Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akishiriki mjadala katika Jukwaa la Serikali za Dunia (WGS2026), tarehe 4 Februari, 2026 Madinat Jumeirah, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Na Mwandishi Wetu

UZINDUZI rasmi wa Global Africa Investment Summit (GAIS) jijini Dubai umeashiria mabadiliko makubwa ya mtazamo kuhusu uwekezaji barani Afrika, ukilenga uaminifu wa taasisi, uthabiti wa sera na miundo imara kama msingi wa uwekezaji wa muda mrefu, badala ya kutegemea fursa za muda mfupi pekee.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa World Governments Summit, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amethibitisha utayari wa Tanzania kushiriki kikamilifu GAIS kama mshirika wa kimkakati anayelenga faida endelevu. Alisisitiza kuwa changamoto kuu ya Afrika si ukosefu wa rasilimali, bali ni miundo na mifumo ya kuziwezesha rasilimali hizo kuzalisha matokeo chanya.

Rais Dkt. Samia alitolea mfano uwekezaji unaotekelezwa Tanzania katika miundombinu ya kimkakati ikiwemo umeme wa maji, reli ya kisasa (SGR), bandari na barabara, pamoja na uthabiti wa sera na utekelezaji wa ahadi za Serikali kama nguzo za kuvutia wawekezaji wa kimataifa.

Kwa upande wake, Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mheshimiwa João Lourenço, alisema GAIS ni jukwaa muhimu linalosaidia Afrika kubadilisha namna inavyoshirikiana na mitaji ya kimataifa, akisisitiza kuwa Afrika lazima ichukue umiliki mkubwa wa maliasili zake na kuzisimamia kwa uwazi, ushindani na uwajibikaji.

Naye Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, alisema GAIS inaakisi ukomavu wa kisera wa Afrika na utayari wake wa kushirikiana na wawekezaji wa kimataifa kwa kuzingatia viwango vya juu vya utawala, uwazi na usimamizi wa vihatarishi. Aliongeza kuwa tatizo si ukosefu wa rasilimali bali ni miundo dhaifu, gharama kubwa za tathmini ya uwekezaji (due diligence) na mifumo ya utawala iliyogawanyika.

Katika hotuba zao, viongozi wengine akiwemo Rais wa Ghana, Mheshimiwa John Mahama, walisisitiza umuhimu wa mageuzi ya kisera, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), ubia wa kibiashara (joint ventures) na uanzishaji wa maeneo maalum ya kiuchumi (SEZs) ili kuharakisha viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kukuza mauzo ya nje.

Kwa Tanzania, GAIS inatarajiwa kufungua fursa za kimkakati za kuvutia mitaji binafsi na ya kimataifa katika maeneo ya bandari na biashara ya kikanda, nishati na viwanda, pamoja na kuiimarisha nchi kama kitovu cha uzalishaji na usafirishaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.

Global Africa Investment Summit ni jukwaa la uwekezaji linaloongozwa na Afrika, lililoanzishwa kwa ushirikiano wa viongozi wa Afrika na wadau wa maendeleo ya kimataifa, likilenga kuibadilisha Afrika kutoka utegemezi wa misaada kwenda kwenye ukuaji unaoongozwa na uwekezaji, ubunifu na ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: