Articles by "HABARI ZA BIASHARA"
Showing posts with label HABARI ZA BIASHARA. Show all posts
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko (wa tatu kutoka kulia), akiwa katika uzinduzi Rasmi wa tawi la benki ya Exim Tanzania wilayani Kahama mkoani Shinyanga. Kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank, Bw. Jaffari Matundu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na benki ya Exim katika tukio lililofanyika mnamo tarehe 25 Februari 2025 mjini Kahama.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa tatu kutoka kushoto), ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akikata utepe wakati hafla ya uzinduzi Rasmi wa tawi la benki ya Exim wilayani Kahama mkoani Shinyanga Wa pili kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank, Bw. Jaffari Matundu na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na benki ya Exim katika tukio hilolilofanyika mnamo tarehe 25 Februari 2025 mjini Kahama.

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga.

25 Februari 2025, Shinyanga: Benki ya Exim imedhihirisha dhamira yake ya kujenga ujumuishi wa kifedha na kupanua huduma zake kwa kuzindua rasmi tawi jipya katika Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga. Tawi hili jipya linalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wafanyabiashara, watu binafsi, na taasisi katika wilaya hiyo. Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa Mheshimiwa Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Bw. Jaffari Matundu, alieleza umuhimu wa upanuzi huu kwa ukuaji wa sekta ya kifedha: "Kahama ni moja ya vituo muhimu vya uchumi nchini, ikiwa na sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya taifa. Mji huu unajulikana sana kwa mchango wake katika sekta ya madini, hususan uzalishaji wa dhahabu, ambao umeifanya Kahama kuwa muhimu katika uchumi wa taifa.”

Jaffari aliongeza kuwa, “Kwa kuanzisha tawi hili, tunalenga kuhudumia mahitaji mbalimbali ya kifedha ya sekta hizi—iwe ni kwa ufadhili wa biashara, huduma za kibenki za kidijitali, au bidhaa za kifedha zinazolenga kukuza maendeleo ya kiuchumi.”
Tawi la Kahama litatoa huduma kamili za kibenki, ikiwemo akaunti za biashara na binafsi, huduma za hazina (treasury services), na mifumo ya kidijitali ya kibenki. Wateja watanufaika na huduma za Exim Bank zinazolenga kutoa suluhisho bora, la kisasa, na lenye ushindani kwa kuzingatia mahitaji ya soko yanayobadilika kila wakati.

Mheshimiwa Doto Biteko, alisifu juhudi za benki ya Exim za kupanua huduma zake, akisisitiza mchango wa taasisi za kifedha katika maendeleo ya Uchumi wa watu na taifa kiujumla:

“Serikali imekuwa ikihimiza taasisi zetu kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati. Kwa kipekee kabisa niwapongeze sana Exim bank kwa kutuwakilisha vyema katika nchi za Comoros, Uganda, Djibouti, pamoja na Ethiopia.”

“Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia Watanzania wengi zaidi, hasa wale walioko nje ya mifumo rasmi ya kifedha. Kwa niaba ya Serikali, naomba nitumie fursa hii kuipongeza Exim Bank kwa hatua hii kubwa na kwa jitihada zenu za kuleta huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi,” alisema Mhe. Biteko.
Tawi hili jipya linaonesha azma ya benki ya Exim ya kutoa suluhisho rahisi na jumuishi za kifedha huku ikiongeza uwepo wake katika maeneo muhimu kote Tanzania. Kwa kujikita katika ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wateja, benki ya Exim inaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya kifedha nchini.

Kadri benki ya Exim inavyoendelea kupanua huduma zake Kahama, benki hii inaendelea kushikilia dhamira yake ya kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kwa huduma za kifedha zinazopatikana kwa urahisi, za kuaminika, na za kisasa.

Upanuzi huu ni sehemu ya mkakati mpana wa benki wa kuchochea maendeleo ya uchumi, kuimarisha biashara za ndani, na kuongeza uelewa wa masuala ya kifedha katika jamii. Kwa mtazamo unaoweka mteja mbele na dira ya mafanikio ya muda mrefu, benki ya Exim iko tayari kubadilisha huduma za kifedha na kuleta maendeleo endelevu nchini Tanzania.
21 Februari 2025, Zanzibar – Benki ya Exim imeingia mkataba wa miaka mitatu na Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI) kwa lengo la kukuza na kuinua sekta ya utalii Zanzibar. Mkataba huo ulisainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Fedha kutoka benki ya Exim, Shani Kinswaga pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Ally, ukishuhudiwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrick Soraga.
Hafla ya msimu wa 35 wa mbio za Kili Marathon imefanyika leo katika viwanja vya ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo benki ya CRDB imeendeleza udhamini wake wa mbio za Kilomita 5 zinazojulikana kama CRDB Bank 5km Fun Run. Kimsingi, huu ni mwaka wa pili mfululizo tangu benki hiyo ianze kufanya udhamini huo jambo ambalo limezifanya mbio hizo kuendelea kuwa na msisimko mkubwa na wa kipekee.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mbio hizo, Mkuu wa kitengo cha Masoko CRDB Bank Bi. Joseline Kamuhanda amesisitiza kuwa benki ya CRDB inafanya hivyo, kwasababu inatambua na kuthamini umuhimu wa michezo kwa afya na kipato kwa wananchi wakiwemo wateja wao ambao wanawajali sana.
Washiriki wakifurahia.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mh. Mudrick Soraga (kulia), akimsikiliza Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shani Kinswaga, wakati wa kongamano la Z-Summit 2025 lililofanyika katika Chuo Kikuu cha SUZA, Zanzibar. Kongamano hilo la kila mwaka, lililofanyika kuanzia Februari 19-20, liliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ili kujadili changamoto na suluhisho za kuendeleza Zanzibar kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Zanzibar, Tanzania – Benki ya Exim Tanzania imeimarisha dhamira yake ya kukuza na kuendeleza sekta ya utalii Zanzibar kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta hiyo, wakiwemo Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ili kuwezesha waendeshaji wa shughuli za utalii kufanya malipo kama ada za kuingia kwenye hifadhi kwa haraka, kwa usalama na kwa urahisi.

Mkutano wa Z-Summit 2025, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha SUZA, Tunguu, uliwakutanisha wadau wa serikali, wafanyabiashara, na wadau wa sekta ya utalii na ukarimu ili kujadili suluhisho bunifu za kuboresha nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani.  
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, alisisitiza safari ya benki hiyo na Z-Summit tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa huu ni mwaka wa tatu mfululizo wa udhamini wao katika mkutano huo.  

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la kushirikiana, kubadilishana maarifa na kujadili mikakati ya kuimarisha zaidi nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani. Uungwaji mkono wa Benki ya Exim unaonesha imani yetu thabiti katika sekta ya utalii kama kiini cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii,” alisema Kinswaga.  

Kinswaga alielezea juhudi za benki hiyo katika kutumia teknolojia kutoa suluhisho rahisi za kifedha zinazokidhi mahitaji ya biashara za utalii. Kwa kuongezeka kwa mahitaji ya miamala ya kidigitali, Benki ya Exim imeanzisha huduma bunifu za kibenki, zikiwemo kutumia simu, kadi, na mifumo ya malipo mtandaoni, ili kuhakikisha ufanisi, usalama, na urahisi kwa wafanyabiashara na watalii.  
Akizungumzia ushirikiano wao na TANAPA, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Benki ya Rejareja wa Benki ya Exim, alisema, “Katika Benki ya Exim, tunatambua kuwa ufanisi, usalama, na urahisi ni muhimu katika sekta ya utalii. Ndiyo maana tumeshirikiana na wadau kama TANAPA na NCAA kuwezesha malipo yasiyo ya fedha taslimu kwa huduma mbalimbali, ikiwemo ada za kuingia kwenye hifadhi. Akaunti ya Waendeshaji wa shughuli za Utalii inajumuisha Kadi ya Exim TANAPA, iliyoundwa mahsusi kurahisisha miamala katika maeneo yote ya hifadhi nchini Tanzania.”  

Katika kuthibitisha dhamira yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, Benki ya Exim ilitangaza mpango wake wa kuendelea kupanua huduma zake Zanzibar. Ikiwa tayari na matawi mawili yanayofanya kazi, benki hiyo ina mpango wa kufungua matawi katika maeneo mengine ya kimkakati. Hii inaonesha azma ya Benki ya Exim ya kusogeza huduma za kibenki karibu na biashara, ikiwawezesha kupata suluhisho za kifedha zinazosaidia maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa biashara, na ufanisi wa uendeshaji.  

Kadri mazingira ya utalii yanavyoendelea kubadilika, Benki ya Exim inasalia kuwa mshirika wa kuaminika wa kifedha kwa biashara zinazotaka kupanuka, kuboresha huduma zao, au kuwekeza katika fursa mpya. Suluhisho zake maalum za kifedha zimeundwa kusaidia kupata rasilimali zinazohitajika ili kustawi katika soko lenye ushindani.  

Kupitia ushirikiano imara, matumizi ya teknolojia za kidigitali, na upanuzi wa huduma zake, Benki ya Exim haitoi tu msaada kwa sekta ya utalii bali pia inachangia katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kwa ujumla. Ushiriki wa Benki ya Exim katika mkutano wa Z-Summit 2025 ni uthibitisho wa dhamira yake isiyotetereka ya kusaidia ukuaji endelevu wa sekta ya utalii Zanzibar. 

Kwa kushirikiana na wawekezaji, wafanyabiashara, na mamlaka za serikali, benki hiyo inaunda mustakabali ambapo utalii utaendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi, kuongeza ajira, na kuifanya Zanzibar kuendelea kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka kote ulimwenguni.  
Katika kuendeleza hamasa ya matumizi ya kadi kwa wateja wake na Watanzania kwa ujumla, Benki ya CRDB imepanga kumzawadia mteja atakayekuwa na matumizi makubwa ya kazi zake za TemboCard Visa gari jipya aina ya Ford Ranger.

Sambamba na gari hilo jipya ambalo halijawahi kuendeshwa (kilomita sifuri), Benki ya CRDB pia imezindua kadi za mkopo za TemboCard credit card ili kuwawezesha wateja wake kukamilisha miamala yao hata katika kipindi ambacho hawana fedha za kutosha kwenye akaunti zao.
Akizungumzia kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kadi inayoitwa TemboCard ni Shwaa, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema itadumu mpaka Juni ili kuwapa wateja wengi fursa ya kujishindia zawadi tofauti ikiwamo kubwa ya gari jipya.

Raballa amesema kampeni hiyo itatoa jumla ya washindi 30 wakiwamo 24 watakaopata fursa ya kutembelea Mbuga ya Serengeti, watano wataofanya ziara barani Ulaya na mmoja atakayeondoka na Ford Ranger jipya ili kumrahisishia shughuli za usafiri kukamilisha mizunguko yake popote alipo nchini.
“Azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma shindani zinazokidhi mahitaji halisi ya wateja wetu. Tunaamini huduma bora na za kisasa ni muhimu kwa maendeleo ya wateja wetu na Taifa kwa ujumla. Tukishirikiana na wabia wetu Visa International, tumejielekeza katika kurahisisha malipo popote pale duniani,” amesema Raballa akisisitiza kwamba:“Kwa kuzingatia ubora wa huduma, uharaka wa malipo hasa teknolojia ya kugusisha kadi, kampeni yetu imepewa jina la ‘TemboCard ni Shwaaa.’”

Kampeni hii inawahusu wateja wote waliopo na wale wapya watakaojiunga na Benki ya CRDB wakitumia kadi yoyote ile iwe ni TemboCard Gold na Platinum kwa ajili ya wateja wetu wa hadhi ya juu, TemboCard Infinite ambayo ni ya kifahari na ya muundo wa chuma (metal card), au kadi ya wateja wadogo yaani TemboCard Classic Debit.
Akieleza kuhusu ushirikiano wa Benki ya CRDB na kampuni ya Visa International, amesema ni wa kimkakati ukilenga kufungua fursa kwa Watanzania hasa wanaofanya biashara za kimataifa, wanaotalii katika mataifa mengine na wanaoenda kusoma au wanaofanya safari za kiofisi nje ya nchi.

“Ripoti ya karibuni ya Visa International inaonyesha duniani kote sasa hivi kuna watoa huduma za malipo zaidi ya milioni 130 ambao wanatumia mfumo wa malipo wa kadi za Visa. Hivyo Mtanzania mwenye kadi ya TemboCard Visa anao wigo mpana wa kupata huduma mahali popote atakapokuwepo duniani,” amesema Raballa.

Ili kuongeza wigo wa matumizi ya kadi, Benki ya CRDB imezindua kadi za TemboCard Credit ambazo ni maalumu kwa ajili ya kupata mkopo utakaoingizwa kwenye kadi hizo kulingana na sifa za mteja husika pamoja na kutambulisha kadi zake za TemboCard Prepaid ambayo inamruhusu mteja kukamilisha miamala yake bila kuihusisha akaunti yake ya benki.

“Kwa mteja binafsi atakayepata kadi ya TemboCard Credit, ataweza kupata mkopo wa kuanzia shilingi 500,000 na kampuni inafika shilingi milioni 500. Iwapo deni hilo litalipwa ndani ya siku 50 basi hakutokuwa na riba kabisa,” amesema Raballa.

Kuhusu kadi za TemboCard Prepaid, amesema zinafanya kazi kama chombo cha malipo kinachojitegemea zikimuwezesha mteja kufanya malipo bila kuigusa akaunti yake ya akiba.

“Kadi hii imetolewa mahususi ili isaidie kupanga bajeti kwani inakuruhusu kutumia tu kiasi ulichoweka. Kipengele hiki ni muhimu sana kwa watu wanaosimamia matumizi ya kila mwezi au wazazi wanaowapa watoto wao hela ya matumizi shuleni au mahali pengine popote. Wateja wataweza kuweka pesa kwenye kadi hata kupitia mitandao ya simu,” amefafanua Raballa.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) wakati wa Kikao cha Baraza hilo linalofanyika tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni (kushoto). Kulia ni Katibu wa Baraza Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Ebeneza Mollel,wakati wa Kikao cha Baraza hilo cha kujadili Mpango na Bajeti hilo linalofanyika tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wakati wa Kikao cha Baraza hilo linalofanyika tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro. Kushoto Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni.
---------
*Ataka Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kuwa na matokeo chanya

*Aipongeza PURA kuwashirikisha Watumishi kujadili mipango ya Bajeti ya Taasisi

MOROGORO

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) kuendelea kuvutia uwekezaji katika vitalu vilivyo wazi vya mafuta na gesi asilia ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini.

Mhe. Kapenga amesema hayo leo wilayani Morogoro, Mkoa wa Morogoro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa PURA kinacholenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemoMpango na Bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

” Mkifanikiwa kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, nchi itaongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kuogeza futi za ujazo wa gesi inayopatikana nchini, Pia mkiendelea kuvutia uwekezaji kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu itakayozinduliwa mwezi machi mwaka huu, pamoja na faida zilizopo, mtakuwa mmeendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuifungua Tanzania kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi.”Amesema Kapinga.

Amesema Wizara ya Nishati inatambua umuhimu wa tukio la Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo imeshafanyika kuelekea uzinduzi wa tukio hilo ambalo amesema kuwa ni muhimu katika

kuvutia uwekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

“ Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukizungumzia ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 pekee ni wakati sasa wa kufanya zaidi na zaidi ili tuweze kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa.” Amesisitiza Mhe.Kapinga

Katika kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi, ameupongeza uongozi wa PURA kwa kuendelea kuwashirikisha watumishi wake katika kujadili, kupanga na kupitisha mipango na Bajeti ya Taasisi kwenye Baraza la Wafanyakazi ikiwa ni utekelezaji pia wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.

Amesema kufanyika kwa vikao hivyo ni ishara tosha ya utawala bora mahala pa kazi kwa kuwa watumishi wanapata fursa ya kuchangia mawazo yao kuhusu hali ya uendeshaji wa Taasisi hivyo kuendelea kuwa ni sehemu muhimu ya Taasisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) Mhandisi. Charles Sangweni, amesema duru ya tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na

gesi asilia nchini inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Machi, 2025 Jijini Dares salaam wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EAPCE’25).

Amesema PURA inaendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini na Kuhakikisha watanzania wazawa wanashirikishwa katika miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli nchini.
Dar es Salaam. Tarehe 18 Februari 2025: Ikiwa katika maadhimisho ya miaka 30 tokea kuanzishwa kwake, Benki ya CRDB imetangaza mafanikio makubwa ya hatifungani ya miundombinu ya ‘Samia Infrastructure Bond,’ ambayo imevuka lengo kwa asilimia 115, ikikusanya Shilingi bilioni 323 - zaidi ya mara mbili ya lengo lake la awali la kukusanya Shilingi bilioni 150.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio makubwa ya mauzo ya Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond iliyokusanya TZS bilioni 323 ambazo ni zaidi ya mara mbili ya lengo la awali la kupata TZS bilioni 150.
Mafanikio haya yaliyopatikana ndani ya mwezi mmoja na nusu wa mauzo hayo yanaonyesha imani kubwa waliyonayo wawekezaji kwa Benki ya CRDB hali inayoiweka mahali pazuri zaidi kuimarisha nafasi yake kama benki kinara katika sekta ya fedha nchini.

Hatifungani hii iliyotajwa kwa heshima ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaonyesha dhamira ya Benki ya CRDB kuchangia kukuza uchumi wa taifa na kuimarisha kipato cha mwananchi mmojammoja.

Kupitia fedha zilizokusanywa baada ya mauzo ya hatifungani hii, wananchi watanufaika kutokana na ukamilishaji kwa wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara za mijini na vijijini.
Mheshimiwa Mchengerwa amesifu mafanikio haya akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji nchini.

“Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond ni mfano halisi wa namna ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi unavyoweza kuleta manufaa kwa taifa letu. Kiasi hiki cha TZS 323 bilioni kilichokusanywa kinatoa mwanga wenye matumaini kwa maendeleo ya miundombinu hasa ya barabara huko mbeleni.
Nawapongeza sana Benki ya CRDB kwa ubunifu huu mliokuja nao katika kuisaidia serikali kukamilisha mipango yake ya kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Waziri Mchengerwa.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu tangu tarehe 29 Novemba 2024 uzinduzi wa mauzo hayo ulipofanyika mpaka Januari 17 dirisha hilo lilipofungwa, kampuni na taasisi 327 zimejitokeza kuwekeza zaidi ya TZS 118.99 bilioni pamoja na watu binafsi 6,896 waliowekeza jumla ya TZS 204.1 bilioni. Asilimia 94 ya kiasi chot ekilichopatikana kimekusanywa kupitia Programu ya SimBanking.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema mafanikio yaliyoyapata yanadhihirisha ukubwa nauwezo wa uwekezaji walionao wananchi pamoja na kampuni zilizopo katika soko letu sambamba na utayari wao kuwekeza hasa wanapojiridhisha na uhakika wa mradi na Benki ya CRDB inajisikia fahari kubwa kuaminiwa na Watanzania kwa ujumla wao.

Kazi kubwa iliyofanywa na menejimenti ya Benki ya CRDB ikishirikiana na Wizara ya TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) amesema imekuwa na mafanikio makubwa ambayo matunda yake yatawanufaisha Watanzania wengi. “Tumepata wawekezaji wengi binafsi kwa sababu walimudu kiwango cha chini cha shilingi 500,000 tu.
Fedha zote tulizozikusanya kwenye mauzo ya hatifungani ya Samia Infrastructure Bond zitatumika kuwawezesha makandarasi wa wanaotekeleza na watakaoshinda zabuni zitakazotangazwa na TARURA. Tunaamini upatikanaji wa fedha hizi utasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha miradi kwa wakati,” amesema Nsekela.

Wawekezaji hawa, Nsekela amesema wataendelea kushirikiana nao kwa kipindi chote cha miaka mitano ya uhai wa hatifungani hii kama walivyowaahidi wakati wa mauzo yaliyofanyika nchi nzima ikiwamo kulipa riba ya asilimia 12 kwa mwaka itakayotolewa kwa awamu nne. “Malipo ya riba yatakuwa yanafanyika kila tarehe 10 Februari, 10 Mei, 10 Agosti, na 10 Novemba. Kwa mwaka huu, wataanza kupokea malipo ya faida tarehe 10 Mei,” amesema Nsekela.

Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond ni awamu ya pili ya Mpango wa Muda wa Kati wa Miaka Mitano kwa ajili ya kukusanya Shilingi za Kitanzania sawa na Dola za Marekani Milioni 300 ambao uliridhiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Fedha na Mitaji (CMSA) mwaka 2023.
Kupitia mpango huo, mwaka 2023 Benki ya CRDB ilikuwa ya kwanza nchini kuzindua hatifungani ya kijani iliyopewa jina la ‘Kijani Bond’, ambayo ilikuwa hatifungani ya kwanza kwa ukubwa kusini mwa Jangwa la Sahara. “Kijani Bond ilikuwa ni awamu ya kwanza ya mauzo ya Mpango wa Muda wa Kati wa Miaka Mitano na Samia Infrastructure Bond ni awamu ya pili ya mpango huo.

Kama tulivyovuka lengo katika mauzo ya Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond, hali ilikuwa hivyo pia kwenye Kijani Bond iliyotuwezesha kukusanya shilingi bilioni 171.82 kutoka shilingi bilioni 40 zilizokusudiwa sawa na ufanisi wa asilimia 429.6,” amefafanua Nsekela.
Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema ushirikiano huu ulioanzishwa kati ya Benki ya CRDB na TARURA utakuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa miradi ya barabara nchini. “Tunayo miradi mingi inayotekelezwa katika maeneo tofauti nchini na changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya malipo ya makandarasi. Naamini wengi sasa watapata fedha zao kwa wakati ili kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa,” amesema Mhandisi Seff.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama alisema kuwa kuorodheshwa kwa Samia Infrastructure Bond kumetongeza thamani ya uwekezaji katika hatifungani za kampuni na taasisi kwa asilimia 38.9, na kufikia TZS trilioni 1.16 kutoka TZS bilioni 837.31.

"Samia Infrastructure Bond ni kielelezo wazi cha nguvu za masoko yetu ya mitaji, na kuufanya Soko la Hisa la Dar es Salaam kuwa mchezaji muhimu katika kuwezesha uwekezaji katika miradi ya miundombinu ya kitaifa ya Tanzania," aliongeza Bwana Mkama.

Baada ya kutangaza matokeo ya mauzo, hatifungani hiyo iliorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kuwaruhusu wawekezaji waliochelewa kupata nafasi ya kushiriki kuijenga nchi yao huku wakipata faida ya asilimia 12 itakayotolewa kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela amesema kila siku idadi ya Watanzania wanaoshiriki sokoni hapo inazidi kuongezeka jambo linalotia matumaini kwamba litazidi kukua hivyo kuwa na manufaa makubwa hapo siku za mbeleni. “Mafanikio zinazopata makampuni yaiyoorodheshwa sokoni ni mfanikio ya soko zima.

Sisi wasimamizi wa soko tunapata faraja kuona mambo yanaenda vizuri kila kunapokuwa na bidhaa mfano wa Hatifungani hii ya Samia Infrastructure Bond ya Benki ya CRDB,” amesema Nalitolela.




Obinna Anyalebechi (Mkurugenzi Mtendaji wa SBL) akizungumza katika warsha ya siku moja iliyokutanisha wadau wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutoka mashirika mbalimbali kuzungumzia mikakati ya kupambana na biashara haramu ya pombe nchini Tanzania. Kuanzia kulia ni Khadija Ngasongwa (Mkurugenzi wa bidhaa bandia kutoka FCC), Mwenyekiti wa zamani wa Shirikisho la wenye Viwanda (CTI) ambae pia ni Mwenyekiti wa bodi ya SBL, Paul Makanza na Lazaro Masasalaga (Mkurugenzi Udhibiti Ubora kutoka TBS). Warsha hii ilifanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa zamani wa Shirikisho la wenye Viwanda (CTI) na mwenyekiti wa bodi ya SBL, Paul Makanza akizungumza katika warsha ya siku moja iliyokutanisha wadau wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutoka mashirika mbalimbali kuzungumzia mikakati ya kupambana na biashara haramu ya pombe nchini Tanzania. Kuanzia kulia ni Khadija Ngasongwa (Mkurugenzi wa bidhaa bandia kutoka FCC), Obinna Anyalebechi (Mkurugenzi Mtendaji wa SBL), na Lazaro Masasalaga (Mkurugenzi Udhibiti Ubora kutoka TBS). Warsha hii ilifanyika leo jijini Dar es Salaam.
Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) liliendesha warsha na wadau mbalimbali kujadili changamoto kubwa la unywaji wa pombe haramu na hatarishi. 

Warsha hiyo iliwaunganisha wadau muhimu wa sekta ya viwanda, watunga sera, na mamlaka za udhibiti kama Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na wadau wengine muhimu katika sekta ya pombe.

CTI ilisisitiza hatari kubwa za kiafya zinazotokana na pombe zisizodhibitiwa, ikiwa ni pamoja na viwango vya juu vya sumu, madhara ya muda mrefu kama ugonjwa wa ini, upofu, na hata vifo. Aidha, pombe haramu inachangia matatizo ya kijamii kama uhalifu, unyanyasaji wa majumbani, na kushuka kwa ufanisi kazini, hali inayoongeza mzigo kwa mifumo ya afya na ustawi wa jamii.
Mwenyekiti wa zamani wa CTI, Paul Makanza, alisema, “Mapambano dhidi ya pombe haramu si tu suala la udhibiti—ni juhudi za kulinda maisha ya Watanzania, kulinda mapato ya serikali, na kuendeleza mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki. Pombe haramu inahatarisha afya ya umma, inachochea matatizo ya kijamii, na inadhoofisha sekta rasmi ambayo inatoa maelfu ya ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi. Tunahitaji kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera huku tukiendelea kuongeza uelewa ili kuhakikisha sekta ya pombe inayowajibika na endelevu ambayo inachangia maendeleo ya Tanzania kwa njia chanya.”

Akiunga mkono maoni ya Mwenyekiti wa zamani, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, aliongeza: “Sisi, kama wazalishaji wa pombe, tuko tayari kushirikiana katika jitihada hizi. Tunaamini kuwa mafanikio ya kweli katika sekta hii hayapimwi tu kwa utendaji wa kifedha, bali pia kwa uwezo wetu wa kuchangia maendeleo endelevu ya jamii yetu. Matumizi mabaya ya pombe ni hatari kwa kila mtu—sekta, afya ya umma, na jamii—na kushughulikia changamoto hii kunahitaji ushirikiano.”
Mbali na athari za kiafya, CTI ilielezea wasiwasi wake juu ya athari za kiuchumi zinazotokana na pombe haramu. Utafiti uliofanywa na Ernest & Young mnamo Novemba 2018 ulibaini kuwa serikali ya Tanzania inapoteza takriban shilingi trilioni 1.2 kila mwaka kutokana na biashara ya pombe haramu. Mauzo yasiyodhibitiwa yanadhoofisha biashara halali na kusababisha hasara kubwa ya mapato ya kodi, hali inayopunguza uwezo wa serikali kufadhili huduma muhimu kama afya na elimu. Zaidi ya hayo, sekta rasmi ya pombe—ambayo inatoa maelfu ya ajira—inakabiliwa na ushindani usio wa haki kutoka kwa waendeshaji wasiosajiliwa ambao wanakwepa kanuni za usalama na viwango vya ubora.

Ili kulinda afya ya umma na uthabiti wa uchumi, CTI ilitoa wito wa udhibiti mkali wa sekta ya pombe, ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha imani ya wawekezaji, kuhamasisha unywaji wa pombe kwa uwajibikaji, na kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa hatari.

CTI na washirika wake wanatoa wito kwa serikali na wadau kuongeza juhudi za kupambana na pombe haramu kupitia utekelezaji madhubuti wa sheria, kuongeza uelewa wa umma, na kuboresha utekelezaji wa sera. Ushirikiano kati ya viongozi wa sekta, mamlaka za udhibiti, na vyombo vya usalama ni muhimu ili kuhakikisha sekta salama na yenye uwajibikaji katika unywaji pombe inayosaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.