Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la Kimani Mtaa wa Kinyamwezi, Kata ya Pugu, Ilala Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa ardhi Februari 13, 2026.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, akizungumza wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.
Ukaguzi wa eneo lenye mgogoro ukiendelea
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameleta nafuu kwa wakazi wa Pugu baada ya Serikali kuingilia kati mgogoro wa muda mrefu wa ardhi inayodaiwa kuvamiwa licha ya kutengwa kwa matumizi ya makaburi.
Mgogoro huo unahusu eneo la Kimani, Mtaa wa Kinyamwezi, Kata ya Pugu jijini Dar es Salaam, ambapo wakazi walimtuhumu Elizabeth Mwakapangala kwa madai ya kuuza eneo hilo na kufukua makaburi kinyume cha sheria.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 13, 2026, Mpogolo alisema ramani ya upimaji inaonesha wazi kuwa eneo hilo lilitengwa rasmi kwa ajili ya maziko kwa mujibu wa mipango miji ya Serikali.
Mpogolo alieleza kuwa kesi ya ardhi namba 202/2020 iliyofunguliwa na Mwakapangala, aliyekuwa msimamizi wa mirathi, ilihusisha Halmashauri ya Jiji, Tanzania Airports Authority na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mpogolo alieleza kuwa kesi ya ardhi namba 202/2020 iliyofunguliwa na Mwakapangala, aliyekuwa msimamizi wa mirathi, ilihusisha Halmashauri ya Jiji, Tanzania Airports Authority na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akisoma hukumu ya Mahakama iliyotolewa na A. M. Msafiri, alisema mlalamikaji alistahili kulipwa fidia lakini hakuwa na haki ya kuuza ardhi ya makaburi wala kuhamisha mabaki ya miili bila kufuata sheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, aliwataka wananchi kuwa watulivu huku Serikali ikiendelea kufuatilia suala hilo kwa mujibu wa sheria.
Wananchi walidai eneo hilo lilitengwa kwa maziko ya wakazi waliohamishwa kutoka Kipawa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Hata hivyo, Mwakapangala amekanusha tuhuma hizo akidai hajawahi kufukua makaburi na kusisitiza kuwa eneo hilo ni mali yake halali, akisema anazo nyaraka zote baada ya kushinda kesi mahakamani mwaka 2022.
Serikali imesema itaendelea kushughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria ili kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha haki inatendeka.













Toa Maoni Yako:
0 comments: