Articles by "MIKOANI"
Showing posts with label MIKOANI. Show all posts
Na Munir Shemweta, WANMM

Dodoma.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeingilia kati mgogoro wa matumizi ya ardhi unaomhusisha mwekezaji Rashid Kwanzibwa katika eneo la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita, kufuatia madai ya kubomoa baadhi ya majengo yaliyopo kwenye maeneo ya serikali na kuanzisha miradi bila kufuata taratibu.

Akizungumza leo Januari 26, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imeanza kushughulikia suala hilo kwa kina ili kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa mujibu wa sheria na taratibu za matumizi bora ya ardhi.

Dkt. Akwilapo amewakumbusha wamiliki wote wa ardhi nchini kuzingatia matumizi yaliyobainishwa katika hati miliki zao, akisisitiza kuwa mmiliki yeyote anayepanga kubadili matumizi ya eneo lake anatakiwa kuomba na kupata kibali cha mabadiliko ya matumizi kama sheria inavyoelekeza.

“Hatua hii itasaidia kuhakikisha maeneo yanaendelezwa kwa mpango, kupunguza migongano ya matumizi ya ardhi, kulinda mazingira na kuhakikisha miji yetu inakuwa nadhifu,” amesema Waziri.

Ameongeza kuwa uendelezaji wowote wa ardhi unapaswa kuzingatia sheria za mipango miji na vijiji, ikiwa ni pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka husika kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi wowote.

Kwa mujibu wa Waziri, timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi na TAMISEMI tayari ipo kazini kuchunguza kwa kina sakata hilo, na baada ya uchunguzi kukamilika, Serikali itatoa taarifa rasmi ya pamoja kueleza hatua zilizofikiwa.

Hatua ya Wizara kuingilia kati imekuja baada ya kusambaa kwa picha na taarifa katika mitandao ya kijamii zikionesha Kamati ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikisitisha shughuli za ujenzi wa vibanda vya maduka katika eneo la viwanja vya CCM Katoro, kufuatia madai kuwa mwekezaji aliingia katika maeneo ya serikali ya kijiji yaliyopo Kitongoji cha Katoro Center.

Serikali imesisitiza itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya ardhi nchini ili kulinda maslahi ya umma, kudumisha amani na kuhimiza maendeleo endelevu katika maeneo yote.

Na Mwandishi Wetu, Manyara.

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi kamati za ushauri wa kisheria pamoja na kliniki za sheria bila malipo zitakazotoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na Wilaya zake, hatua inayolenga kusogeza huduma za haki karibu zaidi na jamii.

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Mount Hanang Katesh, Wilaya ya Hanang, na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wanasheria, wadau wa haki na wananchi mbalimbali.
 Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sendiga amewahimiza wananchi kutumia fursa ya huduma hizo ili kutatua changamoto zao za kisheria kwa wakati na kwa njia sahihi.

Amesema kamati hizo zimeundwa kwa lengo la kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi, watumishi wa umma na viongozi, pamoja na kutambua changamoto za kisheria zilizopo katika jamii na kusaidia kuzitatua kabla hazijawa migogoro mikubwa.
“Kamati hizi za ushauri wa kisheria ambazo zinaanza kazi leo, zinalenga kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wetu, lakini pia kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika maeneo yetu,” amesema Mhe. Sendiga.

Aidha, amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia wanasheria wasio na sifa au watu wasiobobea katika masuala ya sheria, kwani hali hiyo imekuwa ikisababisha hasara ya muda, fedha na wakati mwingine kupoteza haki. Badala yake, amewashauri wawatumie wanasheria waliopo katika kambi za Mount Hanang na kupitia kliniki za sheria zilizoanzishwa.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa amezitaka kamati hizo kuendelea kuboresha utoaji wa elimu ya kisheria kwa jamii, hasa vijijini ambako bado huduma za kisheria hazijawafikia wananchi wengi. Amesisitiza pia umuhimu wa kuanzisha kliniki za sheria zinazotembea (mobile legal clinics) ili kuwafikia wananchi walioko maeneo ya mbali.

“Maelekezo ya serikali na ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma zinamfikia mwananchi moja kwa moja. Hii ndiyo sababu tunaweka nguvu katika kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi,” aliongeza.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na masuala mengine ya kisheria ambayo yamekuwa yakisumbua jamii kwa muda mrefu.

Mpango wa uanzishwaji wa kamati za ushauri wa kisheria na kliniki za sheria Manyara unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utawala wa sheria, kuongeza uelewa wa haki za msingi na kujenga jamii yenye haki na usawa zaidi.

Na Mwandishi Wetu, Manyara.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi namba ya bure ya huduma kwa mteja 0800787722 itakayotumika kupokea kero, changamoto na malalamiko ya wananchi wa mkoa huo, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa namba hiyo, Mhe. Sendiga amesema mfumo huo utarahisisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao, kwani utamwezesha mwananchi kutoa taarifa kwa urahisi bila gharama yoyote.

“Mwananchi atapiga namba hii bure kabisa bila makato yoyote na kutoa taarifa sahihi bila kudanganya. Lengo ni kupata changamoto kwa wakati na kuzifanyia kazi kwa haraka,” amesema RC Sendiga.
Ameeleza kuwa kupitia namba hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itaweza kufuatilia kwa karibu changamoto za wananchi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi unaostahili kwa wakati, huku taarifa zote zikikusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kutengeneza ripoti za kila mwezi.

Aidha, amezitaka ofisi zote zilizo chini ya uongozi wake kuhakikisha zinashughulikia kwa haraka malalamiko yote yatakayopokelewa kupitia namba hiyo na kutoa mrejesho kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

Wananchi wa Mkoa wa Manyara wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema itawapa fursa ya kufikisha moja kwa moja changamoto zao kwa viongozi, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za kijamii na kiutawala katika maeneo yao.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amemtaka Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, kuhakikisha anasimamia kwa karibu malipo ya wakulima wa kahawa ili kuwalinda dhidi ya ucheleweshaji wa fedha zao unaofanywa na baadhi ya kampuni zinazonunua zao hilo.

Mhe. Kapinga, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, ametoa maelekezo hayo mapema wiki hii alipokuwa akizungumza katika kikao na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Amesisitiza kuwa zao la kahawa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Wilaya ya Mbinga na chanzo kikuu cha maisha ya wananchi wengi, hivyo Serikali haitavumilia kuona watu wachache wanaitia doa kutokana na uzembe au kushindwa kusimamia ipasavyo sheria na kanuni ili wakulima walipwe fedha zao za mauzo ya kahawa kwa wakati.

Katika maelekezo yake, Waziri Kapinga amemwagiza Afisa Ushirika wa wilaya hiyo, kufuatilia kwa karibu na kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati bila visingizio, huku akiwataka watumishi kutotumia masuala ya ukomo wa malipo kama kisingizio cha kuwakandamiza wakulima.
Kwa upande mwingine, Waziri Kapinga amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kufanya tathmini upya ya kampuni ya Mamba Coffee ili kubaini kama inastahili kuendelea kupewa kibali cha kununua kahawa, kutokana na malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, amesema kuchelewesha malipo ni sawa na kuwarudisha nyuma wakulima na maendeleo yao.

Vilevile, amewahimiza viongozi wa vyama vya ushirika kukaa vikao na kufanya maamuzi muhimu mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo, ili kuzuia migogoro inayoweza kuepukika. Pia ametoa onyo kali dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za ushirika, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kutumia fedha hizo kwa maslahi binafsi hatavumiliwa.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kusitishwa kwa muda huduma za Mabasi yaendayo Haraka (UDART) katika barabara kuu mbili za jiji hilo — Morogoro kutokaHuduma za Mabasi ya Mwendokasi Zasitishwa kwa Muda Jijini Dar es Salaam katikati ya mji kuelekea Kimara na Morocco, pamoja na barabara ya Kilwa kutoka katikati ya jiji kuelekea Mbagala — kufuatia kuharibika kwa miundombinu.

Akizungumza leo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chalamila alisema uharibifu huo umetokana na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati wa uchaguzi, ambapo baadhi ya waandamanaji waliharibu mifumo ya ukataji tiketi na maeneo ya kupakia abiria.

“Tumelazimika kusitisha huduma hiyo kutokana na uhalifu uliofanyika wakati wa uchaguzi na kusababisha kuharibika kwa mifumo yote ya ukataji tiketi pamoja na vituo vya abiria,” alisema Chalamila. “Kwa sasa tunatoa maelekezo kwa LATRA kutoa vibali vya muda kwa wamiliki wa daladala ili kuwahudumia wakazi wa maeneo hayo.”

Amesema serikali inaendelea kufanya tathmini ya hasara iliyosababishwa na uharibifu huo, na baada ya ukarabati kukamilika, huduma za mabasi ya mwendokasi zitarejeshwa kama kawaida.

Katika hatua nyingine, RC Chalamila ametangaza kufunguliwa kwa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis, na kuwataka wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao katika eneo hilo kurejea kuendelea na biashara kama awali.

Aidha, amewatoa hofu wakazi wa Dar es Salaam akisema kuwa hali ya usalama katika jiji hilo imeimarishwa, huku akibainisha kuwa ulinzi umeongezwa katika Kituo cha Magufuli ili kulinda abiria, mali na shughuli za kibiashara.

Wakati huohuo, Chalamila ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki kuitisha kikao cha dharura na wamiliki wa vituo vya mafuta kujadili utekelezaji wa marufuku ya uuzwaji mafuta kiholela katika vidumu.

RC Chalamila ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa walinzi wa amani ya nchi, akisisitiza kwamba maendeleo hayawezi kupatikana bila utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amewahakikishia wananchi, wageni na watalii wote kuwa hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Arusha ni shwari, na kwamba shughuli zote za kijamii na kiuchumi zimeendelea kama kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Novemba 4, 2025, mara baada ya kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mhe. Makalla alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha ulinzi unakuwepo muda wote ili kuruhusu shughuli za kila siku kuendelea bila wasiwasi.

“Nataka kuwahakikishia wananchi wa Arusha, wageni na watalii wetu kwamba mkoa uko salama. Shughuli zote za kijamii na kiuchumi zinaendelea kama kawaida, na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo kazini masaa 24 kuhakikisha hali hiyo inabaki kuwa tulivu,” alisema Mhe. Makalla.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa serikali imechukua hatua za haraka kuhakikisha mkoa unarejea katika utulivu kamili, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema za viashiria vya uvunjifu wa amani.

Aidha, Mhe. Makalla aliwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kufungua vituo vyao na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, sambamba na wamiliki wa biashara mbalimbali kufungua maduka na maeneo yao ya kazi ili uchumi wa mkoa usisimame.

“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea. Kwa hiyo naagiza vituo vyote vya mafuta vifunguliwe, na huduma zote za kijamii zirudi katika hali ya kawaida,” alisisitiza Makalla.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote mkoani humo, chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa, kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa ipasavyo, hasa kwenye masoko na maeneo ya makazi ya watu.

“Lazima kuhakikisha taka zote zinaondolewa mara moja kwenye maeneo ya masoko na makazi ya wananchi ili kuepuka magonjwa ya mlipuko. Huduma za usafi ni sehemu ya ulinzi wa afya na usalama wa jamii,” alisema CPA Makalla.

Amewataka pia viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu kwa kuhakikisha hali ya usalama inaimarika katika maeneo yao na kutoa taarifa za matukio yote ya uvunjifu wa sheria kwa mamlaka husika.

Kwa mujibu wa Mhe. Makalla, Serikali ya Mkoa wa Arusha inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama na ustawi wa wananchi, huku akisisitiza kuwa mkoa huo unaendelea kuwa kitovu cha utalii na uchumi wa kanda ya kaskazini.
Dar es Salaam, Oktoba 2, 2025: Baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu huduma duni za usafiri wa Mwendokasi, hususan katika njia ya Kimara, Serikali hatimaye imeongeza idadi ya mabasi mapya ili kurahisisha huduma kwa abiria.

Abiria katika kituo cha Kivukoni na maeneo mengine ya Kimara wameeleza kufurahishwa kwao na uamuzi huo, wakisema umeonesha Serikali imesikia kilio cha wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji na msongamano wa abiria.

Maoni ya Abiria

Alex Michael, ambaye amekuwa mtumiaji wa muda mrefu wa mabasi ya Mwendokasi, alisema kabla ya mabasi mapya kuletwa walilazimika kukaa muda mrefu vituoni bila uhakika wa usafiri, jambo lililowalazimu kutumia usafiri mbadala wa bodaboda kwa gharama kubwa.

“Baada ya kuanza kwa mradi huu karibu miaka 10, mwanzo huduma ilikuwa nzuri na inavutia sana, lakini kadri siku zilivyopita mabasi mengi yakawa yanaharibika na huduma ikawa mbovu. Tunaishukuru Serikali kwa hatua hii ya kuleta mabasi mapya,” alisema Michael.

Kwa upande wake, Amina Ramadhani, mkazi wa Kimara Baruti, alihimiza Serikali kuhakikisha mabasi hayo mapya yanabaki kudumu kwenye njia ya Kimara na sio ya muda mfupi pekee.

“Tunataka mabasi haya yaendelee kutoa huduma hapa Kimara kwa muda mrefu, si kama inavyodaiwa kuwa yameletwa kwa muda tu kabla ya kupelekwa njia ya Mbagala–Gerezani,” alisema Amina.

Historia ya Malalamiko
Wananchi wa Kimara wamekuwa wakilalamikia upungufu wa mabasi ya Mwendokasi, hali iliyosababisha foleni kubwa vituoni na abiria kulazimika kutafuta usafiri mbadala.

Ujio wa mabasi mapya unatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa adha hiyo na kuongeza ufanisi wa huduma katika mradi wa usafiri wa Mwendokasi jijini Dar es Salaam.



Buhigwe. Tarehe 27 Agosti 2025: Akizindua tawi la Benki ya CRDB wilayani Buhigwe pamoja na kupokea madarasa mawili ya shule ya sekondari, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango ameisifu Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kutanua huduma jambo linalosaidia kuongeza ujumuishaji wa kiuchumi kwa wananchi.

Mheshimiwa Makamu wa Rais amesema kitendo cha kuwa na matawi katika halamashauri zote nchini kinaifanya Benki ya CRDB kuwafikia wananchi wengi zaidi kutoka katika kila pembe ya nchi. Kutokana na kuwapo kwa matawi ya benki pamoja na mawakala waliotapakaa maeneo mbalimbali, amesema kunasaidia kuwajumuisha wananchi wengi katika huduma za fedha.

“Changamoto kubwa tuliyonayo ni kurasmisha shughuli za kiuchumi za wananchi wetu. Upatikanaji wa huduma za uhakika za fedha katika maeneo waliyopo wananchi ni kati ya nguzo muhimu zitakazowashawishi wananchi kurasmisha shughuli zao. Nawapongeza Benki ya CRDB kwa kuhakikisha mnakuwepo katika kila halmashauri nchini ili kufikisha huduma zenu kwa wananchi,” amesema Mheshimiwa Dkt. Mpango.
Makamu wa Rais amesema changamoto nyingi zilizopo katika jamii zitaondoka iwapo wananchi wengi zaidi watajumuishwa kifedha na shughuli nyingi za kiuchumi zitarasmishwa hivyo ushiriki wa sekta binafsi hasa benki za biashara na taasisi za fedha ni muhimu sana katika kufanikisha hilo. Licha ya kuwa na matawi nchi nzima, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia ameipongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu wake kwenye huduma na bidhaa inazotoa kwa wateja wake zinazozingatia maadili, utamaduni mpaka imani zao za kidini.

“Mkurugenzi ameeleza hapa kwamba sasa hivi wanayo CRDB Al Barakah Sukuk ambayo ni hatifungani inayozingatia misingi ya sharia. Hii ni hatua kubwa ya kuwajali wawekezaji hasa kipindi hiki benki inaapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwenu. Naamini wana Buhigwe, Kigoma na Tanzania nzima wataitumia fursa hii kuwekeza ili kuimarisha uchumi wao. Tawi hili ninalolizingua leo naamini litaleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Buhigwe ambao hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za benki,” ameeleza Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Kati ya vitu alivyoviomba kwa benki za biashara zikiongozwa na Benki ya CRDB ni kutoa elimu ya fedha. Amesema wananchi wanapaswa kuelimishwa kwa kina kuhusu huduma na bidhaa za kisasa zinazotolewa na benki ili ziwanufaishe wananchi ambao ndio walengwa.
“Benki ya CRDB mmekuwa mnatoa hatifungani ikiwamo hii ya sasa hivi mnayoendelea kuiuza ya CRDB Al Barakah Sukuk lakini ni watu wachache sana wanaelewa maana ya hatifungani na namna wanavyoweza kunufaika nazo. Nawasihi mtoe elimu ya huduma zote mlizonazo pamoja na fursa za uwekezaji mnazozileta kwa wananchi,” amesema Mheshimiwa Dkt. Mpango.


Makamu wa Rais amependekeza kutumiwa kwa wasanii ambao hueleweka kwa urahisi zaidi na wananchi kutoa elimu ya fedha, miongoni mwa mbinu zitakazosaidia kufanikisha mkakati wa kufikisha elimu kwa umma.

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kila wakati benki huwatanguliza mbele wateja wake ndio maana imekuwa ikihakikisha inawafuata mahali popote walipo jambo linaloongeza imani yao.
“Mpaka Juni 2025, Benki yetu ilikuwa imepokea amana za wateja kiasi cha shilingi trilioni 14 na kukopesha jumla ya shilingi trilioni 12.25. Katika kipindi cha miaka 30 cha uwepo wa Benki yetu ya CRDB, tumekua na kutanua mtandao wetu wa huduma kutoka matawi 19 yaliyokuwepo mpaka zaidi ya 260 tukilijumuisha hili tunalolizindua leo.

Matawi haya yanatuwezesha kuhudumia zaidi ya wateja milioni sita nchini kote. Huduma zetu zimefika nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na hivi karibuni tutafika Dubai. Juhudi hizi zote zinadhihirisha jinsi tunavyowajali wateja wetu waliopo ndani na nje ya nchi na ndio maana halisi ya kaulimbiu yetu ya ‘ulipo tupo,’” amesema Nsekela.

Ili kuhakikisha wananchi wengi wanakuwa na uelewa mkubwa zaidi, Nsekela amesema Benki ya CRDB ilianzisha kampuni tanzu ya CRDB Bank Foundation ambayo inatoa mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya fedha na kuwapa mtaji wezeshi wale wanaokidhi vigezo kupitia Programu yake ya Imbeju.

Kupitia programu hii, amesema CRDB Bank Foundation imewafikia zaidi ya wananchi milioni moja na juhudi za kuwafikia wengi wengine zinaendelea ili kuhakikisha hakuna anayeachwa wala kupitwa na fursa hizi za kukuza kipato binafsi na kushiriki kuujenga uchumi wa taifa.
“Benki ya CRDB ndio kubwa zaidi nchini na ya tatu kwa ukubwa ukanda wa Afrika Mashariki, lengo letu ni kuwa namba moja hivyo tutaendeleza ubunifu kwa manufaa ya wateja wetu na Watanzania wote kwa ujumla,” amesema Nsekela.

Licha ya kushiriki kutimiza malengo ya mtu mmojammoja, Nsekela amesema Benki ya CRDB inashiriki pia kutatua changamoto za kitaifa akitolea mfano ujenzi wa kiwanda cha mbolea jijini Dodoma.

“Mbolea ni kati ya changamoto tulizonazo kwenye sekta ya kilimo. Najivunia kusema kwamba Benki ya CRDB imeshiriki kuwezesha ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea kinachomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Burundi. Hili pekee linaonyesha namna tunavyokuza diplomasia ya uchumi. Kwa sasa tunayo CRDB Al Barakah Sukuk, hatifungani inayofuata misingi ya sharia inayompa kila fursa kila Mtanzania kuwekeza kuanzia shilingi 500,000 au dola 1,000 za Marekani kwa faida ya asilimia 12 kwa mwaka,” amesema Nsekela.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji kwa jamii, Nsekela amesema Benki ya CRDB hutenga asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kila mwaka ili kuwekeza kwenye miradi ya wananchi hasa iliyopo kwenye sekta ya elimu, mazingira, afya na uwezeshaji wa wanawake na vijana.

