Articles by "KITAIFA"
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts
New York, Marekani

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza hatua zake za kuanza kutekeleza Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2026/27–2030/31 (FYDP IV), ambao ni mpango wa kwanza wa muda wa kati wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yamelezwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais–Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Mbaga Kida, wakati wa mkutano wa pembezoni mwa Jukwaa la Ngazi ya Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa linalosimamia Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (HLPF 2026), uliofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Mkutano huo, wenye mada “Driving Industrial and Inclusive Economic Transformation: Financing, Innovation and Sustainable Growth in Agricultural and Blue Economy Value Chains”, uliandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), pamoja na UNDP, UNIDO na washirika wengine.

Dkt. Kida alisema Tanzania inaingia katika awamu mpya ya utekelezaji wa maendeleo inayolenga kubadilisha mafanikio ya ukuaji wa uchumi na uwekezaji katika miundombinu kuwa ongezeko la uzalishaji, ajira zenye tija, mauzo ya nje, ongezeko la thamani ya bidhaa na ustawi mpana wa wananchi.

Dkt. Kida alisema uchumi wa Tanzania kwa sasa unakua kwa asilimia 5.9 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 ifikapo mwisho wa mwaka huu. Ukuaji huo ulichangiwa na kuimarika kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji na huduma, pamoja na kuendelea kwa uwekezaji katika miundombinu na miradi ya kimkakati.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa lengo si kasi ya ukuaji pekee, bali ukuaji unaogusa maisha ya wananchi wote. “Lengo letu si kuongeza ukubwa wa uchumi pekee. Tunataka ukuaji unaoongeza kipato cha wananchi, unaotengeneza ajira, unaopunguza umaskini na unaowezesha wanawake, vijana, wakulima wadogo na wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika uchumi,” alisema Dkt. Kida.

Dkt. Kida alibainisha kuwa kilimo, misitu na uvuvi vinaendelea kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania, vikichangia asilimia 24.3 ya Pato la Taifa mwaka 2025. Alisema mchango wa uvuvi katika Pato la Taifa uliongezeka kutoka asilimia 1.9 mwaka 2020 hadi asilimia 2.2 mwaka 2025, hatua inayoonesha fursa zinazoongezeka katika uchumi wa buluu.

“Tunataka kuondoka katika uchumi unaouza malighafi na kuelekea uchumi unaosindika, unaoongeza thamani, unaotumia teknolojia na unaounganisha wazalishaji wa ndani na masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa,” alisema.

Dkt. Kida pia alisema Tanzania itawasilisha Mapitio ya Tatu ya Hiari ya Nchi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu tarehe 14 Julai 2026.

Mapitio hayo yanaonesha maendeleo yaliyopatikana katika maji safi, nishati, miundombinu, afya, usafiri, teknolojia ya kidijitali na uimarishaji wa rasilimali za ndani.
Kwa upande wake, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Mhe. Togolani Edriss Mavura, alisema mageuzi ya viwanda barani Afrika yanapaswa kuwa jumuishi na kuwanufaisha wakulima wadogo, wanawake, vijana, wavuvi, wafugaji, biashara ndogo na washiriki wa sekta isiyo rasmi.

Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika teknolojia, uwekezaji, masoko, ujuzi, fedha za maendeleo na ujenzi wa minyororo ya thamani inayounganisha nchi za Afrika.
Ofisa Mkuu wa Fedha wa UNCDF, Bw. Karen Vardanyan, aliitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoonesha namna fedha bunifu zinavyoweza kutumika kuharakisha maendeleo katika ngazi ya taifa na mamlaka za serikali za mitaa.

Alieleza kuwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025. Maendeleo hayo yanaungwa mkono na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, uwekezaji wa sekta binafsi na juhudi za Serikali za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Bw. Vardanyan pia alitaja Tanga UWASA Green Revenue Bond, iliyokusanya dola za Marekani milioni 20.8 kwa ajili ya miundombinu ya maji inayohimili mabadiliko ya tabianchi. Hatifungani hiyo ilikuwa ya kwanza ya kijani katika ngazi ya mamlaka ya chini ya kitaifa Afrika Mashariki, huku wawekezaji wa ndani wakichangia asilimia 65 ya uwekezaji wote.

Mifano mingine iliyotajwa ni PesaTech Accelerator, inayosaidia ubunifu wa huduma za kifedha na biashara zinazoongozwa na vijana, pamoja na mfumo wa LoCAL unaowezesha mamlaka za serikali za mitaa kuongeza uwekezaji unaohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Bw. Vardanyan alitoa wito kwa Serikali, taasisi za fedha, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kubadili ahadi za kimataifa kuwa miradi inayoweza kufadhiliwa na uwekezaji halisi katika kilimo, uchumi wa buluu, viwanda, maji, nishati na miundombinu.

Mkutano huo ulihitimisha kuwa utekelezaji wa Dira 2050 na FYDP IV utahitaji ushirikiano madhubuti kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, Umoja wa Mataifa, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na jamii.

Dira 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati cha juu, yenye Pato la Taifa la dola za Marekani trilioni moja, pato la wastani kwa mtu linalozidi dola 7,000 na kuondoa umaskini ifikapo mwaka 2050.

 

Vodacom Tanzania Plc, kampuni pekee ya mawasiliano iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), imetambuliwa kama mmoja wa walipa kodi wakubwa nchini. 
Utambuzi huu unaonyesha dhamira ya kampuni kuendesha biashara kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria, huku ikichangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa kupitia ulipaji kodi na uwekezaji.

Akipokea tuzo ya mlipakodi mkubwa kutoka sekta ya Mawasiliano iliyotolewa na mamlaka ya mapato (TRA) jana jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom alisisitiza kuwa mafanikio ya kampuni hayapo tu kwenye kutoa huduma za mawasiliano, bali pia katika kuchangia maendeleo ya taifa kupitia kodi, uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali, ubunifu na kukuza rasilimali watu.
Kadri Tanzania inavyotekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Vodacom imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuwekeza katika teknolojia za kidijitali, miundombinu ya mawasiliano na ujuzi, ili kuharakisha ujumuishi wa kidijitali na kukuza maendeleo jumuishi ya kiuchumi.

Kwa zaidi ya miaka 20, Vodacom imekuwa kichocheo cha mageuzi ya kidijitali nchini kwa kuunganisha watu, biashara na taasisi kupitia huduma za mawasiliano na suluhisho za kidijitali zinazoboresha maisha ya Watanzania na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akisalimiana na Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho wa kibalozi katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Katikati ni Mheshimiwa Ahmed Attaf, Waziri wa Mambo wa Nje wa Algeria.
Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akizungumza na waandishi wa habari wa Algeria mara baada ya kukabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Kushoto kwake ni Mwambata wa Ulinzi Kanali Nassoro Kapolo na kushoto kwake ni Afisa wa Ubalozi, Maryam Kilongo.

Na Mwandishi Wetu

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amekabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Algiers, Juni 10, 2026, kuashiria kuanza rasmi kwa majukumu yake ya kuiwakilisha Tanzania nchini humo.

Baada ya hafla hiyo, Balozi Matinyi alimfikishia Rais Tebboune salamu na shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuthamini uhusiano wa kindugu na ushirikiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 kati ya Tanzania na Algeria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Balozi Matinyi alisema mazungumzo yao yalijikita katika namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo, hasa baada ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta za ulinzi na elimu ya juu. Alisema pande hizo mbili zimekubaliana kuweka msukumo mpya katika sekta nyingine zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.

Alitaja maeneo ya kipaumbele yaliyopatiwa msisitizo kuwa ni kilimo, viwanda, utengenezaji wa dawa, nishati, madini na utalii, pamoja na kuendeleza ushirikiano katika sekta za sayansi, teknolojia, utafiti, utamaduni na elimu ili kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili.

"Nimepewa jukumu na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ushirikiano wa Tanzania na Algeria unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili. Kwa kutumia umahiri wa viongozi wetu, tunaamini tutafanikisha azma hiyo," alisema Balozi Matinyi.

Kwa upande wake, Rais Tebboune alieleza utayari wa Algeria kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo, akibainisha kuwa nchi yake iko tayari kufikia makubaliano mapya kupitia vikao vya pamoja na ziara za viongozi wa ngazi za juu.

Balozi Matinyi anakuwa balozi wa nne wa Tanzania nchini Algeria, akitanguliwa na Balozi Omari Yussuf Mzee, Meja Jenerali Jacob Kingu na Balozi Imani Njalikai. Mbali na Algeria, Ubalozi wa Tanzania uliopo Algiers unahudumia pia nchi za Tunisia, Mauritania, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR).

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Massad Boulos, mwanadiplomasia na Mshauri Mwandamizi wa Rais Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika, nchi za Kiarabu na Mashariki ya Kati, baada ya kufanya mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa Oslo Forum unaofanyika Oslo, Norway.

Mkutano huo, unaofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni, 2026, umewakutanisha viongozi, wanadiplomasia waandamizi na wadau wa masuala ya amani, diplomasia na usuluhishi kutoka nchi mbalimbali zenye ushawishi duniani.

Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Petersburg, Urusi

Ulimwengu wa sasa wa diplomasia ya kijiografia unatawaliwa na ushindani mkubwa wa nguvu za kisiasa na kiuchumi kati ya mataifa makubwa ya Magharibi na yale ya Mashariki. 

Katika mazingira haya, mataifa yanayoendelea mara nyingi hujikuta yakitazamwa kwa darubini ya shaka pale yanapochukua hatua za kimkakati kupanua wigo wa washirika wao wa kimaendeleo. 

Ziara ya hivi karibuni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, imezua minong'ono na hisia mbalimbali miongoni mwa wachambuzi wa mambo, wengi wao wakihofia kuwa huenda Tanzania sasa inabadili mwelekeo wake wa sera ya mambo ya nje kwa kuitupa mkono Magharibi na kugeukia upande wa Mashariki. 

Hofu hii haina msingi wowote, kwani majibu thabiti na ya kizalendo aliyoyatoa Rais Samia mbele ya waandishi wa habari pembezoni mwa Jukwaa la Kimataifa ya Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) nchini Urusi, yanadhihirisha ukomavu wa diplomasia ya Tanzania inayojali maslahi ya taifa kwanza kabisa.

Katika mazungumzo hayo maalum yaliyowashirikisha waandishi wa habari 13 walioambatana naye, akiwemo mwakilishi kutoka Mtandao wa Bloggers Tanzania (TBN), Rais Samia alikuwa wazi na alinyoosha maelezo bila kusita. 

Alifafanua kuwa Tanzania haihamishi nguvu zake kutoka upande mmoja kwenda mwingine, bali inaongeza wigo wa washirika ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya kiuchumi yanatimizwa kwa faida ya wananchi wake. 

Hii ina maana kwamba wale wote wenye hofu au mashaka kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Urusi wanapaswa kuondoa shaka hiyo mara moja, kwani serikali haifuati mtu au upande wowote wa kiitikadi, bali inafuata yeyote mwenye nia njema ya kushirikiana katika kuinua maisha ya Watanzania.

Msimamo huu wa Rais Samia si jambo geni wala la kubahatisha, bali ni muendelezo wa misingi imara ya kihistoria iliyowekwa na Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Miaka 57 iliyopita, Mwalimu Nyerere alipotembelea Urusi (wakati huo ikiwa Muungano wa Sovieti), alitamka maneno yaleyale yanayosikika leo kutoka kwa Rais Samia: kwamba Tanzania ni nchi isiyofungamana na upande wowote. Mwalimu alisisitiza kuwa Tanzania itajichanganya na marafiki zake kwa jinsi marafiki hao wanavyotaka kuwa na Tanzania, mradi tu hawataingilia uhuru na mamlaka ya nchi. Falsafa hiyo ya kihistoria ndiyo inayomwongoza Rais Samia hadi leo katika ulimwengu huu unaozidi kuwa na vitovu vingi vya nguvu ya kiuchumi na kiteknolojia.

Sera ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote (Non-Aligned Policy) imekuwa silaha kuu ya kulinda uhuru wa Tanzania wa kufanya maamuzi ya kimkakati. Katika kile kinachoitwa Diplomasia ya Maslahi ya Kitaifa (National-Interest Diplomacy), kigezo kikuu cha kupima ubora wa uhusiano wa kimataifa si itikadi za kisiasa, bali ni mchango gani uhusiano huo unaingiza katika uchumi wa nchi, ajira kwa vijana, na uhamishaji wa teknolojia. 

Rais Samia alifafanua kuwa ziara yake nchini Urusi ilikuja na maombi saba ya kimkakati kutoka Tanzania, na wenyeji wao wa Urusi wakavutiwa kiasi cha kuongeza maombi mengine mawili na kufanya jumla ya maeneo tisa ya ushirikiano. Hii inadhihirisha kuwa pande zote mbili zinazungumza lugha moja inayolenga ustawi wa kiuchumi na maendeleo ya jamii.

Ili kuelewa kwa nini Tanzania inapaswa kuendelea kushirikiana na Urusi pamoja na ulimwengu mzima, ni lazima kuangalia uwiano wa washirika wetu duniani kote. 

Serikali ya Awamu ya Sita haijafunga milango kwa mataifa ya Magharibi; badala yake washirika wetu wa kitamaduni wanaendelea kuwa nguzo muhimu. Kwa mfano, Marekani bado ni mshirika mkubwa sana wa kiuchumi na kibiashara nchini Tanzania, ikiongoza katika kuleta watalii wengi na kuwekeza kupitia kampuni kubwa zaidi ya 500 zilizopo nchini, hususan katika sekta ya madini na uwekezaji mbalimbali wa kimkakati. Vivyo hivyo, mataifa ya Ulaya yameendelea kuwa washirika wakuu katika biashara na utoaji wa misaada pamoja na uwezeshaji wa kifedha. Uhusiano huu wa karibu na Magharibi haujatikisika, na unazidi kuimarika kila uchao.

Wakati huo huo, Tanzania imeendelea kunufaika na uhusiano mkubwa na mataifa ya Asia. China imekuwa mshirika mkuu wa kihistoria na wa sasa katika kuwezesha miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi, huku India nayo ikiwa miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara .

Japan haikuachwa nyuma, kwani imeendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta za nishati, elimu, na ujenzi wa miundombinu ya kijamii. Hata mataifa mengine kama Australia, Uingereza, na Ufaransa yamekuwa yakija nchini kwa kasi kupitia mipango mbalimbali kama vile mpango wa Matei wa Ufaransa ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi. 

Kwa mtazamo huu, Urusi inaingia kama mshirika mwingine muhimu wa kimkakati baada ya Tanzania kumaliza changamoto zilizotokana na masharti magumu ya mabadiliko ya kiuchumi ya Benki ya Dunia katika miaka ya 1980, ambayo wakati huo yalilazimu Tanzania kuangalia upande mmoja tu wa mlango.

Ni dhahiri kuwa Diplomasia ya sasa ya Tanzania inatawaliwa na ukomavu na uhuru wa kuchagua. Kama alivyowahi kunukuu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kuhusu methali maarufu ya kiuchumi: "Tanzania haihitaji kujua rangi ya paka, mradi tu paka huyo ana uwezo wa kukamata panya." 

Maneno haya yana maana kwamba Tanzania haichagui wala haibagui mshirika kwa kuangalia sura au mfumo wake wa kisiasa, bali inaangalia uwezo na utayari wa mshirika huyo kushirikiana nayo katika kutatua changamoto za umaskini na kukuza uchumi. Kila taifa linaloheshimu mamlaka ya Tanzania na liko tayari kuchangia katika ustawi linakaribishwa kwa mikono miwili.

Mkakati huu wa kutafuta washirika wengi kwa wakati mmoja una umuhimu mkubwa sana katika kulinda usalama wa kiuchumi wa Tanzania. Hakika kuweka mayai yote kwenye kikapu kimoja ni hatari kubwa katika ulimwengu wa sasa uliopasuka kutokana na vikwazo vya kiuchumi na migogoro ya kikanda. Kuwa na washirika mbalimbali kunatoa nguvu kubwa ya majadiliano (bargaining power) kwenye meza za kimataifa, kwani hatutegemei chanzo kimoja tu cha mitaji au teknolojia. Kama soko moja likiyumba au kukiwa na mabadiliko ya kisiasa upande mmoja, Tanzania inaweza kuendelea kusonga mbele kwa kutumia milango mingine iliyo wazi.

Kwa kuwa, dira yetu ya maendeleo ya taifa ya 2050 ndiyo dira kuu inayoongoza Tanzania hivi sasa ni vyema kama taifa kutumia diplomasia ya kiuchumi kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, lengo likiwa ni kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa na kufikia thamani ya uchumi wa dola bilioni 1,000 (trilioni moja) ifikapo mwishoni mwa utekelezaji wake. 

Ili kufikia lengo hili kubwa la kihistoria, serikali inahitaji mitaji mikubwa, miundombinu ya kisasa, na teknolojia ya hali ya juu kutoka kila kona ya dunia. Tanzania haiwezi kufikia malengo hayo makubwa kwa kujifungia milango au kwa kuchagua upande mmoja wa kidunia. Ndiyo maana Rais Samia anapiga hatua kwa ujasiri, akifungua milango kila mahali—iwe ni Washington, Beijing, Brussels, au Moscow—kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa yanalindwa na fursa za kiuchumi zinawafikia wananchi wote.

Kwa miaka mingi, chapa nyingi nchini Tanzania zipo kila mahali lakini ni ngumu mtu kuzikumbuka. Nembo kubwa jukwaani, DJ’s maarufu, vinywaji kwa bei nafuu, na watengeneza maudhui wa mitandoni wakituma video zisizofikisha ujumbe kamili kwenye mitandao ya kijamii ( Instagram). Baada ya hapo, kila mtu anarudi nyumbani kwake, hadi kufikia jumatatu tukio lote limesahaulika. 

Huo umekuwa ni ukweli mchungu kwa chapa nyingi zaidi barani Afrika. Kampuni inatumia fedha nyingi zaidi kujitangaza, lakini hushidwa kuacha historia isiyofutika kwa wateja na walaji wake. Kibaya zaidi, walaji nao wamegundua hilo. 

Siku hizi, watumiaji wana ladha tofouti. Hawavutiwi tena na uwepo wa chapa ya kampuni peke yake, bali ubunifu uliopo nyuma ya uwepo wa chapa hiyo. 

 Ndiyo maana, tukio walilolifanya Heineken hivi karibuni la Kuonesha fainali za ligi ya Mabingwa barani Ulaya limeacha historia ya kipekee. Tukio hilo liliibua gumzo kitaifa, sio kwa sababu ya mpira wa miguu tu, bali ni kwa sababu ilionesha kiwango kikubwa cha fursa ambazo bado watu wengi hawajazijua katika kubadilisha namna tunavyotengeneza burudani kwa watumiaji wetu nchini Tanzania.

Kwa usiku mmoja watanzania walipewa burudani kubwa yenye hadhi ya Kimataifa, yenye mvuto wa kisasa na mazingira yaliyobuniwa kwa hali ya juu na kukosha mioyo ya walaji wengi. Muonekano wa eneo lenyewe ilikuwa ni kivutio tosha. Makontena yaligeuka kuwa chanzo cha kivutio, ubunifu wa njia za juu uliwashangaza maelfu ya watu waliohudhuria. Skrini kubwa ilitawala na kufananisha uwoneshaji wa fainali hizo na tamasha kubwa la muziki kimataifa.

Watu hawakuhudhuria tu bali walishiriki historia. 

Tofouti hiyo ni muhimu sana, kwa sababu inawafanya walaji kujisikia umuhimu sana kuwepo katika tukio hilo kubwa. Kwa sababu hiyo itabaki kama historia kwenye maisha yao na sehemu ya utambulisho wao. Watu wanapenda kushiriki matukio yanaoakisi utu wao wa ndani, na mtindo wa maisha wanaoutamani.

Hali hii inaonekana zaidi kwa vijana wa mijini ambao sasa wanaishi katika ulimwengu uliounganishwa kidijitali. Wanatazama maisha ya usiku ya Lagos kupitia TikTok. Wanafuatilia tamasha za Amsterdam au London kupitia Instagram. Kila siku wanakutana na viwango vya kimataifa vya ubunifu na mandhari ya kisasa. Matarajio yao yamebadilika sana zaidi ya chapa za kampuni nyingi walipofikia.  

Hata hivyo kuna Chapa za Kampuni nyingi zaidi bado zinafanya kazi zikiwa na maono ya 2015. Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na dhana ya kwamba walaji wengi wa Afrika Mashiriki hawaitaji utekelezaji wa kiwango cha Kimataifa. Ndio maana wanafanya uzalishaji mdogo, ubunifu mdogo, miundombinu ya kawaida na sauti zisizoridhisha. Nembo za chapa ya kampuni kila mahali bila kuwa na hadithi ya kusimulia. Kauli yao maarufu huwa ni kuwa  “hiki kinatosha kwa soko letu”

.Lakini, pengine soko halikuwa tatizo hata siku moja, huenda tatizo lilikuwa ni ukosefu wa Ubunifu. 

Kwa sababu mwitikio ulioonekana siku ile ulithibisha jambo moja muhimu ambalo ni wananchi wana kiu na ubunifu wa viwango, wanataka vitu vipya, muonekano unaovutia na mradi utekelezwe kwa viwango vinavyohitajika.

Mitandao ya kijamii ililipuka kwa maudhui ya video. Video za drone zilisambaa kila mahali. Watu hawakushiriki tu mechi yenyewe, bali walionyesha mazingira, usanifu wa eneo, nguvu ya umati na ukubwa wa tukio. Hata watu ambao hawakuwa mashabiki wakubwa wa mpira walitamani kuhudhuria kwa sababu mazingira yenyewe yalikuwa kivutio cha kitamaduni.

Hilo linapaswa kuwafanya wataalamu wa masoko wengi kutafakari! Kwa sababu linaashiria mabadiliko makubwa katika namna walaji wanavyohusiana na chapa. Kwa sasa, uzoefu wenyewe unaanza kuwa bidhaa. Si kinywaji, si tiketi wala si udhamini bali ni uzoefu wenyewe. Na hapo ndipo chapa nyingi zinaanza kupoteza umuhimu wake.

Bajeti nyingi za masoko bado zimejikita katika kupima kiwango cha mwonekano badala ya athari za kihisia. Aktivisheni nyingi bado zinaundwa kwa lengo la kuridhisha ripoti za ‘PowerPoint’ na taratibu za manunuzi, badala ya kuunda nyakati ambazo watumiaji watazikumbuka kwa miaka mingi.

Matokeo yake ni sekta yenye matukio makubwa kwa ukubwa, lakini matupu kihisia. Yenye watu wengi, lakini yasiyokumbukwa.

Watumiaji wanaweza kutambua tofauti hiyo mara moja. Wanajua chapa inapojaribu kwa dhati kuunda utamaduni mpya na wanajua inapojaribu tu kujitangaza ndani ya utamaduni uliopo.

Ndiyo maana uzoefu huu wa Heineken ulipokelewa vizuri sana. Ulionekana kuwa wa makusudi. Uliundwa kwa umakini. Uliandaliwa kwa viwango vya juu. Uliwatendea watumiaji kama watu wanaostahili uzoefu wa kiwango cha kimataifa, si kama jambo la mwisho kufikiriwa.

Lakini hadhira ya leo haitoi tu pongezi kwa jitihada. Inatambua na kuthamini ubora. Na hilo linabadilisha kila kitu.

Kwa sababu mara tu watumiaji wanapopata uzoefu wa mazingira ya kuvutia, ya kiwango cha juu na yenye kuamsha hisia, huwa ni vigumu  kuridhika tena na aktivisheni za kawaida zilizojaa viti vya plastiki, msongamano wa watu, mifumo dhaifu ya sauti na mbinu zilezile zinazojirudia kila mwaka.

Kiwango kimepandishwa rasmi, na chapa ambazo zitashindwa kutambua mabadiliko haya zinaweza kuanza kupotea polepole katika mazungumzo ya kitamaduni na kijamii.

Hili si suala la burudani pekee. Ni suala la mustakabali wa masoko. Chapa zitakazoongoza katika miaka kumi ijayo si lazima ziwe zile zenye bajeti kubwa zaidi za matangazo bali zitakuwa zile zinazoweza kujenga ulimwengu ambao watu wanatamani kuwa sehemu yake.

Mustakabali ni wa chapa zinazoelewa umuhimu wa mazingira, simulizi, hisia na kujenga jamii zinazowaunganisha watu. Chapa zinazokoma kuingilia utamaduni na badala yake kuanza kuutengeneza.

Hicho ndicho kilichoufanya uzoefu huu kuwa wa kipekee. Kwa usiku mmoja, ulizipa changamoto dhana zilizokuwepo kwa muda mrefu kuhusu kile ambacho hadhira ya Tanzania inapaswa kutarajia kutoka kwa matukio ya hapa nchini. Ulionyesha wazi kwamba soko hili liko tayari kwa mawazo makubwa, ubunifu wa kiwango kikubwa na utekelezaji unaoweza kushindana na viwango vya kimataifa.

Na pengine ndiyo sababu mjadala wake ulisambaa kwa haraka kote nchini. Si kwa sababu watu walikuja kutazama mpira wa miguu, bali kuona taswira ya kile ambacho uzoefu wa chapa nchini Tanzania unaweza kuwa pale ambapo ubunifu unapopewa nafasi yake stahiki.

Swali la msingi sasa ni hili:

Je, chapa nyingine ziko tayari kuwa jasiri vya kutosha kufuata njia hiyo?

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Asha-Rose Migiro, leo Ijumaa Juni 5,2026 amefanya mazungumzo na Mheshimiwa Marianne Young, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, katika Makao Makuu ya CCM, Dodoma. 

 Mazungumzo hayo yalihusu maeneo ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Uingereza, kwa kuzingatia vipaumbele vilivyobainishwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). 

 Viongozi hao walijadili fursa za kuendeleza ushirikiano kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika kuwawezesha vijana na wanawake kupitia elimu, ujuzi, ubunifu na uwekezaji. CCM inaendelea kuthamini ushirikiano wa kimataifa unaochangia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wa Tanzania.










 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Shahada ya Uzamivu ya Heshima (Honoris Causa) aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi- (RUDN University) nchini Urusi, maarufu kama Patrice Lumumba University ni heshima kubwa kwake binafsi na kwa taifa la Tanzania kwa ujumla.

Akihutubia baada ya kutunukiwa shahada hiyo Rais Samia amesema katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni muhimu kwa nchi kuwekeza katika wataalamu waliobobea ambao wanaelewa kuwa ujuzi wao ni chachu ya maendeleo endelevu ya taifa.

Ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu, utafiti na teknolojia ili kuhakikisha vijana wanapata maarifa yatakayowezesha kushindana katika soko la ajira la kimataifa na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Rais Samia ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima na Chuo Kikuu cha RUDN, kwa kutambua mchango wake katika uongozi bora, diplomasia na maendeleo ya jamii.

Shahada hiyo imetolewa wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais Samia nchini Urusi, ambapo amekuwa akifanya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.

Na Beda Msimbe, TBN – Moscow, Urusi

Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi yake itaendelea kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano kwa Tanzania ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Rais Putin alitoa kauli hiyo jijini Moscow baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya kiserikali ya kihistoria.

Amesema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayotekelezwa Tanzania na kuridhishwa na hatua kubwa za maendeleo zinazopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu maendeleo ya Tanzania na tunafurahishwa na mageuzi yanayofanyika katika sekta mbalimbali za uchumi na ustawi wa jamii. Tunaamini ushirikiano wetu utaendelea kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa nchi zetu,” alisema Putin.

Aliongeza kuwa mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa na tija kubwa na yamefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya biashara, uwekezaji, elimu, teknolojia, nishati na maendeleo ya rasilimali watu.

Putin amesema Urusi itatumia pia Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaotarajiwa kufanyika nchini humo kutangaza na kuhamasisha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazoweza kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kwa sasa Urusi ina miradi takribani 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imechangia kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 3,000.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema ziara yake nchini Urusi ni ya kihistoria kwa Tanzania kutokana na ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Tanzania kufanya ziara ya kiserikali nchini humo baada ya zaidi ya nusu karne.

“Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Hivyo, kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu,” alisema Rais Samia.

Rais Samia pia alimshukuru Rais Putin na Serikali ya Urusi kwa mwaliko pamoja na mapokezi na ukarimu aliopatiwa tangu kuwasili kwake nchini humo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alikumbusha mchango wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kujenga taifa, huku akimpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.

Ziara hiyo ya Rais Samia nchini Urusi ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Tanzania katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, jambo ambalo linaipa uzito mkubwa wa kidiplomasia katika historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili.

Viongozi hao walieleza kuwa mazungumzo yao yamelenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki uliodumu kwa miongo mingi pamoja na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa yanayoendelea duniani.

Ziara ya Rais Samia inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za uwekezaji, biashara, elimu, sayansi na teknolojia, huku ikichochea fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.



Na Mwandishi Maalum

MOSCOW, URUSI – Kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana (Tomb of the Unknown Soldier) jijini Moscow kimeelezwa kuwa ni hatua yenye uzito mkubwa wa kidiplomasia inayobeba ujumbe wa amani, heshima kwa historia na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Rais Samia aliweka shada hilo katika mnara wa kumbukumbu uliopo karibu na Kremlin kama sehemu ya ratiba ya ziara yake ya kitaifa nchini Urusi, hatua iliyotafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kimataifa kuwa ishara ya kuthamini mchango wa mashujaa waliopigania uhuru na usalama wa mataifa yao.

Katika diplomasia ya kisasa, viongozi wa mataifa wanaposhiriki shughuli za kuenzi mashujaa wa kitaifa wa nchi mwenyeji huwa wanatoa ujumbe wa kuheshimu historia ya taifa husika, kuthamini sadaka za waliopoteza maisha kwa ajili ya amani na kuimarisha urafiki kati ya mataifa.




Kwa kushiriki hafla hiyo ya heshima katika Kaburi la Askari Asiyejulikana jijini Moscow, Rais Samia ameonesha kuwa Tanzania inaungana na jumuiya ya kimataifa katika kutambua mchango wa mashujaa waliolinda uhuru wa mataifa yao kwa gharama ya maisha yao.

Hatua hiyo pia inaendana na historia ya Tanzania ambayo tangu kupata uhuru wake mwaka 1961 imeendelea kujijengea sifa ya kuwa miongoni mwa mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele kuunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika, kulinda amani na kusisitiza matumizi ya mazungumzo katika kutatua migogoro.

Kaburi la Askari Asiyejulikana ni moja ya maeneo yenye hadhi kubwa ya kitaifa nchini Urusi. Mnara huo ulijengwa kuwakumbuka askari waliopoteza maisha wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia bila kutambulika majina yao.



Katika eneo hilo kuna kauli maarufu inayosema, “Jina lako halijulikani, lakini ushujaa wako hautakufa,” ambayo imeendelea kuwa alama ya heshima kwa mashujaa wote waliotoa maisha yao kwa ajili ya mataifa yao.

Wachambuzi wa diplomasia wanaeleza kuwa uwepo wa Rais Samia katika eneo hilo unaonesha kiwango cha heshima ambacho Tanzania inaipa historia ya Urusi pamoja na mchango wake katika matukio muhimu ya dunia.

Aidha, hatua hiyo imeonekana kuongeza uzito wa ziara ya Rais Samia nchini humo kwa kuonesha kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi haujajikita tu katika nyanja za uchumi na biashara, bali pia katika kuthamini historia, urafiki na maadili ya pamoja yanayounganisha mataifa hayo mawili.

Katika kipindi ambacho dunia inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za usalama na migogoro, ujumbe wa Rais Samia katika tukio hilo umeonekana kukumbusha umuhimu wa kujifunza kutokana na madhara ya vita na kuendelea kuwekeza katika amani, maridhiano na ushirikiano wa kimataifa.

Kwa mtazamo mpana, tukio hilo limeendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya taifa linalothamini historia, kuenzi mashujaa na kujenga mahusiano ya kirafiki na mataifa mengine kwa lengo la kuimarisha maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wake.

Hivyo, kitendo cha Rais Samia kuweka shada la maua katika Kaburi la Askari Asiyejulikana jijini Moscow hakipaswi kuonekana kama tukio la kawaida la kiitifaki, bali kama sehemu ya diplomasia ya kisasa inayolenga kuimarisha hadhi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa huku ikiendeleza misingi ya amani, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa.