Articles by "ELIMU."
Showing posts with label ELIMU.. Show all posts
Dar es Salaam. Tarehe 27 Aprili 2024: Katika kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu nchini, Benki ya CRDB imeasaini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Wawekezaji katika Elimu Tanzania (TAPIE) utakaowawezesha wanachama wake kupata mikopo nafuu ya kuboresha miundombinu na kuwezesha uendeshaji wakati wote.


Mkataba huo umesainiwa tarehe 27 Aprili 2024 kwenye mkutano mkuu wa 5 wa mwaka wa TAPEI uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt Doto Biteko na kuhudhuriwa na wadau wa elimu nchini.
Akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Benki inatambua changamoto wanazokutana nazo wamiliki binafsi wa shule hivyo imechukua hatua za kusaidia kuzitatua ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi kusoma na kujifunza.


“Ni ukweli usiopingika kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote lile duniani kwani husaidia kujenga maarifa, ujuzi na kuongeza ufanisi hivyo kuwa kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi. Kwa kuyatambua haya yote, Benki ya CRDB imeiweka sekta ya elimu katika moja ya vipaumbele vyake vya uwezeshaji. Tunafanya hivi ikiwa ni sehemu za kusaidia jitihada za Serikali pamoja na wadau wa sekta hii kutoa elimu bora itikayozalisha rasilimali watu bora katika nyanja mbalimbali,” amesema Raballa.


Kwa kuzitambua changamoto zilizopo ukiwamo ukweli kwamba uendeshaji wa shule unategemea mapato yatokanayo na ada ambayo mara nyingi hukusanywa shule zinapofunguliwa hivyo kuwa na uhaba pindi zinapofungwa, Benki ya CRDB imewaletea mkopo wa uendeshaji ili kukidhi mahitaji yanayopaswa kulipiwa wakati mapato mengine yakisubiriwa indi muhula mpya utakapoanza.
Raballa pia amesema shule nyingi zipo kwenye maeneo ambayo hayajarasmishwa jambo linalowanyima wamiliki uwezo wa kukopa kutokana na kutokidhi vigezo vya dhamana hivyo Benki ya CRDB imewaletea suluhisho kwa kuwaruhusu kukopa fedha zitakazowezesha urasmishaji wa maeneo yao ili kupata hati ya wizara itakayowaruhusu kukopa ili kuimarisha biashara zao.


“Tunawaruhusu wamiliki wa shule kukopa mpaka shilingi milioni 10 kwa ajili ya kurasmisha maeneo ya shule. Fedha hizi ni kwa ajili ya kutafuta hati ya wizara hivyo kuyatambulisha maeneo yao ya kisheria. Vilevile, tunayo mikopo kwa dhamana zisizo rasmi yaani maeneo ya shule ambayo hayana hati. Benki yetu inamruhusu mmiliki kuja kukopa mpaka shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule. Tunaamini kwa utaratibu huu rahisi na rafiki, tutasaidia kuwezesha uwekezaji wa shule katika sekta binafsi,” amesema Raballa.
Wakati wamiliki wakipewa mkopo wa uwekezaji wanaoweza kuurejesha mpaka kwa miaka 7, Raballa amesema walimu na wafanyakazi wa shule binafsi nao wanaweza kupata mkopo kwa ajili ya kufanikisha mambo yao binafsi. Mikopo ya wafanyakazi hawa, amesema inajumuisha ‘salary advance’ ambao ni mahsusi kwa wale ambao mishahara yao inapitia Benki ya CRDB ambao wanaweza kupata mpaka asilimia 50 ya mshahara wao na wakalipa ndani ya siku 30 pamoja na mkopo wa binafsi unaofika mpaka shilingi milioni 100 zinazoweza kurejeshwa kwa mpaka miaka 8.


”Kwa miaka mitatu iliyopita, kiwango cha mikopo ya eimu tuliyoitoa kwa kundi hili imekuwa ikiongezeka. Mwaka 2021 Benki yetu ya CRDB ilikopesha zaidi ya shilingi bilioni 78.66 ambazo zilipanda mpaka shilingi bilioni 86 mwaka 2022 na mwaka jana zikawa shilingi bilioni 97.17. Nitumie fursa hii kuweka wazi kwamba mikopo hii tunayotoa kwa wamiliki wa shule binafsi hasa wanachama wa TAPIE, inaweza kurejeshwa mpaka kwa miaka 7,” amesisitiza Raballa.
Kwa upande wake, rais wa TAPIE, Mahmoud Mringo amesema hadi sasa kuna zaidi ya shule 6,362 zinazojumisha za awali 2,364, za msingi 2,270 na sekondari 1,728 zinazomilikiwa na watu binafsi, mashirika ya dini na yasiyo ya dini, majeshi, na jumuiya za wazazi ambazo zimedahili takriban wanafunzi 1,020,772 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita ambazo zimeajiri takribani walimu 59,445 na wataalamumwengine zaidi ya 100,000 wenye taaluma na ujuzi mbalimbali kama wahasibu, madereva, wasimamizi na walezi wa wanafunzi, walinzi na wapishi. Ajira hizi zimesaidia kuinua hali za kimaisha kwa watu husika na kupanua wigo wa kodi mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa taifa.


“Ukitaka kujenga darasa, maabara au kuboresha miundombinu mingine ya shule, ni lazima uende kukopa benki lakini tatizo ni riba kubwa. Kujenga shule ndogo tu kwa sasa unahitaji walau shilingi bilioni 2 lakini kuwa na shule yenye kila kitu basi unahitaji shilingi bilioni 10. Ukizikopa hizi kutoka benki na ukalipa kwa riba iliyopo, itakuchukua miaka 20 ya kumaliza deni ambalo ni lazima lilipwe na mwanafunzi.


Bado kuna kodi na tozo 16 ambazo shule inatakiwa kulipa. Haya mambo yote yanaifanya elimu yetu kuwa ghali na kusoma shule zisizo za serikali inaonekana ni anasa,” amesema Mringo akiiomba serikali iangalie namna ya kupunguza riba ya mikopo tozo pamoja na kodi.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko amepongeza juhudi za sekta binafsi kuchangia kuboresha elimu nchini kwamba zinaifanya jamii iwe na mchango zaidi katika kukuza uchumi. "Niwapongeze kwa ushirikiano na mkataba wa makubaliano mnayosaini leo na Benki ya CRDB. Ili kufanikisha mambo, ushirikiano na wadau wengine ni muhimu sana. Hivi mnavyofanya, ndio namna nzuri ya kukabiliana na changamoto zetu," amesema Dkt Biteko.






Benki ya CRDB kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii, Aprili 24 - 25, 2024 ilikabidhi madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Kikilo na madarasa mengine mawili katika Shule ya Msingi Isabe zote za wilayani Kondoa, mkoa wa Dodoma yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki hiyo.

Hafla ya kukabidhi madarasa hayo, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa pamoja na Maafisa Elimu Sekondari na Msingi.

Katika hafla zote mbili Dkt. Khamis Mkanachi ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukubali maombi ya ujenzi wa madarasa katika Wilaya ya Kondoa, ambayo yapo katika vijiji vya Kikilo na Bukulu. Huku akitoa rai kwa wanafunzi kusoma kwa bidii kwani mazingira ya shule yanaendelea kuboreshwa.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa, Mashauri Vicent aliyekabidhiwa madarasa hayo ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya elimu pia kuahidi kuwa watahakikisha madarasa hayo yanakuwa ni sehemu ya kuchagiza ongezeko la wanufaika ambayo ni watoto kwenye jamii ya Kondoa.

Kwa upande wa Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay aliyeongozana na Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji kwa Jamii pamoja na Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, amesema kuwa Benki ya CRDB imeweka sera ya uwekezaji kwa jamii inayolenga kuchangia maendeleo mbalimbali katika jamii hasa katika swala la Elimu, Mazingira, Afya, Vijana na Wanawake. Aidha, ametoa rai kwa wazazi wa shule hizo kuendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa shule katika kuboresha miundombinu ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay wakiwa pamoja na viongozi wengine pamoja na Wanafunzi katika moja ya madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 katika Shule ya Msingi Isabe, iliyopo katika kijiji cha Bukuru, Wilayani Kondoa, katika hafla  iliyofanyika Aprili 25, 202.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi (wanne kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay (katikati) akiwa pamoja na viongozi wengine wa Benki ya CRDB pamoja na wa Halmashauri ya Kondoa wakiwa katika picha ya paamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikilo, muda mfupi baada ya kukaidhi madarasa mawili katika shule hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dkt. Khamis Mkanachi akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt, Ally Laay akizungumza wakati wa hafla kukaidhi madarasa mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya CRDB yenye thamani ya shilingi Milioni 40 kwa uongozi wa Halmashauri ya Kondoa.












Waziri Mavunde na CEO wa Barrick wakikata utepe kuzindua chuo, katikati ni mkuu wa wilaya ya Kahama, Mboni Mhita
---
Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, ameipongeza Kampuni ya Dhahabu ya Barrick ambayo inaendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals, kwa kufanya uwekezaji unaoendelea kuchangia kukuza uchumi na kufanikisha miradi ya kijamii ambayo inaendelea koboresha maisha ya wananchi.

Mh. Mavunde, ametoa pongezi hizo leo Jumatatu Machi 18,2024 wilayani Kahama wakati wa uzinduzi wa Chuo cha mafunzo cha Barrick chenye hadhi ya kimataifa kijulikanacho kama Barrick Academy, katika mgodi wa zamani wa Buzwagi wilayani Kahama ambao umefungwa ambacho kitakuwa kinatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Barrick wa nchini na nje ya nchi kupata utaalamu wa kuendesha shughuli zao kwa weledi.

Waziri Mavunde amesema ulimwengu wa sasa ni wa sayansi na teknolojia hivyo chuo hicho kimeanzishwa katika wakati muafaka ambapo sekta ya madini nchini inakua kwa kasi sana na kuhitaji wataalamu wa kutosha.

Ametoa wito kwa uongozi wa Barrick kuangalia uwezekano wa kuanzisha kozi za kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo nao wapate maarifa ya kuendesha kazi zao kwa maarifa.

“Barrick mmeanza kwa kufungua chuo katika eneo hili la Ukanda Maalum wa Kiuchumi la Buzwagi la Serikali, nina imani wawekezaji wengi watajitokeza kujenga viwanda ili kuziba athari za kiuchumi zilizotokana na kufungwa kwa mgodi wa Buzwagi”,amesisitiza.

Kwa upande Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, amesema Barrick itaendelea kufanya kazi na Serikali kuhakikisha ubia wake unanufaisha pande zote na kuchangia kukuza uchimi wa nchi,

Bristow amesema Barrick, inalipa umuhimu kubwa suala la elimu na itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha watanzania wanapata elimu na ndio maana imeamua kufungua chuo kikubwa cha kimataifa cha Barrick Academy nchini.

“Tutaendelea kuhakikisha kuwa ubia wetu na Serikali ya Tanzania unakuwa wa kuigwa katika sehemu mbalimbali duniani kwa kufanikisha kuleta mafanikio na maendeleo chanya kwa wananchi”, alisisitiza Dkt. Bristow.

Bristow amesema Chuo cha Barrick kimebuniwa na Barrick ili kutoa programu maalumu za mafunzo zinazoandaliwa kulingana na mahitaji zinazolenga kuandaa mameneja wa mstari wa mbele wa Barrick ili wakue kama watu binafsi na viongozi katika nyanja zao huku kozi hizo zikiwapa ujuzi wa kusimamia timu zao kwa ufanisi zaidi na kuboresha utendaji.

“Chuo cha Barrick kitakuwa kikitoa mafunzo kwa mafomeni, wasimamizi na warakibu zaidi ya 2,000 kutoka Kannda ya Afrika Mashariki na Kati katika kipindi cha miezi 24 ijayo. Tukiwa na maono ya mbele, tunajitayarisha pia kuwajumuisha Wakandarasi wetu na kupanua mtaala ili kufikia taaluma nyingi zaidi ikiwa ni pamoja na kutoa kozi za uongozi katika masuala ya fedha, ujuzi wa ngazi ya juu wa Kompyuta na katika masuala ya usalama”,ameongeza Bristow.

Ameeleza kuwa, ufunguzi wa chuo cha Barrick unafuatia ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Buzwagi Kahama mnamo mwezi Januari 2024 lililofungua fursa kwa ajili ya huduma za ndege zilizopangwa ambalo linaweza kuhudumia zaidi ya abiria 200 kwa wakati mmoja ambapo jengo hilo linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi katika Manispaa ya Kahama.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Barrick katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Sebastiaan Bock amesema uwanja wa ndege na Chuo katika mgodi uliofungwa wa Buzwagi ni sehemu ya mpango wa Barrick wa kuibadili Buzwagi kuwa Ukanda Maalum wa kiuchumi.

“Upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2021 ulionesha kuwa uundwaji wa Kanda maalumu ya kiuchumi ulikuwa na uwezo wa kuchukua nafasi ya mgodi wa Buzwagi kama kichocheo cha uchumi wa eneo hili na unaweza kutengeneza ajira zipatazo 3,000 kila mwaka, kuzalisha zaidi ya dola 150,000 kila mwaka kutokana na tozo za huduma kwa Manispaa ya Kahama na kutoa takribani dola milioni 4.5 kwa mwaka kama kodi ya ajira”,amesema Sebastiaan.

Amesema Serikali ya Tanzania iliidhinisha ubadilishaji wa mgodi wa Buzwagi kuwa ukanda maalum wa kiuchumi (SEZ) kupitia tangazo la Serikali ilitolewa mwezi Februari 2024 na tayari Wawekezaji wameanza mchakato wa kuanzisha viwanda katika eneo hilo.

“Namna tunavyofunga migodi yetu ni muhimu kwetu kama ambavyo tunaijenga na kuiendesha. Mgodi wetu wa Buzwagi ulikuwa kitovu cha uchumi katika ukanda huu kwa takribani miaka 15 kabla ya kutoa dhahabu yake ya mwisho mwaka 2021. Hata hivyo, mtazamo wetu huo siyo mwisho wa hadithi hii kwa Buzwagi tunapoibadilisha kuwa mali mbadala yenye tija ambayo itahudumia jamii kwa miongo kadhaa ijayo”,amesema Bock.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) Charles Itembe, ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kubuni wazo la kuanzisha Chuo cha Barrick huku akiwaomba wawekezaji mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika eneo hilo ili kuongeza thamani ya madini na vitu vingine kwenye eneo la Buzwagi ambako kutakuwa na viwanda zaidi ya 100 na mpaka sasa kuna wawekezaji wanane.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita amesema kuanzishwa kwa Chuo cha Barrick ni matokeo mazuri ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick ili kukuza uwekezaji nchini.
Mbunge wa Jimbo la Kaham Mjini Mhe. Jumanne Kishimba amewapongeza Barrick kuwa wawekezaji wa kwanza katika Mgodi uliofungwa wa Barrick huku akiomba chuo hicho pia kitumike kutoa mafunzo ya madini kwa wachimbaji wadogo na jinsi ya kufanya biashara ya madini huku Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama Thomas Myonga akisema uwekezaji unaofanyika katika eneo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kukuza uwekezaji nchini.

Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Barrick katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Sebastiaan Bock
Meneja wa Barrick nchini, Melkiory Ngido
Waziri wa Madini Antony Mavunde na CEO wa Barrick wakibadilishana mawazo wakati wa hafla hiyo
Sehemu ya wageni waalikwa
Wanafunzi wa awamu ya kwanza katiika chuo katika picha ya pamoja na Waziri Mavunde na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow na viongozi wengine wa mkoa wa Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ndg. Kisena Mabuba akifungua kikao kazi cha Maafisa Elimu na watendaji wa Kata kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri uliopo Kata ya Iselamagazi February 06, 2024
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia kwa ukaribu wakati wa kikao cha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia kwa ukaribu wakati wa kikao cha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Maafisa Elimu na Watendaji wa 
Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ndg. Kisena Mabuba wakati wa kikao cha Mkurugenzi huyo na viongozi hao.
**************Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Ndg. Kisena Mabuba amewaagiza Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata kuhakikisha kuwa watoto wote wanakwenda shule. Maagizo hayo yametolewa leo Februari 06, 2024 wakati wa kikao kazi baina yake na Maafisa Elimu na Watendaji wa Kata kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri uliopo Kata ya Iselamagazi.

Akizungumza katika kikao hicho Mabuba amesema halizishwi na mwenendo wa kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali katika shule mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

"Mkafanye kazi kwa ushirikiano kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shule walizopangiwa na wale wenye umri wa kuandikishwa elimu ya awali na msingi wanaenda shule,"Amesisitiza Ndg Mabuba.

Aidha, amepiga marufuku kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi hususani muda wa masomo. Mkurugenzi huyo amesema viongozi hao wa kata wana wajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya matendo ya kikatili ili kupunguza na kuondoa kabisa changamoto ya ndoa za utotoni na mimba katika umri mdogo.

Maafisa Elimu na Watendaji wa kata hao wameaswa pia kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa weledi na kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma akieleza kuwa uwazi na uwajibikaji ndio nguzo kuu ya utumishi.

Akizungumzia mapato na matumizi, Mkurugenzi Mabuba amewaagiza viongozi hao kuhakikisha kuwa wanafanya vikao na mikutano ya kisheria kwa kila robo ya mwaka. Mikutano hiyo itumike kama majukwaa ya viongozi na wananchi kujadili taarifa za maendeleo ya kata na vijiji pamoja na kuwasomea taarifa za mapato ,miradi ya maendeleo na matumizi ya vijiji na kata.

"Mnayo dhamana ya kusimamia ukusanyaji mapato katika kata zenu. Ni kinyume cha Sheria kukusanya fedha za Umma bila mashine ya 'POS' na kukaa na fedha za umma bila kuziweka Benki. Alisisitiza Ndg. Mabuba.