Articles by "HABARI PICHA"
Showing posts with label HABARI PICHA. Show all posts

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Dar es Salaam imeandika historia mpya katika harakati za kuboresha huduma za afya baada ya Mkoa wa Manyara kufanikisha zoezi kubwa la kuchangisha fedha lililowezesha kupatikana kwa zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa njiti na kuimarisha huduma za afya katika mkoa huo.

Fedha hizo zilikusanywa kupitia hafla maalumu ya chakula cha jioni cha hisani (Manyara Tanzanite Marathon Dinner Gala) iliyofanyika Julai 24, 2026 katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Hatua Moja Okoa Maisha ya Mtoto, ambayo inalenga kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa, kuboresha huduma za watoto wachanga na kupunguza vifo vinavyotokana na kuzaliwa njiti.

Jumla ya Shilingi 1,356,900,000 zilipatikana kupitia ahadi za michango na fedha taslimu kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi za fedha, makampuni binafsi, viongozi wa Serikali, wabunge, wafanyabiashara na wananchi waliojitokeza kuunga mkono kampeni hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kikanda pamoja na wadau wa sekta ya afya, ambapo mshikamano mkubwa ulionekana katika jitihada za kuhakikisha watoto wanaozaliwa njiti wanapata huduma bora na salama.

Akizungumza baada ya harambee hiyo, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Babati Vijijini, Mhe. Daniel Baran Sillo, aliyekuwa mgeni rasmi, alisema mafanikio hayo yanaonesha moyo wa uzalendo na mshikamano wa Watanzania katika kusaidia sekta ya afya.

Alisema lengo la kampeni hiyo ni kufikisha zaidi ya Shilingi bilioni 1.5, huku akiwakaribisha Watanzania kushiriki Manyara Tanzanite Marathon itakayofanyika Agosti 22, 2026 mkoani Manyara.

“Tunawashukuru wadau wote waliojitokeza na kuchangia. Kila mchango una maana kubwa katika kuokoa maisha ya watoto wetu. Tunataka kuhakikisha hospitali zetu zinakuwa na vifaa vinavyohitajika kuwahudumia watoto njiti kwa kiwango cha kisasa,” alisema Mhe. Sillo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, alisema kampeni hiyo imeibuka kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha nguvu za Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto.

Aliwataka wananchi, taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuchangia ili kufanikisha lengo lililowekwa, akisisitiza kuwa uwekezaji katika afya ya watoto ni uwekezaji katika mustakabali wa taifa.


“Kila mtoto ana haki ya kuishi. Tunapowekeza katika vifaa tiba na huduma za watoto njiti, tunaokoa familia, tunaimarisha jamii na tunajenga taifa lenye nguvu,” alisema Mhe. Sendiga.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Method, alieleza kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya watoto wanaozaliwa njiti, ambapo kati ya watoto 3,000 hadi 3,200 huzaliwa njiti kila mwaka.

Alisema idadi hiyo inaweka shinikizo kubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya, hasa katika upatikanaji wa mashine za kusaidia watoto kupumua, incubators, vifaa vya ufuatiliaji wa afya za watoto wachanga na miundombinu ya huduma maalumu.
“Watoto njiti wanahitaji uangalizi wa karibu na vifaa maalumu. Bila uwekezaji wa kutosha, tunakuwa katika hatari ya kupoteza maisha ambayo yangeweza kuokolewa,” alisema Dkt. Method.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kuzaliwa njiti ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia vifo vya watoto wachanga duniani, na huduma bora katika saa na siku za mwanzo baada ya kuzaliwa ndiyo huamua kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mtoto kuendelea kuishi.

Wadau waliohudhuria hafla hiyo walieleza kuwa kampeni hiyo imeonesha mfano wa namna matukio ya michezo yanaweza kutumika kama nyenzo ya kuchangisha fedha kwa ajili ya miradi ya kijamii na maendeleo.
Mbio za Manyara Tanzanite Marathon zimekuwa zikikua kwa kasi na sasa zinatajwa kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo na hisani nchini Tanzania, yakilenga kuhamasisha afya, utalii na maendeleo ya jamii kwa wakati mmoja.

Waandaaji wa marathon hiyo walisema fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika ununuzi wa vifaa tiba, uboreshaji wa huduma za watoto wachanga na kuimarisha uwezo wa hospitali za Mkoa wa Manyara kuhudumia watoto njiti kwa ufanisi zaidi.

Kampeni hiyo pia inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo zimekuwa zikilenga kuboresha huduma za afya, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuimarisha ustawi wa jamii na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika maeneo yote ya nchi.
Waandaaji wameendelea kutoa wito kwa Watanzania kushiriki mbio hizo au kuchangia kupitia akaunti maalumu za kampeni, wakisisitiza kuwa kila mchango ni hatua muhimu katika kuokoa maisha ya mtoto mmoja au zaidi.

Michango inaendelea kupokelewa kupitia CRDB Lipa Namba 113069180 na CRDB Account No. 10401215064 (Manyara Tanzania Marathon).

Kwa mafanikio yaliyopatikana katika usiku huo wa kihistoria, Mkoa wa Manyara umeonesha kuwa mshikamano wa jamii unaweza kuwa nguvu kubwa ya kuokoa maisha, huku kampeni ya Hatua Moja Okoa Maisha ya Mtoto ikiendelea kuwa mwanga wa matumaini kwa maelfu ya watoto wanaozaliwa njiti kila mwaka nchini Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati), akimwakilisha Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, akikata utepe kuzindua rasmi Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dkt. Hussein Ali Mwinyi kilichopo Mwanakwerekwe, Zanzibar. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Anna Athanas Maalim, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais  Ikulu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya Salum, na Afisa Mkuu wa Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, Derick Lugemala. Kituo hicho kimefadhiliwa  na Benki ya Stanbic kinacholenga kupanua upatikanaji wa huduma bora za malezi, makuzi na elimu ya awali kwa watoto nchini Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amefungua rasmi Kituo cha Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto (ECD) cha Mwanakwerekwe kilichofadhiliwa na Stanbic Bank Tanzania, sambamba na uzinduzi wa Mpango wa Zanzibar wa Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto wa Kisekta (2026–2031).

Ufadhili wa kituo hicho umetokana na awamu ya kwanza ya TZS milioni 350 iliyotolewa na Stanbic Bank Tanzania, ikiwa ni sehemu ya ahadi ya benki hiyo ya TZS milioni 500 kwa mpango wa Serikali wa Adopt an ECD unaoendeshwa na Shirika la Save the Children.

Kituo hicho kitatoa huduma bora za malezi na elimu ya awali kwa watoto wa wafanyabiashara na familia zinazofanya kazi katika Soko la Mwanakwerekwe na maeneo jirani.

“Uwekezaji huu unaakisi dhamira ya Stanbic Bank Tanzania ya kuendeleza malezi na makuzi ya awali ya mtoto kama msingi wa kujenga rasilimali watu, kukuza uchumi shirikishi na kuimarisha ustawi wa muda mrefu wa Zanzibar. Aidha, unaonesha mafanikio yanayowezekana pale Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo wanapounganisha nguvu kuelekea dira moja,” amesema Derick Lugemala, Afisa Mkuu wa Fedha, Stanbic Bank.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Mhe. Hemed aliipongeza Stanbic Bank kwa kuunga mkono ajenda ya serikali ya kuwekeza katika maendeleo ya mtoto katika umri wa awali na kuzitaka benki nyingine pamoja na taasisi za kifedha kuiga mfano huo wa kuchangia maendeleo ya taifa.
 
"Tunaipongeza Benki ya Stanbic kwa uwekezaji huu wa kimkakati na mchango wake endelevu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, si Zanzibar pekee bali Tanzania nzima kwa ujumla. Nazihimiza benki nyingine na taasisi za kifedha kuiga mfano huu mzuri wa kushiriki katika ujenzi wa taifa," alisema kabla ya kukifungua rasmi kituo hicho kilichopewa jina la Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya utapeli wa mitandaoni vinavyotumia majina, picha na nembo za viongozi wa Serikali, taasisi na watu maarufu kwa lengo la kuwalaghai wananchi na kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.

Katibu Mkuu wa TRAMEPRO ambaye pia ni mtaalamu wa tiba asili, Boniventura Mwalongo, alisema matapeli wamekuwa wakisambaza matangazo yanayodai viongozi, wafanyabiashara au taasisi mbalimbali zinatoa mikopo, ruzuku, misaada au fursa za uwekezaji wa haraka, huku wakitumia ushuhuda wa uongo kuwashawishi wananchi.

Mwalongo aliwataka wananchi kutothamini taarifa hizo bila kuzithibitisha kupitia mamlaka au taasisi husika, akisisitiza kuwa ni muhimu kutumia taarifa zinazotolewa kupitia njia rasmi pekee na kuepuka kutuma fedha, nyaraka au taarifa binafsi kwa watu wasiojulikana.

Alisema matumizi mabaya ya nembo za vyombo vya habari na majina ya viongozi wa kitaifa katika kusambaza taarifa za uongo yanachochea upotoshaji wa umma, hupunguza imani kwa taasisi na yanaweza kuhatarisha usalama, amani na mshikamano wa Taifa.

Mbali na hilo, TRAMEPRO imeeleza kuwa bado kuna haja ya kuimarisha mapambano dhidi ya mila potofu zinazodhuru afya, utu na haki za binadamu, ikibainisha kuwa baadhi ya vitendo hivyo vinaendelea kufanyika kwa siri katika maeneo mbalimbali nchini.

Shirika hilo limeitaka Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya utapeli wa mitandaoni kwa kushirikisha vyombo vya dola na mamlaka zinazohusika, huku ikiendelea kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii na huduma za kidijitali.

Aidha, TRAMEPRO imezitaka mamlaka za mawasiliano na usalama kuchukua hatua za haraka dhidi ya akaunti bandia na mitandao inayotumiwa kufanya utapeli, pamoja na kushirikiana na kampuni za mitandao ya kijamii kuziondoa akaunti zinazojifanya viongozi au taasisi.

Mwalongo amewataka wananchi kutokuwa wepesi wa kuamini matangazo yanayoahidi fedha, mikopo au ruzuku bila uthibitisho, akisisitiza umuhimu wa kuhakiki taarifa kupitia ofisi au tovuti rasmi.

Alisema jamii salama na yenye maendeleo endelevu hujengwa kwa msingi wa ukweli, elimu, uwajibikaji na ushirikiano, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya utapeli wa mitandaoni, taarifa za uongo na mila potofu.

Na Mwandishi Wetu.

Nairobi, Kenya

Rais wa Kenya, William Ruto, amesema Serikali yake inaendelea kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya taifa kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali zinazolenga kuongeza ajira, kukuza vipaji na kuimarisha uchumi.

Ruto amesema Serikali imewekeza katika michezo, uchumi wa ubunifu na kidijitali, ajira za nje ya nchi, uwezeshaji wa biashara, makazi nafuu pamoja na maendeleo ya miundombinu, hatua ambazo zimeanza kuzaa matunda kwa kuunda mamilioni ya nafasi za ajira na fursa nyingine kwa vijana.
Amesema katika sekta ya michezo pekee, Serikali inaendelea kujenga na kuboresha viwanja 34 vya michezo nchini ili kusaidia kukuza vipaji vya vijana na kuongeza fursa za maendeleo kupitia michezo.

Kwa mujibu wa Rais huyo, uwekezaji huo umeanza kuleta mafanikio, huku wanamichezo wa Kenya wakiendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Pia aliipongeza timu ya taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17, Junior Harambee Starlets, kwa kuweka historia ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA kwa wanawake chini ya miaka 17.
Ruto aliyasema hayo baada ya kuikaribisha Ikulu ya Nairobi timu ya Migori Youth FC, mabingwa wa National Super League msimu wa 2025/26, ambapo aliikabidhi basi maalumu litakalowasaidia kusafiri kwa urahisi katika mechi za ligi nchini kote.

Aidha, alisema Serikali inaendelea kujenga uwanja wa kisasa katika Kaunti ya Migori utakaotumiwa na Migori Youth FC pamoja na jamii kwa ujumla, kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kukuza vipaji vya michezo na maendeleo ya vijana nchini Kenya.

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa waandishi wa habari, wadau wa sekta ya habari na wananchi kupitia banda lake lililopo katika Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Huduma zinazotolewa ni pamoja na ugawaji wa vitambulisho vya ithibati kwa waandishi wa habari waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, usajili wa waandishi wa habari, marekebisho ya taarifa za usajili pamoja na utoaji wa elimu kuhusu majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi hiyo.

JAB imesema ushiriki wake katika maonesho hayo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na wadau wa sekta ya habari, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma pamoja na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa ithibati na usajili wa waandishi wa habari nchini.

Bodi hiyo imewahimiza waandishi wa habari na wadau wengine kutumia fursa ya maonesho hayo kupata huduma kwa haraka na kwa ukaribu, huku ikieleza kuwa huduma hizo zinaendelea kutolewa pia katika Makao Makuu ya JAB.

Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanaendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazowasilisha huduma na bidhaa zao kwa wananchi.