“Rushwa inadhalilisha utu wa binadamu na inazorotesha utoaji wa huduma za jamii. Ni lazima tuchukue hatua za kuizuia kabla haijaleta madhara makubwa. Rushwa ni ajenda ya kitaifa,” alisisitiza Dkt. Nchemba.
Waziri Mkuu aliagiza taasisi zote za Serikali kubaini na kuziba mianya ya rushwa, hususan katika maeneo ya manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi na usimamizi wa mikataba, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya Serikali hupitia kwenye maeneo hayo, hivyo yanahitaji uangalizi wa karibu.
Aidha, aliwahimiza wananchi kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kulinda usiri na usalama wa watoa taarifa. Pia alisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi, wadau wa maendeleo, vijana na wanawake katika mapambano hayo.
Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya kisheria na kiutawala pale itakapobainika kuna vikwazo vinavyoathiri utendaji wa TAKUKURU, na kuwataka viongozi wa taasisi hiyo kutoa mapendekezo yao kwa uwazi. Pia alielekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya TAKUKURU na Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kujenga misingi imara ya uadilifu na uwajibikaji.
Akihusisha mapambano dhidi ya rushwa na maendeleo ya Taifa, Waziri Mkuu alisema jitihada hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030, ambazo zimeweka wazi kuwa utawala bora na kupambana na rushwa ni nguzo muhimu za ustawi wa wananchi.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Nchemba aliwataka viongozi wa TAKUKURU kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanakuwa chachu ya kuongeza juhudi zaidi, huku akirejea kaulimbiu ya mkutano:
“Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
Baada ya hotuba hiyo, Waziri Mkuu alitangaza rasmi kufunguliwa kwa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2025 wa Viongozi wa TAKUKURU.








Toa Maoni Yako:
0 comments: