
Na Mwandishi Wetu, Manyara
Zaidi ya kaya 2,000 zenye uhitaji maalum mkoani Manyara zinatarajiwa kunufaika na msaada wa vyakula unaotolewa na Mati Foundation, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kampuni ya Mati Super Brands Ltd wa kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii inayozunguka maeneo ya uzalishaji na biashara zake.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada wa awamu ya kwanza kwa kaya 37 katika Kata ya Bagara, Wilaya ya Babati, Meneja wa Mradi wa Mati Foundation, Isack Piganio, amesema mpango huo unalenga kusaidia makundi yaliyo katika mazingira magumu, yakiwemo kaya zenye mahitaji maalum, ili kupunguza changamoto za maisha wanazokabiliana nazo kila siku.
Piganio ameeleza kuwa msaada huo wa vyakula ni sehemu ya dhamira ya taasisi hiyo kushiriki kikamilifu katika juhudi za kijamii kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo, huku akisisitiza kuwa lengo la sasa ni kuongeza wigo wa msaada huo ili kuwafikia walengwa wengi zaidi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kaya nyingi zaidi zenye uhitaji zinanufaika. Tunatarajia kufikia takriban kaya 2,000 ifikapo mwisho wa mradi huu wa msaada wa vyakula,” amesema Piganio.

Baadhi ya wanufaika wa msaada huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakipongeza juhudi zinazofanywa na Mati Super Brands Ltd kupitia taasisi yake ya Mati Foundation kwa kuwakumbuka wananchi wenye uhitaji, hususan wale wanaoishi katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho.
Wanufaika hao wamesema msaada wa vyakula walioupokea utawapunguzia kwa kiasi kikubwa changamoto za kimaisha, hasa katika kipindi cha ugumu wa upatikanaji wa mahitaji ya msingi, na wameishukuru kampuni hiyo kwa moyo wa kujali na kugusa maisha ya wananchi wa kawaida.
Viongozi mbalimbali wa Serikali waliokuwa mashuhuda wa zoezi hilo wameipongeza Mati Foundation kwa moyo wa kujitolea na ushirikiano wake na Serikali katika kutatua changamoto za kijamii, wakisema mchango huo ni mfano mzuri wa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya jamii.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa ushirikiano wa aina hiyo unasaidia kuimarisha ustawi wa jamii na kupunguza mzigo kwa Serikali katika kuwahudumia wananchi wenye uhitaji.
Mati Foundation ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyo chini ya kampuni mama Mati Super Brands Ltd, inayojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa vinywaji changamshi mbalimbali nchini. Miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ni pamoja na Strong Dry Gin, Sed Pineapple Flavoured Gin, Strong Coffee, Tai Original Portable Spirit, Tanzanite Premium Vodka na Tanzanite Royal Gin.
Kupitia Mati Foundation, kampuni hiyo imeendelea kutekeleza programu mbalimbali za kijamii zenye lengo la kuinua ustawi wa jamii na kuchangia maendeleo endelevu katika maeneo inayofanyia shughuli zake.













Toa Maoni Yako:
0 comments: