Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza zoezi maalum la upandaji miti kitaifa litakalofanyika tarehe 27 Januari, 2026 katika eneo la Bungi Kilimo, Kizimkazi, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, zoezi hilo lenye kaulimbiu “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti” linaakisi dhamira ya Rais Samia katika kulinda na kutunza mazingira, ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa zoezi hilo si tu la kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Rais, bali pia ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja na fursa kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kujenga utamaduni wa kulinda mazingira kwa kupanda miti mara kwa mara, akisisitiza kuwa ulinzi wa mazingira ni msingi wa maisha, maendeleo na usalama wa taifa.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imewahimiza wananchi, taasisi, mashirika pamoja na wadau wa mazingira kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki katika utekelezaji wa agenda ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kampeni ya kupanda angalau mti mmoja nyumbani, shuleni, kazini na katika maeneo ya jamii.

Taarifa hiyo imetolewa Zanzibar tarehe 22 Januari, 2026 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: