Na Munir Shemweta, WANMM

Dodoma.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeingilia kati mgogoro wa matumizi ya ardhi unaomhusisha mwekezaji Rashid Kwanzibwa katika eneo la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita, kufuatia madai ya kubomoa baadhi ya majengo yaliyopo kwenye maeneo ya serikali na kuanzisha miradi bila kufuata taratibu.

Akizungumza leo Januari 26, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imeanza kushughulikia suala hilo kwa kina ili kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa mujibu wa sheria na taratibu za matumizi bora ya ardhi.

Dkt. Akwilapo amewakumbusha wamiliki wote wa ardhi nchini kuzingatia matumizi yaliyobainishwa katika hati miliki zao, akisisitiza kuwa mmiliki yeyote anayepanga kubadili matumizi ya eneo lake anatakiwa kuomba na kupata kibali cha mabadiliko ya matumizi kama sheria inavyoelekeza.

“Hatua hii itasaidia kuhakikisha maeneo yanaendelezwa kwa mpango, kupunguza migongano ya matumizi ya ardhi, kulinda mazingira na kuhakikisha miji yetu inakuwa nadhifu,” amesema Waziri.

Ameongeza kuwa uendelezaji wowote wa ardhi unapaswa kuzingatia sheria za mipango miji na vijiji, ikiwa ni pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka husika kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi wowote.

Kwa mujibu wa Waziri, timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi na TAMISEMI tayari ipo kazini kuchunguza kwa kina sakata hilo, na baada ya uchunguzi kukamilika, Serikali itatoa taarifa rasmi ya pamoja kueleza hatua zilizofikiwa.

Hatua ya Wizara kuingilia kati imekuja baada ya kusambaa kwa picha na taarifa katika mitandao ya kijamii zikionesha Kamati ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikisitisha shughuli za ujenzi wa vibanda vya maduka katika eneo la viwanja vya CCM Katoro, kufuatia madai kuwa mwekezaji aliingia katika maeneo ya serikali ya kijiji yaliyopo Kitongoji cha Katoro Center.

Serikali imesisitiza itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya ardhi nchini ili kulinda maslahi ya umma, kudumisha amani na kuhimiza maendeleo endelevu katika maeneo yote.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: