Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani dereva wa daladala pamoja na mmiliki wa gari hilo kufuatia ajali ya barabarani iliyosababisha kifo cha askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana, Coplo Tumsifu Kileo, aliyekuwa akitekeleza majukumu yake kazini.

Washtakiwa hao ni Mohamed Rashid Mumba (40), mmiliki wa gari la abiria namba T.234 BUM aina ya Toyota Hiace, na dereva Alphonce Fredrick Kashozi (25). Wamefikishwa mahakamani Februari 20, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana na kusomewa mashtaka manane yanayohusiana na kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha ajali na kuua bila kukusudia.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, ajali hiyo ilitokea Februari 10, 2026 majira ya saa 2:00 asubuhi katika eneo la mzunguko wa Mwanza Hotel, ambapo Coplo Kileo alikuwa akisimamia usalama wa barabarani. Inadaiwa dereva wa daladala hilo alishindwa kulidhibiti gari, likampiga askari huyo pamoja na mtembea kwa miguu, Lucia Rweikiza, aliyepata majeraha.
Baada ya ajali, askari huyo alipelekwa hospitali kupatiwa matibabu kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Bugando Medical Centre, ambako alifariki dunia Februari 13, 2026 alipokuwa akiendelea na matibabu.

Kifo cha askari huyo kimeibua majonzi makubwa miongoni mwa jeshi la polisi, familia na wananchi wa Mwanza, wengi wakisisitiza umuhimu wa madereva kuheshimu sheria za usalama barabarani na maelekezo ya askari.

Upande wa mashtaka umeeleza kuwa uchunguzi bado unaendelea huku ukiomba mahakama kuendelea kuwashikilia washtakiwa hao kwa mujibu wa sheria. Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe itakayopangwa baadaye kwa hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa wito kwa madereva wote kuendesha vyombo vya moto kwa umakini, likionya kuwa uzembe barabarani unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: