Dar es Salaam, Februari 10, 2025 — Kampuni ya Samsung Electronics East Africa imezindua rasmi maduka mawili mapya ya chapa (Brand Stores) katika maeneo ya Kunduchi na Ubungo, ikiwa ni mkakati wa kupanua uwekezaji wake nchini Tanzania na kuimarisha ushindani katika soko la teknolojia na rejareja.

Maduka hayo yamebuniwa kuunganisha bidhaa za simu za mkononi na vifaa vya kielektroniki vya nyumbani chini ya paa moja, yakilenga kuwapatia wateja uzoefu wa moja kwa moja wa mfumo wa bidhaa unaofanya kazi kwa pamoja. Kupitia mpangilio huo, wateja wanapata fursa ya kuona, kujaribu na kuelewa namna simu janja, kompyuta kibao, runinga, vifaa vya kuvaa pamoja na vifaa vya nyumbani vinavyoweza kuunganishwa ili kurahisisha shughuli za kila siku.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Kitengo cha Simu za Mkononi wa Samsung Electronics East Africa (Tanzania), Mgope Kiwanga, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kampuni katika soko la Tanzania. Alisema maduka hayo yanatoa nafasi kwa wateja kujionea kwa vitendo namna teknolojia ya Samsung inavyoweza kuleta tija katika mawasiliano, burudani na matumizi ya nyumbani.

Tofauti na maduka ya kawaida ya rejareja, maduka hayo mapya ni makubwa na yameundwa mahsusi kuonesha wigo mpana wa bidhaa za kampuni hiyo. Mbali na mauzo, yanatoa maelezo ya kitaalamu, maonesho ya matumizi ya bidhaa (product demonstrations), upatikanaji wa vifaa halisi (original accessories) pamoja na huduma baada ya mauzo kupitia wafanyakazi waliofunzwa na kuthibitishwa na Samsung.

Kwa upande wake, Meneja wa Biashara wa Samsung Tanzania, Daesong Ra, alisema uwekezaji huo unaonesha imani ya kampuni katika ukuaji wa soko la Tanzania na mchango wake katika mageuzi ya kidijitali. Alibainisha kuwa upanuzi huo unachochea ajira, unakuza ujuzi wa wafanyakazi wa ndani na kuongeza upatikanaji wa teknolojia bora kwa watumiaji.

Mbali na kuboresha uzoefu wa wateja, maduka hayo yanatarajiwa kuchangia ukuaji wa uchumi wa ndani kupitia ajira na mafunzo ya kitaalamu kwa Watanzania, huku yakiiweka Samsung katika nafasi imara zaidi ya ushindani katika sekta ya teknolojia inayokua kwa kasi nchini.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: