Na Mwandishi Wetu, Manyara.

WANANCHI wa kaya maskini katika Kijiji cha Imbilili, Kata ya Sigino, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wameanza kunufaika na huduma za afya baada ya kuandikishwa na kukabidhiwa kadi za Bima ya Afya kwa Wote, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya.

Zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanoela Mtatifikolo Kaganda, pamoja na Ofisi ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Manyara.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhe. Sendiga alisema mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni nyenzo muhimu ya kuboresha ustawi wa wananchi na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu, hususan kwa kaya zisizo na uwezo wa kifedha.

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa huduma za afya kutokana na ukosefu wa bima, akisisitiza kuwa uandikishaji huo utaendelea kufanyika katika vijiji mbalimbali wilayani Babati na maeneo mengine ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa NHIF, Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa kila Mtanzania, ambapo kaya zinaweza kujiunga kwa gharama ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwaka kwa kaya isiyozidi watu sita, na kupata huduma katika hospitali zote nchini.
Kwa wananchi wasio na uwezo, wakiwemo wazee, watoto na watu wenye ulemavu, Serikali itaendelea kugharamia bima hiyo ili kuhakikisha wanapata huduma za afya bila kikwazo chochote.

Wananchi wa Imbilili waliopokea kadi hizo wameishukuru Serikali kwa mpango huo, wakisema utawasaidia kupata matibabu kwa wakati na kupunguza gharama ambazo hapo awali zilikuwa kikwazo kwao.

Zoezi hilo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote kwa usawa, hususan walioko vijijini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: