
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya teknolojia ya Google imetangaza upanuzi mkubwa wa huduma zake za utafutaji kwa kutumia Akili Bandia (AI) kwa kuongeza lugha 13 za Afrika, ikiwemo Kiswahili na Kisomali, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa mamilioni ya watumiaji barani humo.
Kupitia taarifa iliyotolewa Machi 6, 2026, kampuni hiyo ilisema maboresho hayo yatawezesha watumiaji kuvinjari mtandao, kujifunza na kuunda maudhui kwa kutumia lugha zao za asili. Huduma hiyo mpya pia inaongeza uwezo wa kipengele cha muhtasari wa majibu ya AI (AI Overviews) ambacho kinatoa majibu mafupi yanayotengenezwa na AI pamoja na viungo vya taarifa zaidi kwa mtumiaji.
Aidha, mfumo wa AI Mode unawaruhusu watumiaji kuwasiliana na mfumo huo kwa kutumia maandishi, sauti au picha ili kupata majibu ya kina zaidi kulingana na lugha wanayopendelea. Maboresho hayo yameanza kutolewa kwa watumiaji katika nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Kenya, Nigeria, Ethiopia na Tanzania ambako matumizi ya utafutaji mtandaoni yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.
Mbali na Kiswahili na Kisomali, lugha nyingine zilizoingizwa katika mfumo huo ni pamoja na Afrikaans, Akan, Amharic, Hausa, Kinyarwanda, Afaan Oromoo, Sesotho, Setswana, Wolof, Yorùbá na isiZulu.
Google imesema hatua hiyo inalenga kuwasaidia wanafunzi, walimu na wajasiriamali kutumia teknolojia ya AI katika kutatua changamoto halisi katika jamii zao badala ya kusikia tu kuhusu teknolojia hiyo. Maboresho hayo pia yanajengwa juu ya utafiti wa mradi wa lugha za Kiafrika wa Google Waxal language project unaotumia ujifunzaji wa mashine na ushirikiano wa wataalamu wa lugha ili kuboresha uelewa wa AI katika lugha za Afrika.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, watumiaji wanaweza kutumia huduma hiyo kwa kufungua programu ya Google app kwenye simu za Android au iOS au kupitia kivinjari cha simu, kisha kuchagua kipengele cha AI Mode na kuuliza maswali kwa lugha wanayopendelea. Google imewahimiza watumiaji barani Afrika kujaribu huduma hiyo na kutoa maoni ili kuboresha zaidi matumizi ya AI katika lugha za Kiafrika.


Toa Maoni Yako:
0 comments: