
Mtaalamu wa tiba viungo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Jackline Mariki akitoa elimu kuhusu afya bora mahala pa kazi wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa Boharai Kuu ya Dawa (MSD) iliyoanza leo katika ofisi za MSD zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Mboyi Wishega akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wafanyakazi wa MSD wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya inayofanywa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika ofisi za MSD zilizopo jijini Dar es Salaam.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akimuonesha namna uwiano wa uzito na urefu unavyatakiwa kuwa Mfanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Christopher Komba wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya inayofanywa na wataalamu kutoka JKCI katika ofisi za MSD zilizopo jijini Dar es Salaam.Baadhi ya Wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya iliyoanza leo katika ofisi za Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha na Khamis Mussa
Baadhi ya Wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya iliyoanza leo katika ofisi za Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha na Khamis Mussa.
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
27 Januari, 2026
Wafanyakazi wanaotumia muda mwingi ofisini wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Daktari bingwa wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Theophilly Mushi, wakati akitoa mafunzo maalumu kuhusu namna ya kuzuia magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu katika kambi maalumu ya siku mbili ya upimaji wa afya kwa wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Akizungumzia hali ya afya nchini, Dkt. Mushi alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa asilimia 20 ya vijana nchini wanakabiliwa na shinikizo la juu la damu, huku kwa watu wazima kiwango hicho kikifikia asilimia 35. Alibainisha kuwa mazingira ya kazi za mijini, kukaa muda mrefu bila mazoezi, pamoja na kushindwa kupata muda wa kufanya uchunguzi wa afya, ni miongoni mwa sababu zinazoendelea kuchochea ongezeko la magonjwa hayo.
“Magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu yameendelea kuwa tishio kubwa kwa jamii, hususan kwa wafanyakazi wa mijini. Ndiyo maana tumefika MSD kutoa elimu ya afya mahali pa kazi, kufanya upimaji wa afya na kuwahamasisha wafanyakazi kuzingatia mazoezi, uzito wa mwili na lishe bora,” alisema Dkt. Mushi.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Tiba ya Viungo kutoka JKCI, Hospitali ya Dar Group, Jackline Mariki, alisema elimu ya afya mahali pa kazi ni muhimu ili kuwasaidia wafanyakazi kuepuka maumivu ya shingo, mabega na mgongo yanayosababishwa na kukaa vibaya au kwa muda mrefu.
“Tumewaelimisha wafanyakazi kuhusu namna sahihi ya kukaa, aina ya viti vinavyofaa, namna ya kupanga vifaa kazini na mbinu bora za kunyanyua vitu ili kujikinga na matatizo ya viungo,” alisema.
Wafanyakazi wa MSD waliopata mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata imewasaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kujali afya zao na kuchukua hatua za kinga mapema.
Afisa TEHAMA Mwandamizi wa MSD, Emanuel Kiunga, alisema elimu hiyo itamsaidia kubadili mtindo wa maisha na kuanza kufanya mazoezi mara kwa mara.
“Kinga ni bora kuliko tiba. Elimu hii imenifungua macho na itanisaidia kujilinda dhidi ya magonjwa ya moyo,” alisema.
Naye Dorothy Mtatifikolo alisema amejifunza umuhimu wa kupangilia muda wake ili kupata nafasi ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuzingatia ushauri wa wataalamu kwa ajili ya kulinda afya yake.
Kambi hiyo ya siku mbili ya upimaji na elimu ya afya ni sehemu ya jitihada za JKCI kuimarisha huduma za kinga na kuongeza uelewa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza mahali pa kazi.





Toa Maoni Yako:
0 comments: