Articles by "MAMA SAMIA SULUHU"
Showing posts with label MAMA SAMIA SULUHU. Show all posts

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,ametoa tuzo kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa kampuni na wadau wengine katika juhudi zao za uhifadhi wa mazingira na kuliletea taifa maendeleo endelevu.

Tuzo hiyo ya kihistoria Pongezi ambao ni ya kwanza kwa SBL kutolewa na kingozi mkuu wa nchi, zinaonesha dhamira ya dhati ya kampuni hiyo katika utekelezaji wa mipango ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG).
Kupitia programu zake mbalimbali, SBL hadi sasa imefanikiwa:

● Kupanda miti zaidi ya 10,000 katika Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kati

● Kutekeleza miradi ya maji safi na salama zaidi ya 28 kwa jamii zinazozunguka maeneo yake ya uzalishaji

● Kuwekeza katika kilimo endelevu kwa kuunga mkono vijana zaidi ya 300 kupitia mpango wa Kilimo Viwanda

Aidha, SBL imeanzisha mpango wa Shamba ni Mali, unaolenga kuwapatia wakulima mbolea, mbegu bora, teknolojia ya kisasa na elimu ya kilimo, na lengo la kuwafikia wakulima zaidi ya 4,000 ifikapo mwaka 2030.

Utambuzi huu unaakisi mchango wa SBL kama mdau anayejali mazingira na kuthamini jamii anazozihudumia, sambamba na kuunga mkono ajenda ya Taifa ya maendeleo endelevu


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipanda mti wa Muembe (Mangifera indica) katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Zanzibar. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepitisha majina ya wanachama walioteuliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa chama na uwakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi, kufuatia kikao chake kilichofanyika Januari 25, 2026 mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Labani Kihongosi, uteuzi huo umezingatia taratibu na kanuni za chama, pamoja na vigezo vya uwakilishi wa kijinsia na makundi mbalimbali.

Wagombea kutoka Tanzania Bara

Katika nafasi za Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wanaotokana na Bunge kutoka Tanzania Bara, Kamati Kuu imepitisha:

● Wanaume (nafasi 2): Paul Christian Makonda na Livingstone Joseph Lusinde

● Wanawake (nafasi 1): Asia Abdulkarim Halamga

Wagombea kutoka Zanzibar

Kwa upande wa Zanzibar, walioteuliwa ni:

Wajumbe wa NEC kutoka Bunge:

● Wanaume: Khamis Mussa Omar

● Mwanamke: Tauhida Cassian Galos

Nafasi nyingine za kitaifa

Katika nafasi ya Katibu wa Wabunge wote wa CCM, ameteuliwa Agnes Elias Hokororo.

Kwa nafasi za Wenyeviti wa Bunge, waliopitishwa ni:

● Najma Murtaza Giga

● Deodatus Philippo Mwanyika

● Cecilia Daniel Pareso

Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, walioteuliwa ni pamoja na:

Wajumbe wa NEC kutoka Baraza la Wawakilishi:

● Wanaume: Said Ali Juma na Hamza Hassan Juma

● Mwanamke: Lela Muhamed Mussa

Aidha, Kamati Kuu imepitisha pia majina ya wawakilishi wa CCM watakaoingia Bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo:

● Wanaume: Bakar Hamad Bakar, Dkt. Shaame Ali Ali, na Simai Mohammed Said

● Mwanamke: Fatma Ramadhan Mandoba

Nafasi ya Katibu wa Wawakilishi wote wa CCM imeenda kwa Machano Othman Said, huku nafasi za Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi zikiwapitisha Mahmoud Omar Hamad na Hudhaima Mbarak Tahir.

Mchakato wa Uchaguzi Mdogo Peramiho

Katika taarifa hiyo, Kamati Kuu imefanya pia uteuzi wa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho (Mkoa wa Ruvuma), na kumpitisha Dkt. Lazaro Killian Komba kugombea ubunge, kufuatia mamlaka ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 (Toleo la Julai 2025).

CCM yasema ni kuimarisha demokrasia ya ndani

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi huo una lengo la kuimarisha uwakilishi, kuongeza ufanisi wa uongozi na kuendeleza misingi ya demokrasia ya ndani ya chama, sambamba na kuhakikisha makundi yote yanapata nafasi stahiki katika vyombo vya maamuzi.

CCM imewahimiza walioteuliwa kuzingatia maadili, umoja na mshikamano, huku ikiwataka wanachama na wananchi kuendelea kukiamini chama katika kuendeleza maendeleo ya taifa.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza zoezi maalum la upandaji miti kitaifa litakalofanyika tarehe 27 Januari, 2026 katika eneo la Bungi Kilimo, Kizimkazi, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, zoezi hilo lenye kaulimbiu “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti” linaakisi dhamira ya Rais Samia katika kulinda na kutunza mazingira, ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa zoezi hilo si tu la kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Rais, bali pia ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja na fursa kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kujenga utamaduni wa kulinda mazingira kwa kupanda miti mara kwa mara, akisisitiza kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi wa maisha, maendeleo na usalama wa taifa.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imewahimiza wananchi, taasisi, mashirika pamoja na wadau wa mazingira kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki katika utekelezaji wa agenda ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kampeni ya kupanda angalau mti mmoja nyumbani, shuleni, kazini na katika maeneo ya jamii.

Taarifa hiyo imetolewa Zanzibar tarehe 22 Januari, 2026 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, pamoja na Wawakilishi wa Heshima katika sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, pamoja na Wawakilishi wa Heshima wakiwa kwenye sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Amidi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Comoro nchini Tanzania Mhe. Ahmada El Badaoui Mohamed Fakih, akizungumza kwenye sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Thabit Kombo akizungumza kwenye sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Amidi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Comoro nchini Tanzania Mhe. Ahmada El Badaoui Mohamed Fakih, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Thabit Kombo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Mululi Majula Mahendeka kwenye picha ya pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania katika sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party), Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Amidi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Comoro nchini Tanzania Mhe. Ahmada El Badaoui Mohamed Fakih, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Thabit Kombo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu. Mululi Majula Mahendeka kwenye picha ya pamoja na Wawakilishi wa Heshima na Kaimu Mabalozi katika sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party), Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Amidi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Comoro nchini Tanzania Mhe. Ahmada El Badaoui Mohamed Fakih, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Thabit Kombo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Ikulu Ndugu. Mululi Majula Mahendeka kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa katika sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party), Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
Buyu, Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika sekta za elimu, sayansi, utafiti na ubunifu ili kujenga uchumi imara, shindani na endelevu, unaowanufaisha Watanzania kwa upana zaidi.

Rais Samia ameyasema hayo Januari 8, 2026, katika eneo la Buyu, visiwani Zanzibar, mara baada ya kuzindua Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Zanzibar (UDSM–IMS). Amesisitiza kuwa taasisi hiyo ni mdau muhimu wa Serikali katika kukuza uchumi shirikishi, hususan uchumi wa buluu, unaotegemea rasilimali za bahari.

Amesema uwepo wa IMS utaimarisha uvuvi endelevu, utalii wa baharini, pamoja na ulinzi na matumizi bora ya rasilimali za bahari, hivyo kuchangia moja kwa moja katika kukuza pato la Taifa na ustawi wa wananchi.
Katika hotuba yake, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa usimamizi mzuri wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), akisema mradi huo umeleta matokeo chanya katika miundombinu na ubora wa elimu ya juu nchini. Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kupata elimu na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Rais pia amewapongeza viongozi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vya juu, huku akiishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mradi wa HEET.

Aidha, amewataka wahadhiri na watafiti kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili tafiti na bunifu zitakazofanywa ziweze kuleta matokeo ya moja kwa moja katika maendeleo ya Taifa. Vilevile, amewahimiza wanafunzi kuwa walinzi na mabalozi wa rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ameiomba Serikali kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuanzisha Awamu ya Pili ya Mradi wa HEET, itakayowezesha kukamilisha maeneo ya utekelezaji ambayo bado hayajakamilika.

Dkt. Kikwete amesema majengo mapya yaliyozinduliwa ni msingi muhimu wa kuendeleza tafiti za kisasa, kutoa mafunzo bora na kukuza uchumi wa buluu, sambamba na kuchochea maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema uwekezaji huo utaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS). Amesema kwa sasa IMS ina uwezo wa kudahili takribani wanafunzi 172 kwa mwaka, lakini baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, uwezo utaongezeka hadi wanafunzi 472 kwa mwaka, sawa na ongezeko la wanafunzi 300.

Prof. Anangisye ameongeza kuwa IMS inaingia awamu mpya ya maendeleo kufuatia uzinduzi wa miundombinu ya kisasa katika eneo la Buyu, pamoja na kuimarishwa kwa vituo vya Mizingani na Pangani, hatua itakayoongeza uwezo wa taasisi katika kufundisha, kufanya tafiti na kuendeleza bunifu zitakazochangia maendeleo ya Taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Isaac Njenga Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2025. Balozi wa Kenya Mhe. Isaac Njenga alifika Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuaga Mhe. Rais Dkt. Samia ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia kuimarika kwa uhusiano wa kibiashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Kenya.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Kenya nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Isaac Njenga Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uapisho wa Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 18 Novemba, 2025.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaingia katika kipindi chake cha pili ikiwa na mkakati mahsusi wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje, kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi.

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akiwaapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma, ambapo amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatoa matokeo ndani ya muda mfupi, kwa kuzingatia uwajibikaji na uadilifu.
Amesisitiza kuwa dhamana waliyopewa haina nafasi ya uzembe, na kwamba Serikali haitasita kuwawajibisha watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Ameongeza kuwa jukumu kubwa lililo mbele ya Mawaziri na Manaibu ni kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inaenda sambamba na matarajio ya wananchi.

Katika kuelekea utekelezaji wa mpango wa siku 100 wa Serikali, Rais Samia amewaagiza Mawaziri kushirikiana kwa karibu na Makatibu Wakuu wa Wizara zao ili kuanza mara moja kutimiza majukumu waliyopewa. Ameeleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani halisi ya matumizi ya fedha.
Vilevile, Rais Samia amewataka viongozi walioteuliwa kuwa mfano wa utendaji bora, nidhamu na uadilifu, akisema kuwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wanatazama namna wanavyoongoza na kusimamia majukumu yao.

Akiwapongeza viongozi waliomaliza muda wao katika awamu ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita, Rais Samia amesema wametoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuhakikisha maendeleo hayakwami licha ya changamoto za upatikanaji wa fedha kutoka nje.

Mwisho, Rais Samia amewatakia heri Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya walioteuliwa, akiwataka kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Serikali inaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.