Na Mwandishi Wetu, London – Uingereza

Mfuko wa kimataifa wa uwekezaji wa Sino American Global Fund (SinoAm LLC) umetangaza nia ya kuwekeza hadi Dola za Marekani bilioni 5 nchini Tanzania, hatua inayotarajiwa kuimarisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta za miundombinu, usafirishaji, nishati, teknolojia, huduma za kifedha na maendeleo ya viwanda.

Nia hiyo iliwasilishwa wakati wa mkutano rasmi kati ya uongozi wa SinoAm LLC na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, uliofanyika jijini London, Uingereza, pembezoni mwa ziara ya kikazi ya Waziri huyo nchini humo.

Akizungumza kwa niaba ya SinoAm LLC, Mwenyekiti wa mfuko huo, Bw. Najib Choufani, alisema kuwa SinoAm imejipanga kuwekeza kiasi hicho kwa awamu kupitia miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Alieleza kuwa baada ya kufanya tathmini ya kina ya mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania, mfuko huo umebaini fursa zenye tija kubwa ikiwemo ujenzi na uendeshaji wa barabara za kisasa za kulipia (toll expressways), miradi ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) pamoja na miundombinu ya usafirishaji na nishati itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ushindani wa Tanzania kikanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SinoAm LLC, Bw. Tarek Choufani, alisema mfuko huo una uzoefu mkubwa wa kimataifa katika usimamizi wa miradi mikubwa ya miundombinu na uko tayari kuleta nchini Tanzania si tu mitaji mikubwa bali pia utaalamu wa kiufundi, mifumo ya kisasa ya usimamizi na mbinu bora za kimataifa.

Akizungumza katika mkutano huo, Prof. Mkumbo aliipongeza SinoAm LLC kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini Tanzania, akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kufanya mageuzi ya sera, mifumo ya kisheria na kiutendaji ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aliongeza kuwa Tanzania ina utulivu wa kisiasa, sera rafiki za uwekezaji, na dira ya muda mrefu ya maendeleo, hali inayotoa uhakika na ulinzi kwa wawekezaji wa kimkakati.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: