Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

ALIYEKUWA mfanyakazi wa Kampuni ya Mabasi ya NBS, Mzee Nassor Hamdan Seif (NBS), amefariki dunia leo asubuhi, na kuacha huzuni kwa familia, ndugu, jamaa na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia na uongozi wa NBS, mwili wa marehemu kwa sasa upo Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, na unatarajiwa kusafirishwa leo jioni kwa ndege kwenda mkoani Tabora kwa ajili ya mazishi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mazishi ya Mzee Nassor Hamdan yatafanyika kesho saa 7 mchana mkoani Tabora, nyumbani kwao, ambapo ndugu, jamaa na marafiki wanatarajiwa kuhudhuria kumpa heshima ya mwisho.

Aidha, Kampuni ya Mabasi ya NBS imetangaza kuweka mabasi maalum kwa ajili ya kusafirisha waombolezaji wanaotaka kwenda Tabora kushiriki mazishi hayo. Mabasi hayo yatakuwa Temeke, jijini Dar es Salaam, na yataondoka leo jioni kuelekea Tabora.

Imesisitizwa kuwa usafiri huo ni bure kwa waombolezaji wote na utahusisha safari ya kwenda na kurudi, ikiwa ni sehemu ya mchango wa NBS katika kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki cha majonzi.

Familia ya marehemu imewashukuru waombolezaji wote kwa michango, dua na faraja wanayoendelea kutoa, na imetoa wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana katika kumpa marehemu heshima ya mwisho.

Marehemu Nassor Hamdan atakumbukwa kwa mchango wake katika sekta ya usafiri na kwa ushirikiano wake mzuri na jamii aliyokuwa akiishi nayo. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: