Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya Exim Bank Tanzania imehitimisha rasmi kampeni yake ya ‘Chanja Kijanja, Dili Ndio Hili’ kwa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi iliyofanyika katika tawi lake jipya la Ubungo jijini Dar es Salaam. Kampeni hiyo iliyodumu kwa miezi miwili ililenga kuhamasisha matumizi ya kadi za benki katika malipo ya kila siku na kuendeleza utamaduni wa miamala ya kidijitali isiyotumia fedha taslimu.
Katika hafla hiyo, mshindi wa zawadi kuu Asif K. Dhalla alijishindia shilingi milioni 15, huku mshindi wa pili Aliakber Zoeb Hakimjee akipokea shilingi milioni 10 na John Estomih Kweka akishinda shilingi milioni 5 kama mshindi wa tatu. Aidha, zaidi ya washindi 60 wa kila wiki na mwezi walijinyakulia zawadi mbalimbali, ambapo washindi wa kila wiki walipokea shilingi 100,000 kila mmoja na washindi wa kila mwezi shilingi 200,000 kila mmoja kama motisha ya kuendelea kutumia kadi.
Kupitia kampeni hiyo, wateja pia walinufaika na ofa maalum, punguzo la bei na zawadi walipotumia kadi zao katika maeneo washirika wakiwemo Shoppers Plaza, Village Supermarket, Karambezi Café pamoja na CIP Lounge Julius Nyerere International Airport.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu, alisema kampeni hiyo imelenga kuonesha kuthamini wateja na kuongeza uelewa wa faida za malipo ya kidijitali, akisisitiza kuwa matumizi ya kadi ni salama, rahisi na yanaweza kumpatia mteja manufaa ya ziada. Naye Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala na Mabadiliko ya Kidijitali, Silas Matoi, alisema mwitikio wa wateja unaonesha mabadiliko chanya kuelekea uchumi usiotegemea fedha taslimu.
Makabidhiano hayo yalifanyika chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania ili kuhakikisha mchakato wote unafuata kanuni na taratibu zilizowekwa. Mwakilishi wa bodi hiyo, Neema Tatock, alithibitisha kuwa droo zote ziliendeshwa kwa uwazi na haki, huku mshindi wa zawadi kuu akieleza ushindi wake umempa motisha zaidi ya kuendelea kutumia kadi katika miamala yake ya kila siku.






Toa Maoni Yako:
0 comments: