Na Mwandishi Wetu.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Idadi ya Watu (UNFPA) kwa nchi za Comoro, Mauritius, Seychelles na Madagascar, Bi. Josiane Yaguibou, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika masuala ya sensa.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadili maandalizi ya Sensa ya Watu itakayofanyika nchini Comoro mwaka 2027, ambapo UNFPA ni miongoni mwa waratibu wakuu wa zoezi hilo. Walizungumzia namna Tanzania inaweza kushiriki kama mdau kwa kutoa uzoefu na utaalamu wake katika uendeshaji wa sensa.

Balozi Yakubu alimueleza Bi. Yaguibou kuwa Tanzania ilifanikiwa kwa kiwango kikubwa kuendesha Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa kutumia vifaa vya kisasa vya kidijitali pamoja na kushirikisha waangalizi wa kimataifa, jambo lililoongeza uwazi na ufanisi wa zoezi hilo.
Kwa upande wake, Bi. Yaguibou aliahidi kuendeleza mawasiliano na Ubalozi wa Tanzania ili kupata uzoefu na mbinu bora zilizotumika katika sensa ya mwaka 2022, kwa lengo la kuhakikisha Sensa ya Comoro 2027 inakuwa ya mafanikio.

Mazungumzo hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania, Comoro na UNFPA katika kuimarisha mifumo ya takwimu na upangaji wa maendeleo kwa kuzingatia taarifa sahihi za idadi ya watu.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: