Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, ametuma ujumbe mzito wa rambirambi kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mwanzilishi wa chama hicho, Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei, akimtaja kama mjenzi wa taifa, kiongozi wa mfano na hazina ya historia ya Tanzania.
Katika ujumbe wake alioutoa akiwa Gereza Kuu la Ukonga, Lissu amesema kifo cha Mzee Mtei ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na wanachama wa CHADEMA, bali kwa taifa lote la Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa taifa, uchumi na demokrasia.
Lissu ameeleza kuwa marehemu Mtei alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa misingi ya uchumi wa Tanzania baada ya uhuru, akihudumu kama Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na baadaye Waziri wa Fedha, ambapo jina na saini yake zilionekana kwenye noti za kwanza kabisa za taifa.
Akizungumzia uadilifu wake, Lissu amesema Mzee Mtei alionesha ujasiri wa kipekee wa kisiasa pale alipothubutu kumshauri Mwalimu Julius Nyerere kubadili sera za kiuchumi za Azimio la Arusha baada ya kubaini kuwa zilikuwa zimeshindwa, na baadaye akaamua kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Fedha kwa misingi ya dhamira na uaminifu kwa nchi.
“Huu ndio uzalendo wa kweli. Mzee Mtei hakutafuta madaraka, bali alisimamia ukweli na maslahi ya taifa,” amesema Lissu katika ujumbe wake.
Kuhusu mchango wake ndani ya CHADEMA, Lissu amesema marehemu alikuwa mfano wa uongozi wa kujitolea, kwani hakuwahi kupokea mshahara, posho wala kunufaika binafsi kupitia nafasi yake ya uongozi ndani ya chama.
Ameongeza kuwa Mtei aliimarisha utamaduni wa uongozi wa kupisha damu changa, alipostaafu uenyekiti wa chama mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 66, jambo linaloendelea kuifanya CHADEMA kuwa chama chenye misingi ya kidemokrasia.
Lissu pia amemsifu marehemu kwa kuchapisha kitabu chake cha maisha “From Goatherd to Governor” mwaka 2009, akisema kitabu hicho kimekuwa hazina muhimu ya historia ya kisiasa na kiuchumi ya Tanzania.
Akihitimisha ujumbe wake, Lissu amesema badala ya kuomboleza kifo cha Mtei, Watanzania wanapaswa kusherehekea maisha yake yenye maana, busara na mchango mkubwa kwa taifa, huku akimuombea apumzike kwa amani.



Toa Maoni Yako:
0 comments: