
Dar es Salaam, Januari 30, 2026: Jimbo Kuu la Dar es Salaam limeingia katika majonzi kufuatia kifo cha Padre Paul Nsekela Mboje SABUNI, Paroko wa Parokia ya IPTL, aliyefariki dunia leo Ijumaa Januari 30, 2026, saa 10:31 alfajiri, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya kifo hicho imetolewa na Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambaye amesema Kanisa Katoliki limepoteza mtumishi mwaminifu, mchungaji mwenye upendo na padre aliyelitumikia Kanisa kwa unyenyekevu na kujitoa kwa hali ya juu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Padre Paul Nsekela Mboje alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo kabla ya kuitwa nyumbani kwa Baba wa Milele, tukio lililowaacha waamini, mapadre wenzake na jamii nzima ya waumini katika simanzi kubwa.
Ratiba ya mazishi yatangazwa
Askofu Mkuu Ruwa’ichi ametangaza kuwa mazishi ya Padre Paul Nsekela Mboje yatafanyika siku ya Jumatano, Februari 4, 2026, katika Makaburi ya Mapadri yaliyopo katika Kituo cha Hija cha Pugu, mkoani Dar es Salaam.
Ibada ya Misa ya Mazishi itaanza rasmi saa 3:00 asubuhi, ambapo waamini, mapadre, watawa na wageni mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria ili kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.
Rai yatolewa kwa waamini
Habari za msiba huo zimeombwa ziwafikie Maaskofu, Mapadri, Mashemasi, Watawa, waamini walei wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wenye mapenzi mema.
Kanisa limewahimiza waamini kuendelea kumuombea marehemu, wakikumbuka huduma yake kubwa kwa Parokia ya IPTL na Kanisa kwa ujumla.
Katika ujumbe wake wa faraja, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema Kanisa linaungana na familia na waamini wote katika kipindi hiki cha majonzi, likiwa na imani ya Kikristo kwamba kifo si mwisho bali ni mwanzo wa uzima wa milele.
Maombi ya Kanisa
Kanisa Katoliki limeendelea kutoa wito kwa waamini kuungana katika sala maalum kwa ajili ya marehemu, likitamka kwa pamoja sala ya:
“Raha ya Milele umpe Ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie. Apumzike kwa Amani; Amina.”


Toa Maoni Yako:
0 comments: