Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Kamishna Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Ofisi ya Zanzibar, Mhe. Khatibu Mwinyi Mwinyichande, amewahimiza watumishi wa Tume hiyo kuendelea kuwatii viongozi wao, kuwa na nidhamu, pamoja na kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa weledi na uadilifu.

Mhe. Mwinyichande alitoa nasaha hizo wakati wa hafla fupi ya kuwaaga watumishi wa THBUB wa Ofisi za Zanzibar na Pemba, kufuatia kustaafu kwake rasmi katika utumishi wa umma ndani ya Tume hiyo.

Katika hotuba yake, aliwasisitiza watumishi hao kuendelea kujifunza mara kwa mara, kuongeza ujuzi wa kitaaluma na kuwa tayari kupokea ushauri na kukosolewa pale wanapokosea, hatua itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kulinda misingi ya haki na utawala bora.

“Watumishi wa umma mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii. Kubalini kukosolewa, endeleeni kujifunza na mtimize wajibu wenu kwa uadilifu,” alisema Mhe. Mwinyichande.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa THBUB wa ofisi za Zanzibar na Pemba, Naibu Katibu Mtendaji wa THBUB, Bw. Juma Msafiri Karibona, alimshukuru Mhe. Mwinyichande kwa mchango mkubwa alioutoa wakati wa utumishi wake ndani ya Tume hiyo.

Bw. Karibona alisema Kamishna huyo amekuwa mfano wa kuigwa kutokana na busara, hekima, uadilifu na ushirikiano aliouonesha kwa watumishi wote, na kuongeza kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa ndani ya taasisi hiyo.

Ikumbukwe kuwa jumla ya Makamishna sita wa THBUB walistaafu rasmi Januari 16, 2026, baada ya kuitumikia Tume hiyo kwa kipindi chao cha kisheria. Miongoni mwao ni:

● Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mst. Mhe. Mathew P. M. Mwaimu

● Makamu Mwenyekiti, Mhe. Muhammed Khamis Hamad

● Kamishna Amina Talib Ali

● Kamishna Nyanda Shuli

● Kamishna Thomas Masanja

● Kamishna Khatibu Mwinyi Mwinyichande

Kustaafu kwao kunatajwa kuwa ni sehemu ya mzunguko wa kawaida wa uongozi unaolenga kuipa Tume nafasi ya kuendelea kuimarika na kutekeleza majukumu yake ya kulinda haki za binadamu na kuimarisha utawala bora nchini

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: