Articles by "TEKNOLOJIA"
Showing posts with label TEKNOLOJIA. Show all posts
Wataalamu kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) wamehitimisha mafunzo maalum ya ulinzi na usalama dhidi ya mionzi kwa wafanyakazi wa Maweni Limestone Company. Mafunzo haya, yaliyofunguliwa na Meneja wa Idara ya Ubora wa kampuni hiyo, yalilenga kuwajengea uwezo wafanyakazi wanaoshughulika moja kwa moja na vifaa vya X-Ray Fluorescence (XRF) na nuclear gauges.

Kwa muda wa siku kadhaa, washiriki walipata nafasi ya kujifunza kwa kina kuhusu utambulisho wa mionzi ayonishi, kiasi cha mionzi na vipimo, matumizi ya mionzi, athari zake kiafya, kanuni za ulinzi, mfumo wa kisheria wa Tanzania, majukumu ya Afisa Usalama wa Mionzi (RSO), pamoja na usalama wa nyuklia na udhibiti wa usafirishaji haramu.

Katika hotuba ya kufunga mafunzo, wataalamu wa TAEC walisisitiza umuhimu wa kuimarisha utamaduni wa usalama kazini. “Tunataka kuona kila mfanyakazi akibeba jukumu la kulinda afya yake, wenzake na jamii kwa ujumla. Usalama wa mionzi si jambo la hiari, ni wajibu wa kitaifa,” alieleza Ndugu Mungubariki Nyaki, mkufunzi na msimamizi wa Ofisi ya TAEC Jijini Tanga.

Washiriki walionekana wenye shauku na ari ya kupeleka maarifa mapya kazini. Baadhi walikiri kuwa mafunzo haya yamewapa ujasiri wa kushughulika na vifaa vya mionzi kwa umakini zaidi, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kushirikiana na TAEC ili kuhakikisha viwango vya kitaifa na kimataifa vinazingatiwa.

Mafunzo haya pia yaligusia hatua za dharura endapo ajali za mionzi zitatokea, jambo lililowapa washiriki uelewa wa namna ya kukabiliana na changamoto kwa utulivu na ufanisi.

Kwa ujumla, kufungwa kwa mafunzo haya kumeacha taswira ya matumaini na uwajibikaji. Kampuni ya Maweni Limestone imeonyesha dhamira ya dhati ya kulinda wafanyakazi wake na jamii kwa kuhakikisha teknolojia za kisasa zinatumika kwa usalama na kwa manufaa ya Taifa.

Timu ya Vodacom Tanzania ikiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukamilisha mabadiliko ya huduma ya M-Pesa kwenda mfumo mpya wa kisasa wa  fintech 2.0. Tukio hili limefanyika tarehe 2 Aprili 2026, katika makao makuu ya Vodacom Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam — Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza kukamilika kwa maboresho makubwa ya huduma yake ya kifedha ya M-Pesa kufuatia uwekezaji wa dola za Marekani milioni 28, hatua inayolenga kuongeza ubora, usalama na ufanisi wa huduma hiyo nchini.

Akizungumza wakati wa kutangaza mafanikio hayo Aprili 1, 2026, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Philip Besiimire, alisema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha huduma za kifedha kidijitali na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wateja.

“Tunaijengea M-Pesa misingi imara kwa ajili ya siku zijazo. Lengo letu ni kuhakikisha huduma inabaki kuwa salama, ya kuaminika na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi wa hali ya juu,” alisema Besiimire.

Maboresho hayo yamehusisha uhamishaji wa mfumo kutoka teknolojia ya awali ya G2 kwenda mfumo wa kisasa wa fintech, unaotarajiwa kuongeza uwezo wa kushughulikia miamala mingi kwa wakati mmoja pamoja na kupunguza changamoto za kukatika kwa huduma.

Kwa mujibu wa Vodacom, muundo huo mpya unarahisisha matengenezo ya mfumo kwa muda mfupi zaidi, kutoka saa nyingi hadi dakika chache, hali itakayosaidia kuhakikisha huduma inaendelea bila usumbufu mkubwa kwa watumiaji.

Aidha, kampuni hiyo imeimarisha viwango vya usalama wa taarifa na miamala ya kifedha, hatua inayotarajiwa kuongeza imani ya watumiaji katika huduma za fedha kwa njia ya simu.

Kwa upande wa mawakala na wafanyabiashara, maboresho hayo yanaleta fursa ya kupata taarifa za kina za miamala, kurahisisha usimamizi wa biashara pamoja na kuboresha huduma kwa wateja.

Vodacom pia imeeleza kuwa mfumo huo mpya utawezesha kuanzishwa kwa huduma mpya kwa haraka zaidi, hususan katika maeneo ya akiba, mikopo na malipo ya kibiashara, huku ukiendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Katika kuhakikisha ufanisi wa huduma mpya, kampuni hiyo imeanzisha kipindi maalum cha siku 30 kinachojulikana kama HyperCare, ambapo timu za kiufundi zitakuwa zikifuatilia kwa karibu utendaji wa mfumo na kushughulikia changamoto zozote zitakazojitokeza.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Vodacom Tanzania ya kuendelea kuwekeza katika mageuzi ya kidijitali, huku ikiimarisha nafasi yake kama mdau muhimu katika kukuza ujumuishwaji wa kifedha na maendeleo ya uchumi jumuishi nchini Tanzania.

Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya teknolojia ya Google imetangaza upanuzi mkubwa wa huduma zake za utafutaji kwa kutumia Akili Bandia (AI) kwa kuongeza lugha 13 za Afrika, ikiwemo Kiswahili na Kisomali, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa mamilioni ya watumiaji barani humo.

Kupitia taarifa iliyotolewa Machi 6, 2026, kampuni hiyo ilisema maboresho hayo yatawezesha watumiaji kuvinjari mtandao, kujifunza na kuunda maudhui kwa kutumia lugha zao za asili. Huduma hiyo mpya pia inaongeza uwezo wa kipengele cha muhtasari wa majibu ya AI (AI Overviews) ambacho kinatoa majibu mafupi yanayotengenezwa na AI pamoja na viungo vya taarifa zaidi kwa mtumiaji.

Aidha, mfumo wa AI Mode unawaruhusu watumiaji kuwasiliana na mfumo huo kwa kutumia maandishi, sauti au picha ili kupata majibu ya kina zaidi kulingana na lugha wanayopendelea. Maboresho hayo yameanza kutolewa kwa watumiaji katika nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Kenya, Nigeria, Ethiopia na Tanzania ambako matumizi ya utafutaji mtandaoni yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.

Mbali na Kiswahili na Kisomali, lugha nyingine zilizoingizwa katika mfumo huo ni pamoja na Afrikaans, Akan, Amharic, Hausa, Kinyarwanda, Afaan Oromoo, Sesotho, Setswana, Wolof, Yorùbá na isiZulu.

Google imesema hatua hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi, walimu na wajasiriamali kutumia teknolojia ya AI katika kutatua changamoto halisi katika jamii zao badala ya kusikia tu kuhusu teknolojia hiyo. Maboresho hayo pia yanajengwa juu ya utafiti wa mradi wa lugha za Kiafrika wa Google Waxal language project unaotumia ujifunzaji wa mashine na ushirikiano wa wataalamu wa lugha ili kuboresha uelewa wa AI katika lugha za Afrika.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, watumiaji wanaweza kutumia huduma hiyo kwa kufungua programu ya Google app kwenye simu za Android au iOS au kupitia kivinjari cha simu, kisha kuchagua kipengele cha AI Mode na kuuliza maswali kwa lugha wanayopendelea. Google imewahimiza watumiaji barani Afrika kujaribu huduma hiyo na kutoa maoni ili kuboresha zaidi matumizi ya AI katika lugha za Kiafrika.

Na Mwandishi Wetu.

 Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewasisitiza waajiri kwenye vyombo vya habari nchini kuzingatia kikamilifu masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, hususan wanapoajiri au kuwasainisha mikataba watumishi wa kada ya habari, ili kuepuka migogoro ya kisheria inayoweza kujitokeza baadaye.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, tarehe 20-21 Januari, 2026 wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi katika mikoa ya Dodoma na Iringa, ilipotembelea vyombo kadhaa vya habari kwa lengo la kukagua kiwango cha uzingatiaji wa Sheria hiyo kwa watumishi wanaojihusisha na shughuli za kihabari, wakiwemo wahariri, waandishi wa habari, watangazaji, wapiga picha waandaaji na waandishi wa kujitegemea
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Wakili Kipangula amesema Bodi imebaini uwepo wa waandishi wenye sifa stahiki kwa mujibu wa Sheria kwenye vyombo hivyo, lakini bado hawajajisajili katika Mfumo wa TAI-HABARI ili kuomba ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari, hali inayoweza kuwaweka waajiri na waajiriwa katika hatari ya kukiuka Sheria.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa waajiri kuhakikisha kuwa watumishi wote wa kada ya habari wanakuwa wamekamilisha taratibu za usajili na kupata ithibati kabla ya kupewa majukumu au kuajiriwa ili kulinda uhalali wa ajira na kuepuka athari za kisheria.
Aidha, Wakili Kipangula amesema changamoto nyingine iliyobainika katika baadhi ya vyombo vya habari ni malipo madogo ya posho au mishahara kwa waandishi, hali inayohitaji mjadala mpana na mikakati maalum ya pamoja kati ya waajiri, wadau wa habari na Serikali ili kuhakikisha mazingira bora na ya haki ya kazi kwa waandishi wa habari.

Hata hivyo, amepongeza baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari waliobainika kuzingatia kwa umakini masharti ya Sheria, kushughulikia changamoto za waandishi wao kwa uwazi, na kufanya uwekezaji mkubwa unaolenga kujenga mazingira wezeshi, salama na rafiki ya utendaji wa kazi za kihabari.

Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, juhudi hizo ni mfano wa kuigwa na zinachangia moja kwa moja katika kulinda hadhi ya taaluma ya habari, kuongeza weledi wa waandishi na kuimarisha uaminifu wa vyombo vya habari kwa jamii.

Na Mwandishi Wetu.

KAMPUNI ya Mati Super Brands Ltd kupitia tawi lake la Mati Technology imezindua teknolojia mpya ya ndege nyuki (drone) zinazotengenezwa nchini, zenye uwezo wa kuboresha sekta ya kilimo na huduma nyingine za kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Group of Companies, David Mulokozi, amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika uzalishaji wa drone zinazotumika kunyunyizia dawa mashambani, kupima maeneo, kupanda mbegu, kusafirisha mizigo na kusaidia kaguzi mbalimbali.

Mulokozi ameeleza kuwa drone hizo zitauzwa kuanzia Shilingi milioni 17, bei ambayo ni nafuu ukilinganisha na gharama kubwa za kuagiza kutoka nje ya nchi. Pia, kampuni ipo katika mazungumzo na benki ili kuwezesha wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kumudu teknolojia hiyo.


“Tumeona changamoto kubwa inayowakabili wakulima hasa kwenye upuliziaji wa dawa. Kwa kutumia drone hizi, hekari moja inaweza kunyunyiziwa dawa ndani ya dakika saba pekee, jambo linaloongeza ufanisi na kulinda afya za wakulima,” alisema Mulokozi.

Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa drone hizo utatoa ajira kwa wahandisi wa Kitanzania na kufanikisha uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa wataalamu wa kigeni
Kwa upande wake, Afisa Ushirika kutoka ofisi ya Msajili mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, amesema teknolojia hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa mazao kama mbaazi ambayo hukua kwa urefu na kufanya unyunyiziaji wa dawa kuwa mgumu na wa gharama kubwa.

“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kuimarisha vyama vya ushirika. Tutaanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia hii,” alisema Merinyo.
Naye Afisa Kilimo wa mkoa wa Manyara, Paulo Eugine, amesema drone hizo zitasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya madhara ya kiafya yaliyokuwa yanawapata kutokana na kutumia pampu za mgongoni.

“Sasa mkulima ataweza kutumia remote control bila kuingiliwa na sumu, jambo linaloimarisha usalama na afya zao,” alisisitiza Eugine.

Hatua hii ya Mati Technology inatarajiwa kuchochea mapinduzi ya kilimo nchini na kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza tija kwa kutumia teknolojia za kisasa.

 
Vodacom Tanzania imeadhimisha miaka 25 ya kuwahudumia Watanzania tangu kuanzishwa kwake katika hafla iliyofanyika Agosti 15, 2025, ikianzia makao makuu yake jijini Dar es Salaam. Sherehe hizo zilipambwa na ukataji wa keki iliyoashiria robo karne ya ukuaji, ubunifu na uongozi wa sekta ya mawasiliano nchini.

Baada ya hafla hiyo, familia ya Vodacom ilijumuika na wateja wake katika Soko la Stereo lililoko Temeke, ikiwa ni ishara ya kuthibitisha msemo wao wa “Tupo Nawe, Tena na Tena.” Kupitia tukio hilo, Vodacom iliendelea kuonesha dhamira yake ya kusogea karibu zaidi na wananchi, kusherehekea nao mafanikio yaliyopatikana kwa pamoja.

Vodacom pia ilitumia fursa hiyo kuwashukuru wateja kwa mapokezi makubwa ya huduma ya M-Pesa, tangu ilipoanzishwa mwaka 2008. Huduma hiyo imekuwa chachu ya mageuzi makubwa katika ujumuishi wa kifedha nchini kwa kutoa suluhisho kama mikopo midogo, uwekezaji kupitia M-Wekeza, pamoja na huduma za vikoba vya kidigitali kupitia M-Koba.
Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango akizungumza kwenye kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Salome Kessy (katikati) akifurahia jambo na Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango (kushoto kwake) wakati wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA, Bw. Mohamed Mashaka.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wakimsikiliza Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Salome Kessy (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bi. Mary Mwakapenda (wa kwanza kulia) akiwa katika kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wakimsikiliza Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango (hayupo pichani) alipokuwa akifafanua jambo kuhusu TEHAMA wakati wa kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Paul Seadin (aliyesimama) akichangia hoja wakati wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wakimsikiliza Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Bw. Priscus Kiwango (hayupo pichani) alipokuwa akifafanua jambo kuhusu TEHAMA wakati wa kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali wakimsikiliza Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Salome Kessy (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Sera za Tehama na Viwango, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Ibrahim Toure (wa kwanza kulia) akiwa katika kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Salome Kessy (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.


Na Veronica Mwafisi-Dar es Salaam.

Mradi wa Tanzania ya Kidijitali umeleta mapinduzi makubwa ya miundombinu ya TEHAMA nchini ikiwemo kuunganisha jumla ya taasisi za umma 600 ambazo ni Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi zote zilizohamia Dodoma ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na watumishi wa umma.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango wakati wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.

“Mradi huu umeleta mafanikio makubwa katika kuunganisha Serikali kwenye mitandao ya TEHAMA ambapo taasisi 600 ikiwemo Wizara, Mikoa, Halmashauri na Taasisi zote zilizohamia Dodoma zimeunganishwa na mifumo ya TEHAMA ili kutoa huduma kwa wananchi na watumishi wa umma nchini, amesema Bw. Kiwango
Ameongeza kuwa katika kutoa huduma bora, watumishi wa umma wameendelea kutekeleza majukumu yao kupitia mifumo mbalimbali na kupimwa kupitia mifumo iliyojengwa ya Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma na Taasisi (e-Utendaji).

Aidha, Mfumo wa Daftari la Huduma za Serikali utawasaidia wananchi kupata huduma sehemu moja kwa urahisi, kwa wakati na kwa uwazi.

Mkurugenzi Kiwango ametoa wito kwa wananchi kutumia simu zao za viganjani kupiga namba *152*00# kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za Serikali bila kufika katika ofisi husika endapo hawatakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

 

Na Mwandishi Wetu.

Mawaziri wa Mawasiliano kutoka Tanzania na Kenya wamezindua rasmi maunganisho ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) wa Tanzania unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), na mikongo ya baharini ya Mombasa kupitia Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (ICTA).

Uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidigitali wa Kenya, Injinia William Kabogo Gitau, pamoja na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Jerry Silaa.

Mawaziri hao wamesisitiza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria, ikilenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika, pamoja na kupunguza changamoto za kukatika kwa mtandao.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Gitau amesema: “Jambo la msingi ni ushirikiano wa dhati kati ya nchi zetu mbili. Ni muhimu kuhakikisha tunatunza miundombinu hii ya kimkakati ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababisha kukatika kwa umeme na mtandao. Pia tuendelee kuimarisha mahusiano yetu kwa manufaa ya pande zote.”

Kwa upande wake, Mhe. Jerry Silaa alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya pamoja ya mawasiliano kati ya nchi washirika ni wajibu wa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya kikanda.

“Kuna faida kubwa ya kuwa na maunganisho mengi ya mikongo ya mawasiliano. Hii husaidia kuwepo kwa mtandao wa uhakika, unaotegemewa hata wakati wa changamoto za kiufundi katika njia moja ya mawasiliano,” alisema Silaa.

Mkongo huo tayari umeanza kufanya kazi nchini Kenya, hatua inayowezesha huduma za intaneti na mawasiliano kusambaa kwa kasi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Uzinduzi huu unaashiria mafanikio makubwa katika juhudi za kuunganisha ukanda huu kidigitali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Na Mwandish wetu, Dar es Salaam.

CHAMA cha Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) kimeshukuru uamuzi wa serikali ya kuwapatia mafunzo maalumu ya kunoa weledi na uzalendo wa wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Mabloga zaidi ya 200 wakiwemo wa diaspora walioanzisha Mtandao huo mwaka 2015 watapata mafunzo hayo.
 
“Tumekuwa na mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao kimsingi ndio wasimamizi wakuu wa maudhui na wametuthibitishia kwamba wapo hatua za mwisho za kutekeleza maagizo ya serikali ya kutoa mafunzo kwa mabloga wote nchini,” alisema Mwenyekiti wa TBN , Beda Msimbe.

Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Msimbe alisema kwamba lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea mabloga weledi, uzalendo, na umakini katika kutambua na kupambana na habari feki, huku wakiwezesha usambazaji wa taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu ujao.

“ Tunahitaji kukumbushana kuhusu nchi hii, katiba yetu, amani na umuhimu wa uchaguzi katika demokrasia ya aina yetu.Uamuzi huu wa serikali wa kutupiga msasa ni muhimu sana” alifafanua.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mwenyekiti huyo wa TBN, Beda Msimbe, alieleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali kufanikisha mafunzo. Alisema wameomba mafunzo hayo kipindi cha sasa kwa kuwa wapo wanablogu ambao ni mara ya kwanza kuelekea katika uchaguzi mkuu, na kurejea ombi lao tena wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo.

Alisema kwamba uongozi wa TBN kwa sasa unafanya kazi kwa karibu na serikali kuhakikisha kuwa zaidi ya wanachama 150 wa chama hicho waliotawanyika nchini kote wanafaidika kikamilifu na mafunzo haya muhimu.

Msimbe aliwataka mabloga wote nchini kuhakikisha wanawasiliana na Mratibu wa TBN, Bw. Gadiola Emanuel ili kuthibitisha anwani zao na kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kwa ajili ya ushiriki. Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wale wote ambao bado hawajajiunga na TBN kufanya hivyo sasa ili waweze kunufaika na fursa hii muhimu ya mafunzo.

Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kinajumuisha mabloga wanaotengeneza aina mbalimbali za maudhui, ikiwemo michezo, habari za siasa, afya, uchumi, na habari mchanganyiko. Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha uwezo wao wa kutoa taarifa zenye ukweli na uhakika, hivyo kuchangia katika mazingira ya uchaguzi yenye uwazi na uwajibikaji.