Dar es Salaam, Tanzania, 25 Novemba 2024 – MultiChoice Tanzania imetangaza ushirikiano na Vodacom Tanzania PLC, kampuni inayoongoza katika mawasiliano ya simu nchini, kwa ajili ya kuzindua Showmax – jukwaa maarufu la burudani kupitia video barani Afrika. Ushirikiano huu muhimu unaashiria zama mpya za burudani bora na rahisi kufikiwa Tanzania, huku ukiunga mkono matumizi ya kidijitali nchini na kuinua vipaji vya ndani.  

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Jacqueline Woiso, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, alisema, “hili ni tukio kubwa nchini kwetu ambapo makampuni makubwa mawili katika sekta za mawasiliano na burudani wameungana kwa maslahi ya wateja wetu. Ushirikiano huu unasisitiza dhamira yetu ya kutoa maudhui ya kimataifa ya kiwango cha juu huku tukitumia teknolojia ya kisasa ya Vodacom Tanzania.”

Woiso aliongeza, “Ushirikiano huu utawezesha wateja wa Vodacom kote Tanzania kupata maudhui bora ya vipindi vya TV, filamu, michezo, na makala kupitia Showmax, hivyo kufanya burudani ya kiwango cha juu iwe rahisi kufikiwa katika vifaa mbalimbali vya kidijitali. Showmax ina maktaba kubwa ya maudhui inayojumuisha uzalishaji wa ndani na nje ya Tanzania, pamoja na michezo ya Ligi Kuu ya Uingereza, ikienda sambamba na ladha mbalimbali za burudani. Ushirikiano huu ni mfano dhahiri wa jinsi ushirikiano unavyoweza kuleta thamani kubwa kwa wateja, kuweka maslahi yao mbele ya ushindani.”  

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Phillip Besiimire, alisema “Ushirikiano huu unaendana kikamilifu na dhamira yetu ya kusaidia Tanzania kuelekea zama za kidijitali huku tukiboresha maisha kupitia teknolojia. Kadri upatikanaji wa simu janja unavyoongezeka nchini, tumejikita katika kuboresha huduma zetu za kidijitali kwenye burudani, elimu, kilimo, afya, na usafiri. Leo, tunajivunia kuongeza Showmax katika orodha yetu ya burudani, tukiwawezesha wateja wetu kufurahia maudhui ya kiwango cha juu yanayowagusa moja kwa moja.”  
Uzinduzi wa Showmax pia unaangazia umuhimu wa kuunga mkono vipaji na uzalishaji wa maudhui ya ndani. Kupitia maudhui ya ndani yanayoonyeshwa kwenye jukwaa hili, lengo ni kuinua sauti za wasanii wa Kitanzania na kuhakikisha kazi zao zinafikia hadhira kubwa zaidi. Hatua hii si tu inaimarisha sekta ya burudani bali pia inachangia ukuaji wa uchumi wa ubunifu wa ndani. 
 
Ili kunufaika na ushirikiano huu, Vodacom na MultiChoice wanatoa vifurushi vya kipekee vya data vinavyowezesha wateja wa Vodacom kufurahia maudhui ya burudani kwa gharama nafuu. Watumiaji wanaweza kupakua programu ya Showmax, kununua kifurushi, na kufurahia ulimwengu wa burudani ya kuvutia.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: