Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KLABU ya Simba SC imemtakia kila la heri mshambuliaji wake, Kibu Denis Prosper, baada ya kukamilisha uhamisho wake kwenda klabu ya Al Nasr SC ya Libya kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu wenye thamani ya dola za Kimarekani 250,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Simba usiku huu, Kibu anaondoka Msimbazi baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa misimu minne na nusu tangu alipojiunga mwaka 2021 akitokea Geita Gold.
“Baada ya kuwa sehemu ya kikosi chetu kwa misimu minne na nusu, Kibu Denis ‘Mkandaji’ ameuzwa na sasa anakwenda kuanza maisha mapya nje ya Simba SC,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Katika kipindi chake akiwa Simba, Kibu amekuwa mshambuliaji tegemeo akichangia mabao na pasi za mabao katika mashindano ya ndani na kimataifa, huku akisaidia timu kutwaa mataji mbalimbali ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Uhamisho wake kwenda Al Nasr unamkutanisha tena na mshambuliaji wa Kimataifa wa Uganda, Steven Dese Mukwala, ambaye tayari alishasajiliwa na klabu hiyo ya Libya mapema.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mabadiliko ya kikosi cha Simba kuelekea nusu ya pili ya msimu, huku mashabiki wakimtakia mafanikio mema Kibu katika changamoto yake mpya nje ya Tanzania.



Toa Maoni Yako:
0 comments: