Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (PDPC) imetangaza kuanza rasmi kwa ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria kwa taasisi za umma na binafsi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi za wananchi, hatua inayolenga kuhakikisha utekelezaji kamili wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 na kanuni zake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Januari 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema ukaguzi huo unaanza mara moja baada ya kuisha kwa kipindi cha hiari ambacho taasisi zilipaswa kukamilisha usajili wao, kwa mujibu wa tangazo la Tume lililoweka ukomo wa Aprili 8, 2026.
Dkt. Mkilia amesema ukaguzi huo utalenga kubaini taasisi zinazokusanya, kuhifadhi, kuchakata au kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi bila kuzingatia matakwa ya sheria, na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka sheria.
“PDPC tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu, taasisi au kampuni yoyote itakayokiuka sheria hii, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini, kifungo, kulipa fidia kwa waathirika au adhabu hizo kwa pamoja,” amesema.
Ameongeza kuwa hakuna taasisi itakayovumiliwa kutumia taarifa binafsi za mtu bila ridhaa yake au kinyume na taratibu za kisheria, bila kujali ukubwa au hadhi ya taasisi husika.
“Taasisi yoyote itakayokiuka misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi itawajibishwa ipasavyo. Sheria hii inalenga kulinda haki za wananchi na kujenga mazingira salama ya matumizi ya taarifa katika zama za TEHAMA,” ameongeza.
PDPC imeeleza kuwa pamoja na mafanikio makubwa ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), changamoto ya ukiukwaji wa faragha imekuwa ikiongezeka, huku taarifa binafsi zikiendelea kukusanywa, kuchakatwa na hata kusafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine bila kufuata taratibu zinazotakiwa kisheria.
Tume hiyo imewataka wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa PDPC pale wanapohisi haki zao za faragha zimekiukwa, huku taasisi zote zikihimizwa kuhakikisha mifumo yao inazingatia kikamilifu sheria na kanuni za ulinzi wa taarifa binafsi.



Toa Maoni Yako:
0 comments: