Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, amezitaka wizara zinazohusika na sekta ya mazingira kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweka mpango wa pamoja utakaosaidia kuhakikisha uhifadhi endelevu wa mazingira nchini.
Makamu wa Rais alitoa wito huo wakati wa kikao cha mazungumzo kilichowakutanisha viongozi wa wizara mbalimbali zinazohusika na masuala ya mazingira kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kilihusisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni pamoja na Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew.
Wengine walioshiriki ni pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Festo Dugange na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Richard Muyungi pamoja na wataalamu kutoka wizara hizo.
Akizungumza katika kikao hicho, Nchimbi alisema wizara hizo zina uhusiano mkubwa katika kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unatekelezwa ipasavyo. Alifafanua kuwa mafanikio ya sekta ya maji yanategemea uwepo wa vyanzo vya maji vilivyohifadhiwa, huku matumizi ya nishati safi ya kupikia yakisaidia kupunguza ukataji miti ovyo na hivyo kulinda misitu.
Aidha, Makamu wa Rais aliwahimiza viongozi hao kuongeza jitihada za kulifanya taifa la Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika uhifadhi wa mazingira barani Afrika na duniani kwa ujumla, akibainisha kuwa nchi ina rasilimali za misitu na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia uhifadhi huo.

Aliongeza kuwa juhudi hizo zinaungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye tayari amezindua mpango wa kukijanisha nchi na kuendelea kuhamasisha upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Nchimbi pia aliwataka viongozi wa wizara hizo kuandaa mkakati madhubuti wa kukabiliana na changamoto za kuhifadhi miti baada ya kupandwa ili kuhakikisha malengo ya kampeni za upandaji miti yanafikiwa.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuanzisha mpango wa upandaji miti kitaifa unaoendana na maadhimisho ya International Day of Forests, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika juhudi za kuhifadhi mazingira nchini.






Toa Maoni Yako:
0 comments: