Na Mwandishi Wetu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Uganda zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za miundombinu, biashara, nishati na usalama kwa lengo la kuchochea maendeleo ya pamoja na ya kikanda.
Akizungumza leo Februari 7, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya mazungumzo yake na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Dk. Samia alisema viongozi hao wamejadili masuala ya kimkakati yanayohusu ustawi wa kiuchumi wa nchi zao.

Dk. Samia alisema wamezungumzia mradi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda kupitia Tanzania pamoja na mpango wa kusafirisha mafuta yaliyosafishwa kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga kwa ajili ya masoko ya nje.

Alisema korido hiyo hiyo itatumika pia kusafirisha mafuta safi kutoka Uganda hadi Tanga, hatua itakayoongeza ufanisi wa usafirishaji na kukuza biashara ya kimataifa.

Viongozi hao pia walijadili matumizi ya bandari za Tanzania hususan Dar es Salaam na Tanga, ambazo ni muhimu kwa nchi zisizo na bandari ikiwemo Uganda, ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.

Katika sekta ya reli, Rais Samia alisema Tanzania inapanga kujenga reli itakayounganisha Mkoa wa Tanga hadi Musoma, itakayorahisisha usafiri wa mizigo kupitia Ziwa Victoria hadi Uganda.

Aidha, walijadili upanuzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Isaka hadi Lusahunga, huku Uganda ikiombwa kuunganisha reli hiyo kuelekea Murongo ndani ya nchi yao.
Rais Samia pia alitaja kuanza kwa huduma za meli ya MV Mwanza katika Ziwa Victoria, akisema meli hiyo itaimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Tanzania na Uganda.

Kuhusu biashara, alisema wamekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyokwamisha biashara ya ndani ya Afrika Mashariki ili kujenga soko la pamoja lenye ushindani.

Katika ngazi ya kimataifa, Dk. Samia alimshukuru Rais Museveni kwa kuunga mkono Tanzania katika kinyang’anyiro cha kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku Tanzania ikiiahidi Uganda ushirikiano katika Umoja wa Afrika.

Kuhusu usalama wa kikanda, Rais Samia alisema Tanzania inaunga mkono juhudi za Rais Museveni kama Mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu katika kuleta amani na utulivu kwenye eneo hilo.

Kwa upande wake, Rais Museveni alimshukuru Rais Samia kwa mapokezi mazuri na kusisitiza umuhimu wa kuwa na soko la uhakika na usalama imara ili wananchi wa Afrika Mashariki wanufaike na maendeleo ya kiuchumi.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: