

Wagombea kutoka Tanzania Bara
Katika nafasi za Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wanaotokana na Bunge kutoka Tanzania Bara, Kamati Kuu imepitisha:
● Wanaume (nafasi 2): Paul Christian Makonda na Livingstone Joseph Lusinde
● Wanawake (nafasi 1): Asia Abdulkarim Halamga
Wagombea kutoka Zanzibar
Kwa upande wa Zanzibar, walioteuliwa ni:
Wajumbe wa NEC kutoka Bunge:
● Wanaume: Khamis Mussa Omar
● Mwanamke: Tauhida Cassian Galos
Nafasi nyingine za kitaifa
Katika nafasi ya Katibu wa Wabunge wote wa CCM, ameteuliwa Agnes Elias Hokororo.
Kwa nafasi za Wenyeviti wa Bunge, waliopitishwa ni:
● Najma Murtaza Giga
● Deodatus Philippo Mwanyika
● Cecilia Daniel Pareso
Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, walioteuliwa ni pamoja na:
Wajumbe wa NEC kutoka Baraza la Wawakilishi:
● Wanaume: Said Ali Juma na Hamza Hassan Juma
● Mwanamke: Lela Muhamed Mussa
Aidha, Kamati Kuu imepitisha pia majina ya wawakilishi wa CCM watakaoingia Bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo:
● Wanaume: Bakar Hamad Bakar, Dkt. Shaame Ali Ali, na Simai Mohammed Said
● Mwanamke: Fatma Ramadhan Mandoba
Nafasi ya Katibu wa Wawakilishi wote wa CCM imeenda kwa Machano Othman Said, huku nafasi za Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi zikiwapitisha Mahmoud Omar Hamad na Hudhaima Mbarak Tahir.
Mchakato wa Uchaguzi Mdogo Peramiho
Katika taarifa hiyo, Kamati Kuu imefanya pia uteuzi wa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho (Mkoa wa Ruvuma), na kumpitisha Dkt. Lazaro Killian Komba kugombea ubunge, kufuatia mamlaka ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 (Toleo la Julai 2025).
CCM yasema ni kuimarisha demokrasia ya ndani
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi huo una lengo la kuimarisha uwakilishi, kuongeza ufanisi wa uongozi na kuendeleza misingi ya demokrasia ya ndani ya chama, sambamba na kuhakikisha makundi yote yanapata nafasi stahiki katika vyombo vya maamuzi.
CCM imewahimiza walioteuliwa kuzingatia maadili, umoja na mshikamano, huku ikiwataka wanachama na wananchi kuendelea kukiamini chama katika kuendeleza maendeleo ya taifa.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, ametuma ujumbe mzito wa rambirambi kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mwanzilishi wa chama hicho, Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei, akimtaja kama mjenzi wa taifa, kiongozi wa mfano na hazina ya historia ya Tanzania.
Katika ujumbe wake alioutoa akiwa Gereza Kuu la Ukonga, Lissu amesema kifo cha Mzee Mtei ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na wanachama wa CHADEMA, bali kwa taifa lote la Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa taifa, uchumi na demokrasia.
Lissu ameeleza kuwa marehemu Mtei alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa misingi ya uchumi wa Tanzania baada ya uhuru, akihudumu kama Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na baadaye Waziri wa Fedha, ambapo jina na saini yake zilionekana kwenye noti za kwanza kabisa za taifa.
Akizungumzia uadilifu wake, Lissu amesema Mzee Mtei alionesha ujasiri wa kipekee wa kisiasa pale alipothubutu kumshauri Mwalimu Julius Nyerere kubadili sera za kiuchumi za Azimio la Arusha baada ya kubaini kuwa zilikuwa zimeshindwa, na baadaye akaamua kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Fedha kwa misingi ya dhamira na uaminifu kwa nchi.
“Huu ndio uzalendo wa kweli. Mzee Mtei hakutafuta madaraka, bali alisimamia ukweli na maslahi ya taifa,” amesema Lissu katika ujumbe wake.
Kuhusu mchango wake ndani ya CHADEMA, Lissu amesema marehemu alikuwa mfano wa uongozi wa kujitolea, kwani hakuwahi kupokea mshahara, posho wala kunufaika binafsi kupitia nafasi yake ya uongozi ndani ya chama.
Ameongeza kuwa Mtei aliimarisha utamaduni wa uongozi wa kupisha damu changa, alipostaafu uenyekiti wa chama mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 66, jambo linaloendelea kuifanya CHADEMA kuwa chama chenye misingi ya kidemokrasia.
Lissu pia amemsifu marehemu kwa kuchapisha kitabu chake cha maisha “From Goatherd to Governor” mwaka 2009, akisema kitabu hicho kimekuwa hazina muhimu ya historia ya kisiasa na kiuchumi ya Tanzania.
Akihitimisha ujumbe wake, Lissu amesema badala ya kuomboleza kifo cha Mtei, Watanzania wanapaswa kusherehekea maisha yake yenye maana, busara na mchango mkubwa kwa taifa, huku akimuombea apumzike kwa amani.
KAMPALA, UGANDA — Tume ya uchaguzi nchini Uganda imeitangaza rasmi ushindi wa Rais Yoweri Kaguta Museveni katika uchaguzi mkuu uliofanyika Alhamisi wiki hii, akipata kura 7,946,772, sawa na asilimia 71.65% ya kura zote halali zilizopigwa. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana Jumapili, Museveni ataendelea kushika nafasi ya urais hadi mwaka 2031 baada ya kushinda kwa tofauti kubwa dhidi ya wapinzani wake.
Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81, atahifadhi madaraka na kuendelea kuongoza nchi hii kwa awamu ya saba mfululizo hadi mwaka 2031.
Mpinzani wake wa karibu, Robert Ssentamu Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, alishinda nafasi ya pili akipata kura 2,741,238, sawa na asilimia 24.72%, akipigwa chini kwa zaidi ya asilimia 46 kutoka kwa Rais Museveni.
Tume ya uchaguzi ilibainisha kuwa jumla ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi huu ni 11,366,201, zikionyesha asilimia 52.50 ya idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kushiriki. Kura batili zilikuwa 275,353, sawa na asilimia 2.42% ya kura zote.
Matokeo hayo yalitangazwa katika mazingira ya mvutano mkubwa kisiasa na shut-down ya mtandao wa intaneti, ambayo ilifanywa na mamlaka kabla ya uchaguzi. Shughuli za uchaguzi zilikuwa na changamoto kadhaa ikiwemo matatizo ya mashine za utambuzi wa wapiga kura, na kusababisha matumizi ya rejista za karatasi kwa baadhi ya vituo vya kupiga kura.
Bobi Wine ametangaza kutokubali matokeo hayo, akieleza kwamba yalijazwa na udanganyifu na udhibiti wa hali ya usalama uliochochea upinzani kusambaratika. Mbali na hayo, kulikuwa na taarifa kuhusu mipaka iliyowekwa na vikosi vya usalama na kukamatwa au kuwekwa chini ya ulinzi wa karibu baadhi ya wakaazi wa upinzani na maafisa wa upigaji kura, madai ambayo mamlaka ya polisi imeyakanusha.
Rais Museveni, mmoja wa viongozi wanaotumikia muda mrefu zaidi barani Afrika baada ya kushika mamlaka tangu 1986, ameendelea kushikilia madaraka kupitia marekebisho ya katiba ambayo yaliondoa vikwazo vya vigezo vya umri na idadi ya mihula. Wafuasi wake wanaiona ushindi huu kama njia ya kuendeleza utulivu na maendeleo, huku wapinzani na mashirika ya haki za binadamu wakiendelea kusisitiza haja ya mageuzi ya demokrasia na uwazi wa vyombo vya uchaguzi.
Kwa upande wa Bunge, matokeo ya awali yanadhihirisha kushinda kwa wingi kwa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), huku upinzani ukipata viti vichache zaidi kuliko awali, lakini bado umbali mkubwa dhidi ya chama kilichoongoza nchi kwa miongo kadhaa.





















