Na Mwandishi Wetu.

Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limetoa adhabu kali kwa timu za taifa za Senegal na Morocco kufuatia vurugu na vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyotokea wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyochezwa Januari 18, 2026 jijini Rabat, Morocco.

Katika adhabu hizo, Kocha Mkuu wa Senegal, Pape Bouna Thiaw, amefungiwa mechi tano za mashindano ya CAF na kutozwa faini ya Dola za Marekani 100,000 baada ya kupatikana na hatia ya mwenendo usio wa kiungwana na kuchafua taswira ya mchezo, kufuatia maamuzi yake ya kuwaamuru wachezaji wake kuondoka uwanjani.

Tukio hilo lilitokea baada ya Morocco kupewa penalti katika dakika za majeruhi, huku Senegal wakidai kuwa walinyimwa bao la halali muda mfupi kabla, pale mwamuzi Jean-Jacques Ndala alipositisha mchezo kwa madai ya faulo dhidi ya nahodha wa Morocco, Achraf Hakimi, kabla Ismaila Sarr hajafunga kwa kichwa. Baada ya penalti ya Panenka iliyopigwa na Brahim Diaz kuokolewa na kipa Edouard Mendy, mwamuzi alipuliza filimbi ya kuashiria mwisho wa mchezo, hali iliyozidisha sintofahamu.
Mchezo huo ulisitishwa kwa takribani dakika 17 baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani, kabla ya mshambuliaji nyota Sadio Mané kuwashawishi kurejea na mchezo kuendelea hadi dakika za nyongeza. Senegal hatimaye walitwaa ubingwa baada ya Pape Gueye kufunga bao la ushindi katika dakika ya nne ya muda wa nyongeza, na kuipa taifa hilo taji lake la pili la AFCON ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Kwa upande wa wachezaji, CAF imewafungia washambuliaji wa Senegal Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr mechi mbili kila mmoja kwa tabia isiyofaa dhidi ya mwamuzi. Aidha, Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limetozwa jumla ya faini ya Dola 615,000 ikijumuisha adhabu kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi.

Morocco nayo haikuachwa salama, ambapo beki nyota Achraf Hakimi amefungiwa mechi mbili za mashindano ya CAF, huku mshambuliaji Ismael Saibari akifungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Dola 100,000. Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) pia limetozwa faini ya Dola 200,000 kwa mwenendo usiofaa wa wachezaji wake uwanjani, pamoja na Dola 100,000 nyingine kwa wafanyakazi wa kiufundi na wachezaji waliovamia eneo la VAR na kuzuia kazi ya mwamuzi.

CAF pia ilitupilia mbali ombi la FRMF la kutaka matokeo ya fainali hiyo yafutwe au kubadilishwa, ikieleza kuwa hatua za kinidhamu zilitosha na matokeo ya mchezo yanasalia kuwa halali.

Licha ya adhabu hizo, CAF imethibitisha kuwa vifungo vyote vinahusu mashindano yake pekee, hivyo havitaathiri maandalizi ya Senegal wala Morocco kuelekea Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Katika ujumbe alioutoa kupitia mtandao wa Instagram, Kocha Thiaw aliwashukuru mashabiki kwa sapoti yao, lakini akawaomba kutoandaa michango ya kumsaidia kulipa faini hiyo, akisisitiza fedha hizo zielekezwe kwenye misaada ya dharura kwa wahitaji zaidi.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: