Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewahimiza wanafunzi wa uandishi wa habari kusoma, kuielewa na kuizingatia Sheria ya Huduma za Habari ili kujijenga kitaaluma na kuepuka migongano ya kisheria wanapoingia kwenye tasnia ya habari.
Wakili Kipangula ametoa wito huo wakati akitoa mhadhara kwa wanafunzi wa Mwaka wa Pili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, uliofanyika Januari 30, 2026, chuoni hapo. Mhadhara huo ulilenga kuwaongezea uelewa wanafunzi kuhusu majukumu ya JAB na misingi ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.
Katika wasilisho lake, Wakili Kipangula ameeleza kuwa JAB ina jukumu la kusimamia ithibati ya waandishi wa habari nchini, kulinda taaluma ya uandishi wa habari na kuhakikisha maadili na weledi vinazingatiwa. Amesisitiza kuwa wanafunzi na waandishi chipukizi wanapaswa kuifahamu Sheria ya Huduma za Habari kabla ya kuanza kazi rasmi ili kujiepusha na makosa yanayoweza kuathiri taaluma yao.
Ameeleza pia kuwa ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari ni muhimu kwa wanafunzi wanapokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo (field), akisisitiza kuwa uwepo wa nyaraka hizo unatoa uhalali wa kisheria katika utekelezaji wa majukumu ya kihabari, hususan wanapokuwa wakikusanya habari katika maeneo mbalimbali.
Akijibu swali kutoka kwa wanafunzi kuhusu mafunzo katika vyombo vya habari vya vyuo, ikiwemo Mlimani Radio na Televisheni pamoja na SAUT, Wakili Kipangula amesema Sheria inatambua uwepo wa wanafunzi katika vituo hivyo kwa kipindi maalumu cha mafunzo. Amesema baada ya kukamilisha muda wa mafunzo kwa vitendo, wanafunzi wanapaswa kurejea katika ratiba yao ya kawaida ya masomo chuoni.









Toa Maoni Yako:
0 comments: