Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiondoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, tarehe 12 Februari, 2026, kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi mbalimbali katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Februari, 2026 kabla ya kuondoka nchini kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

Na Mwandishi Wetu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo Februari 12, 2026 kuelekea Addis Ababa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Februari 14 hadi 15, 2026.

Kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu, Rais Dkt. Samia anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) utakaofanyika Februari 13, 2026 chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. William Samoei Ruto. Mkutano huo unalenga kujadili masuala ya mabadiliko ya tabianchi, uchumi na maendeleo endelevu barani Afrika.

Mkutano Mkuu wa AU kwa mwaka 2026 utafunguliwa rasmi Februari 14, 2026 ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda 2063.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha hatua za pamoja za nchi wanachama katika kulinda rasilimali maji, kuboresha afya ya jamii na kuharakisha maendeleo endelevu barani Afrika.

Mbali na kushiriki vikao rasmi, Rais Dkt. Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Mhe. Russell Mmiso Dlamini; Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assoumani; Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed; pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah. Aidha, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed Ali, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi.

Katika mkutano huo, Tanzania inatarajiwa kuthibitishwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ikiendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda na kimataifa. Aidha, Rais Dkt. Samia amependekezwa kuteuliwa kuwa Kiongozi wa AU katika masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi unaotarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Kupitia ushiriki wake katika mkutano huo, Tanzania inalenga kuendelea kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano na maendeleo endelevu, huku ikiimarisha mchango wake katika ajenda za bara na kulinda maslahi ya taifa katika jukwaa la kimataifa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: