London, Uingereza — Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), amewahakikishia wawekezaji wa Uingereza kuwa Tanzania ni nchi salama, yenye uthabiti wa kisiasa na inayoendelea kutekeleza mageuzi ya kina ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Prof. Mkumbo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza ulioandaliwa na taasisi ya kimataifa ya Clyde & Co, ikiwa ni sehemu ya ziara yake rasmi ya kikazi nchini humo.
Katika hotuba yake, Waziri alisema Tanzania inaanza safari ya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwa katika nafasi nzuri, kutokana na uthabiti wa uchumi, amani na utulivu wa kisiasa, pamoja na mageuzi yanayoendelea kufanyika ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alieleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika baada ya athari za janga la UVIKO-19, ambapo kasi ya ukuaji imepanda kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 hadi asilimia 5.9 mwaka 2025, huku ikitarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026. Aidha, aliongeza kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kimeendelea kubaki chini ya asilimia 5 kwa zaidi ya muongo mmoja, jambo linaloonesha uthabiti wa mazingira ya kiuchumi.

Akizungumzia mazingira ya uwekezaji, Prof. Mkumbo alisema Serikali inaendelea kuimarisha amani na usalama, kufanya maboresho ya sera za kodi na udhibiti, pamoja na kuongeza uwazi na utabiri wa sera ili kuwapa wawekezaji uhakika zaidi. Alifafanua kuwa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) kupitia kuunganisha taasisi mbili kuwa moja, kumeongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wawekezaji.
Waziri huyo aliainisha pia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini, akibainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 44 za ardhi yenye rutuba, rasilimali nyingi za madini na nishati, pamoja na nafasi ya kipekee ya kijiografia inayoiunganisha Afrika Mashariki, Kati na Kusini kupitia bandari, reli, barabara na anga. Alisisitiza kuwa Tanzania ina madini 22 ya kimkakati yanayohitajika katika mpito wa nishati duniani.
Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Uingereza, Prof. Mkumbo alisema ushirikiano wa nchi hizo mbili umeendelea kwa zaidi ya miongo sita, ambapo biashara ya pande mbili imefikia thamani ya pauni milioni 650, huku uwekezaji wa Uingereza unaokadiriwa kufikia pauni bilioni 4.89 ukizalisha zaidi ya ajira 131,000 nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Clyde & Co, Bw. Michael Clayton, aliipongeza Tanzania kwa juhudi zake za kufanya mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji, akisisitiza kuwa majukwaa ya majadiliano kama hayo ni muhimu katika kujenga imani na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya serikali na wawekezaji wa kimataifa.
Akihitimisha hotuba yake, Prof. Mkumbo aliwaalika wawekezaji wa Uingereza kuwa washirika wa karibu wa Tanzania katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050, akisisitiza kwa msisitizo:
“Tuko wazi kwa biashara. Tunafanya mageuzi. Tunakua. Na tuko tayari kushirikiana.”













Toa Maoni Yako:
0 comments: