Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amezindua rasmi Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la pili, uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia amesema Mkakati wa KKK ni miongoni mwa ahadi zake za siku 100 alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akisisitiza kuwa msingi wa elimu bora hujengwa katika hatua za awali za ujifunzaji.
Rais amesema mkakati huo unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wizara na taasisi nyingine zinazohusika na maendeleo ya awali ya mtoto, ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa pamoja na wenye tija.

Amesema mtoto anayekosa stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu mapema hukumbwa na changamoto kubwa katika masomo ya juu zaidi, hali inayomfanya kubaki nyuma kielimu. Aidha, Rais amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wote wanapata umahiri wa KKK kabla ya kufika darasa la tatu ili waweze kujifunza kwa ufanisi katika ngazi zinazofuata.
Katika maelekezo yake, Rais Dkt. Samia ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa mkakati huo yanafanyika kwa kutumia mbinu shirikishi, bunifu na za kisasa, ikiwemo matumizi ya zana na nyenzo za kufundishia zinazowavutia watoto.

Rais pia amesisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya ukaguzi wa elimu, tathmini za mapema na endelevu za ujifunzaji pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa mkakati huo ili kubaini changamoto kwa wakati na kuchukua hatua stahiki.

Amesema Mkakati wa KKK utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027 hadi 2030/2031, sambamba na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, kuajiri walimu wapya pamoja na kuimarisha rasilimali watu. Rais amebainisha kuwa Serikali imeajiri walimu 7,000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati, ambapo walimu 6,044 tayari wameanza kazi.

Aidha, Rais Dkt. Samia ametambua mchango wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuunga mkono utekelezaji wa mkakati huo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema utekelezaji wa Mkakati wa KKK unaenda sambamba na maboresho ya miundombinu ya elimu, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Lengo Namba Nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG4) linalohusu elimu bora.

Profesa Mkenda ameongeza kuwa mkakati huo unaweka mkazo katika uwajibikaji, uwazi na kuzingatia matokeo halisi ya ujifunzaji wa watoto badala ya taarifa pekee, ili kuhakikisha watoto wote wanapata stadi stahiki za kusoma, kuandika na kuhesabu mapema.

Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unalenga kubadilisha kwa kiasi kikubwa matokeo ya ujifunzaji wa awali nchini, sambamba na mchango wa Tanzania katika utekelezaji wa Ajenda ya Afrika 2063.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: