Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC,Khadija Ngasongwa akizungumza na wadau wa Wazalishaji wa Ndani wa Saruji wakati walipokutana kujadiliana kuhusiana hali ya Soko ya bidhaa hiyo jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC,Khadija Ngasongwa akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiana na ofisi hiyo kufanya majadiliano na Wazalishaji wa Ndani wa Saruji jijini Dar es Salaam.
FCC katika kikao cha Wazalishaji wa Ndani wa Saruji jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya matukio katika picha ya katika kikao cha majadiliano.
Na Mwandishi Wetu
Tume ya Ushindani (FCC) imekutana na wadau wa uzalishaji wa ndani wa saruji kwa lengo la kujadili hali ya uzalishaji, mwenendo wa bei na namna ya kulinda ushindani wa soko pamoja na maslahi ya walaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema kikao hicho kinalenga kujenga uelewa wa pamoja kati ya tume na wazalishaji ili kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki bila kumuathiri mlaji.
Alisema baadhi ya wazalishaji waliwasilisha taarifa ya kusudio la kupandisha bei ya saruji, hatua iliyolazimu FCC kufanya tathmini ya kina kuhusu gharama za uzalishaji, ikiwemo uendeshaji na malighafi, kabla ya kuchukua msimamo wowote.
“Majadiliano haya yatatusaidia kupata mwanga wa namna bora ya kulinda afya ya soko la saruji na kuhakikisha mlaji anapata bidhaa kwa bei stahiki na upatikanaji wa uhakika,” alisema Ngasongwa.
Aliongeza kuwa sekta ya saruji ni mhimili muhimu katika uchumi wa Tanzania, hususan katika kipindi hiki ambacho nchi inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu na viwanda kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya mwaka 2050.
Ngasongwa alibainisha kuwa FCC itaendelea kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara katika kutoa miongozo itakayosaidia kuimarisha ushindani wa soko huku Serikali ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei ili kulinda maslahi ya walaji.





.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments: