Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani (wa pili kushoto), akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kambi ya Huduma za Afya iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania Foundation, yenye lengo la kutoa huduma bure za upimaji wa afya, ushauri na elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu na kisukari. Kambi hiyo inatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine hivi karibuni. Tukio hilo limefanyika Visiwani Zanzibar na kushuhudiwa na Kaimu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi (kushoto), pamoja na Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald (wa pili kulia).

Na Mwandishi Wetu.

ZANZIBAR – Vodacom Tanzania Foundation imeanza rasmi utekelezaji wa kambi za afya bure Zanzibar kwa lengo la kusaidia jamii kupata uchunguzi wa mapema, elimu na huduma za kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), yakiwemo shinikizo la damu na kisukari, ambayo yameendelea kuwa changamoto kubwa kwa afya ya wananchi.

Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 34 ya magonjwa sugu nchini Tanzania yanahusishwa na magonjwa yasiyoambukiza, hali inayosababisha madhara makubwa kiafya endapo hayatagunduliki mapema. Zanzibar imekuwa miongoni mwa maeneo yenye ongezeko la wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari, hali iliyochochea haja ya kuimarisha jitihada za kinga na uchunguzi wa afya katika jamii.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Vodacom Tanzania Foundation inaendelea na mpango wake wa muda mrefu wa kambi za afya bila malipo, ambao umeanza kutekelezwa Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka huu. Mpango huo umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika mikoa saba na wilaya 16 nchini, ukiwa na lengo la kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

Kambi ya afya inayofanyika kuanzia Februari 3 hadi 6, 2026 inalenga kutoa huduma za upimaji wa afya, ushauri wa kitaalamu na elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza. Uzinduzi rasmi wa kambi hiyo ulifanyika Februari 4, 2026, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Marijani alisema magonjwa ya shinikizo la damu na kisukari mara nyingi hayana dalili za awali, hivyo uchunguzi wa mapema ni muhimu katika kuzuia madhara makubwa ya kiafya. Alipongeza mchango wa Vodacom Tanzania Foundation katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha afya ya jamii kupitia mipango ya kinga na elimu.

Kwa upande wake, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Sandra Oswald, alisema kambi hizo zimebuniwa mahsusi ili kupeleka huduma za afya moja kwa moja kwa wananchi, hususan wale wenye ufinyu wa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa mara kwa mara. Alisema kuanza kwa mpango huo Zanzibar ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma na kuongeza athari chanya kwa jamii.

Aliongeza kuwa Vodacom Tanzania Foundation itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya pamoja na wadau mbalimbali ili kuendeleza na kupanua mpango huo katika maeneo mengine ya nchi, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kufanikisha Lengo la Maendeleo Endelevu namba 3 (SDG 3) la Afya Njema na Ustawi.

Foundation hiyo imewahimiza wakazi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kambi hizo za afya, ikisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema, elimu na hatua za kinga ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye afya njema na ustawi endelevu.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: