikiwa na chaguo la nyongeza ya shilingi bilioni 3, imepokelewa kwa mwitikio chanya kutoka kwa wawekezaji, ishara kuwa soko la mitaji nchini linaendelea kukua na kuaminiwa. Wachambuzi wa masuala ya fedha wanaeleza kuwa muundo wa hatifungani hiyo umebuniwa kwa umakini mkubwa, ukilenga kutoa faida za kifedha kwa wawekezaji huku ukiendeleza athari chanya kwa jamii.
First Housing Finance Tanzania, ambayo ni taasisi inayoongoza katika utoaji wa mikopo ya nyumba nje ya mfumo wa kawaida wa kibenki, imeendelea kuimarisha nafasi yake sokoni kwa kufikia asilimia 5.3 ya hisa ya soko la mikopo ya nyumba hadi Machi 31, 2025, na tayari imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 36 kwa mamia ya Watanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, amesema hatifungani hiyo ni ushahidi kuwa masoko ya mitaji yanaweza kutumika kama chombo madhubuti cha kutatua changamoto halisi za kiuchumi.
“Makazi siyo tu paa juu ya kichwa; ni msingi wa familia imara, jamii zenye mshikamano na uchumi unaokua kwa kasi. Kupitia bidhaa za uwekezaji zilizo salama na zinazoaminika, tunaweza kuhamasisha mtaji na kuuelekeza kwenye maeneo yenye tija kubwa,” amesema Rwegasira.
Kwa mtazamo wa biashara, mapato yatakayopatikana kupitia hatifungani hiyo yataongeza uwezo wa FHF kutoa mikopo zaidi ya nyumba, hatua itakayoongeza wigo wa wateja, kukuza mapato ya taasisi hiyo na wakati huo huo kufungua minyororo mipya ya fursa katika sekta ya ujenzi, biashara ya vifaa vya ujenzi na huduma za kitaalamu.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kibenki kwa Makampuni na Uwekezaji wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, amesema uaminifu wa wawekezaji katika masoko ya mitaji hujengwa kupitia uwazi, uwajibikaji na nidhamu ya hali ya juu.
“Vyombo vya kifedha vinapaswa kuwa wazi, vinavyoeleweka na vinavyolingana na malengo ya muda mrefu ya uchumi. Hii ndiyo njia pekee ya kuyawezesha masoko ya mitaji kukua na kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” amesema.
Naye Makamu Mkuu wa Rais wa Kitengo cha Masoko ya Mitaji na Usambazaji wa Madeni, Sarah Mkiramweni, amesema mpango huo unaendana kikamilifu na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambayo inalenga kukuza uchumi jumuishi na ustawi wa jamii.
Kwa kuwalika wawekezaji wa ndani na nje kushiriki katika Hatifungani ya Makazi, Stanbic Bank Tanzania inaendelea kujiweka kama daraja muhimu kati ya mitaji na fursa, ikiimarisha nafasi yake katika kuleta mageuzi ya sekta ya fedha na kuchangia kwa vitendo maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.




















