“Leo tunakabidhi madarasa mawili, ofisi ya mkuu wa shule, viti 80 na meza 80. Hata hivyo, tumegundua kuna changamoto ya malazi shuleni hapa hasa kwa wanafunzi waliopo kwenye madarasa ya mitihani. Benki yetu ya CRDB italeta hapa magodoro 150 kwa ajili ya wanafunzi hawa wanaosoma katika Sekondari hii ya Kibande,” amesema Nsekela.
Licha ya msaada huo uliotolewa kwa Shule ya Sekondari kibande, Benki ya CRDB ilishapeleka madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 3.35 kwa Shule Msingi Kasebuzi iliyopo wilayani Kibondo, madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 3.75 kwa Shule Msingi Ruyenzi ya Kakonko, madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 3.4 kwa Shule ya Nguruka ya Uvinza, na madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 3.075 kwa Shule Msingi Sokoine ya Kigoma Vijijini pamoja na madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 4 Shule Msingi Kabulazili ya Kasulu Mjini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum- Dkt. Doroth Gwajima anatarajiwa kuzindua kampeni ya ‘Badilika, Tokomeza Ukatili’ yenye lengo la ukatili wa kijinsia mkoani Kigoma.

Uzinduzi huo umepangwa kufanyika Jumatatu Julai 28, 2025 katika uwanja wa Mwanga Community Centre ambapo kampeni hiyo inatarajiwa kuleta hamasa makundi ya kijamii kuwa wanamabadiliko kupitia elimu itakayotolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za watoto na wanawake la KIVULINI, Yassin Ally amesema kampeni hiyo inawezeshwa na shirika la maendeleo la Ubelgiji (ENABEL), linalosaidia utekelezaji wa miradi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia mkoani Kigoma.

Elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi inatarajiwa kutolewa kwenye uzinduzi huo huku burudani ikinogeshwa na msanii wa nyimbo za Singeli, Dogo Paten.
Tazama Video hapa chini

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (wakwanza kushoto) akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa makazi ya watumishi wa umma Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (aliyevaa miwani) akisisitiza jambo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kijiweni, Bw. Hassan Kalembo (wapili kutoka kulia) na Mwalimu wa Taaluma wa Shule hiyo, Bw. Samson Bihole mara baada ya Katibu Mkuu huyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa makazi ya watumishi wa umma katika Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (kushoto) akitoka kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa makazi ya watumishi wa umma katika Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kijiweni, Bw. Hassan Kalembo.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (watano kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi kutoka katika ofisi yake na Viongozi na Watendaji wa Shule ya msingi Kijiweni mara baada ya Katibu Mkuu huyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa makazi ya watumishi wa umma katika Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi

Mwonekano wa jengo la mradi wa makazi ya watumishi wa umma lililopo katika Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.

Na Veronica Mwafisi-Lindi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma unaojengwa katika Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ili kuwasaidia watumishi hao kuwa karibu na ofisi wanazofanyia kazi kwa lengo la kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo leo, Katibu Mkuu Mkomi amesema ujenzi wa makazi ya watumishi hao utawasaidia kuepeukana na changamoto ya makazi ambayo imekuwa ikiwakabili na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiwajali sana watumishi wa umma katika kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo utekelezaji wa mradi wa makazi ya watumishi.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuujenga utumishi wa umma pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi wa umma ili wawe na tija katika utoaji wa huduma kwa maendeleo ya taifa,” Katibu Mkuu Mkomi ameongeza.

Bw. Mkomi amesema mradi wa ujenzi wa makazi hayo ya watumishi upo katika hatua ya majaribio katika Manispaa ya Lindi, mkoa wa Lindi ambapo pia unatekelezwa katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Ruvuma.

Katibu Mkuu Mkomi katika ziara hiyo aliambatana na baadhi ya Wakurugenzi wa ofisi yake ambapo kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Bw. Patrick Allute amesema Watumishi Housing Investments ndiyo kandarasi inayojenga makazi katika mradi huo.

Bw. Allute ameongeza kuwa, mradi huo unafuatiliwa na kusimamiwa kikamilifu ili uweze kukamilika kwa wakati.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma kwa ajili ya Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ana ule wa Afrika Mashariki ukiimbwa katika Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa, Mtumba Jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiweka silaha za jadi ikiwemo mkuki na ngao katika mnara wa Mashujaa kwenye Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika Mtumba Jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025.
Matukio mbalimbali kwenye Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mtumba Jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025.
Viongozi, wananchi, wageni mbalimbali wakiwa kwenye Maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa katika uwanja wa Mashujaa Mtumba Jijini Dodoma tarehe 25 Julai, 2025.