Na Mwandishi wetu, Ruvuma.
Wapiga Kura 127,632 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi wa kuchagua Mbunge katika Jimbo la Peramiho lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma na Kata ya Shiwinga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele ameyasema hayo leo Februari 25, 2026 mjini Songea Mkoani Ruvuma wakati akisoma risala maalum kuhusu uchaguzi katika jimbo na kata husika utakao fanyika kesho Februari 26, 2026 na kusema kuwa jumla ya vituo 373 vya Kupigia Kura vitatumika.
“Kati yao wapiga kura 120,780 ni wa Jimbo la Peramiho na wapiga kura 6,852 wapo katika kata ya shiwinga na jumla ya vituo 373 vya Kupigia Kura vitatumika, ambapo vituo 354 vipo Jimbo la Peramiho na vituo 19 vipo katika Kata ya Shiwinga Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi,”amesema Jaji Mwambegele.
Aidha, amesema kwa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Peramiho vyama vya siasa 15 vimesimamisha wagombea na kwa upande wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Shiwinga vyama vya siasa nane (08) vimesimamisha wagombea.
“Natumia fursa hii kuvikumbusha Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho Februari 26, 2026 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya zoezi la kupiga, kuhesabu na kujumlishia kura. Wasimamizi wa uchaguzi katika Jimbo na Kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.
Amesema, mawakala hao, wanawajibika katika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
Jaji Mwambegele amesema vituo vitafunguliwa saa 01:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni na kwamba ifikapo muda wa kufunga kituo saa 10:00 kamili jioni, kama wapiga kura bado wapo kwenye mistari, mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mtu wa mwisho na zoezi la upigaji kura litaendelea hadi wapiga kura walio kwenye mstari watakapomalizika.
“Baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kuondoka eneo la kituo cha kupigia kura; na Mpiga kura awapo kituoni, anatakiwa kufuata maelekezo yote atakayopewa na karani mwongozaji wapiga kura,”amesema Jaji Mwambegele.
Kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na taarifa zake zipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililopo katika kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi yake imeharibika, ataruhusiwa kupiga Kura kwa kutumia moja wapo ya vitambulisho cha Taifa NIDA, Leseni ya udereva au Pasi ya kusafiria (Passport).



Toa Maoni Yako:
0 comments: