Na Mwandishi Wetu, Manyara.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amezindua rasmi namba ya bure ya huduma kwa mteja 0800787722 itakayotumika kupokea kero, changamoto na malalamiko ya wananchi wa mkoa huo, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa namba hiyo, Mhe. Sendiga amesema mfumo huo utarahisisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao, kwani utamwezesha mwananchi kutoa taarifa kwa urahisi bila gharama yoyote.
“Mwananchi atapiga namba hii bure kabisa bila makato yoyote na kutoa taarifa sahihi bila kudanganya. Lengo ni kupata changamoto kwa wakati na kuzifanyia kazi kwa haraka,” amesema RC Sendiga.
Ameeleza kuwa kupitia namba hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itaweza kufuatilia kwa karibu changamoto za wananchi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi unaostahili kwa wakati, huku taarifa zote zikikusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kutengeneza ripoti za kila mwezi.
Aidha, amezitaka ofisi zote zilizo chini ya uongozi wake kuhakikisha zinashughulikia kwa haraka malalamiko yote yatakayopokelewa kupitia namba hiyo na kutoa mrejesho kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
Wananchi wa Mkoa wa Manyara wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo wakisema itawapa fursa ya kufikisha moja kwa moja changamoto zao kwa viongozi, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za kijamii na kiutawala katika maeneo yao.




Toa Maoni Yako:
0 comments: