Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya kitabu kutoka kwa Makamu wa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, mara baada ya mazungumzo kati yao, kando ya Mkutano wa Dunia (WGS2026) hapa, Dubai, tarehe 04 Februari, 2026. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Makamu wa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, kando ya Mkutano wa Dunia (WGS2026) hapa, Dubai, tarehe 04 Februari, 2026.
Na Mwandishi Wetu
TANZANIA na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimekubaliana kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uwekezaji, biashara na ustawi wa uchumi wa pande zote mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo ya pande mbili kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa UAE pamoja na Mtawala wa Dubai, Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa World Governments Summit (WGS) 2026 jijini Dubai.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha utekelezaji wa Mikataba ya Ushirikiano wa Biashara (CEPA) na Mikataba ya Uwekezaji wa Nchi na Nchi (BIT), hatua inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji baina ya Tanzania na UAE.
Aidha, wamejadili utekelezaji wa miradi ya pamoja ikiwemo kuanzishwa kwa safari mpya za ndege za Shirika la Ndege la Emirates, zikiwemo safari za Kilimanjaro na Zanzibar, kwa lengo la kukuza sekta ya utalii, biashara na usafirishaji wa anga.
Rais Dkt. Samia amewasilisha uzoefu wa Tanzania katika kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kisheria, ikiwemo maboresho ya sera, sheria na taratibu za uwekezaji, akisisitiza umuhimu wa uthabiti wa sera, uwazi wa mifumo ya utawala na ulinzi wa maslahi ya wawekezaji kama msingi wa kujenga imani ya muda mrefu kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameainisha uwekezaji mkubwa unaotekelezwa na Serikali katika miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa (SGR), bandari za Bahari ya Hindi na maziwa makuu pamoja na mtandao wa barabara, akibainisha kuwa hatua hizo zimeipanga Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameshiriki katika mjadala wa kimataifa kuhusu uwekezaji uliofanyika ndani ya Mkutano wa World Governments Summit 2026, wenye mada “Serikali na Mustakabali wa Uwekezaji: Mtazamo wa Afrika”, uliolenga kujadili nafasi ya serikali katika kuvutia mitaji na kukuza uchumi barani Afrika.
Kwa upande wake, Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa karibu na Tanzania kupitia miradi ya maendeleo, akisisitiza dhamira ya UAE katika kukuza ustawi wa kiuchumi wa pande zote mbili.
Kwa mujibu wa maelezo kwa vyombo vya habari, uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na UAE umeendelea kuimarika kwa kasi, ambapo thamani ya biashara imeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 985.31 mwaka 2018 hadi dola bilioni 2.1 mwaka 2024, na kuifanya Tanzania kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa UAE barani Afrika.



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: