Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza mazingira ya kifo cha kijana mmoja aliyefariki dunia ndani ya nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema marehemu ambaye ametambuliwa kwa jina la Gidioni Mbwambo (34), mkazi wa Manispaa ya Morogoro, alikutwa amefariki dunia ndani ya chumba alichokuwa amepanga katika nyumba ya kulala wageni ya Kisanga, iliyopo Mtaa wa Nguzo, Kata ya Mazimbu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, tukio hilo lilitokea Januari 27, 2026 majira ya asubuhi, huku marehemu akiwa amefika katika nyumba hiyo Januari 26, 2026 na kupanga chumba namba 106.

Amesema tukio hilo liligundulika baada ya wahudumu wa nyumba hiyo kubaini dalili zisizo za kawaida nje ya chumba hicho, hali iliyosababisha kutoa taarifa kwa uongozi na baadaye kwa Jeshi la Polisi.

“Baada ya hatua za kiusalama kuchukuliwa na uchunguzi wa awali kufanyika, ilibainika kuwa marehemu alikuwa tayari ameshafariki dunia. Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo kamili cha tukio hilo,” amesema Kamanda Mkama.

Aidha, amesema taarifa za awali zinaonyesha marehemu alikuwa katika hali isiyo ya kawaida kabla ya tukio hilo, na uchunguzi unaendelea ili kupata ukweli zaidi.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni kuendelea kuzingatia taratibu za usajili na utambuzi wa wageni wao, ili kurahisisha hatua za kiusalama na uchunguzi pindi matukio yanapotokea.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: