Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza rasmi uteuzi wa Mbunge na Diwani Mwanamke wa Viti Maalumu kufuatia nafasi zilizoachwa wazi baada ya vifo vya waliokuwa wakizishikilia awali.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume hiyo Januari 30, 2026, Jijini Dodoma, uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na kifungu cha 112 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343.
Katika uteuzi huo, Tume imemteua Ndugu Bengi Mazana Issa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Mbunge Mwanamke wa Viti Maalumu. Nafasi hiyo imekuwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge Mwanamke wa Viti Maalumu kupitia CCM, Ndugu Halima Idd Nassor, aliyefariki dunia Januari 18, 2026.
Aidha, Tume hiyo imemteua Ndugu Irene Linus Mwangara wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kuwa Diwani Mwanamke wa Viti Maalumu katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 25(1)(c) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288, pamoja na kifungu cha 113 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343.
Tume imeeleza kuwa uteuzi wa Diwani Mwanamke huyo umefanyika baada ya kukamilika kwa zoezi la uchaguzi wa marudio katika Kata ya Mzinga, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo uchaguzi huo uliahirishwa awali kutokana na kifo cha mgombea katika kata husika.
Taarifa hiyo imetolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, ikibainisha kuwa uteuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kikatiba na kisheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika kuhakikisha uwakilishi wa wananchi unazingatia sheria na taratibu zilizopo.
Hatua hiyo inaendelea kudumisha uwiano wa uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, sambamba na misingi ya Katiba na sera ya Serikali ya kukuza usawa wa kijinsia katika uongozi.



Toa Maoni Yako:
0 comments: